526; HEKIMA: Sumu Niliyowekewa Kwenye Chakula.

jacobmushi
4 Min Read

“Ilikuwa ni siku za mwisho wa mwaka ambapo tulikuwa na utaratibu wa kwenda kuwasalimia ndugu na jamaa ambao hatujawaona miaka mingi.

Katika kuwatembelea ndugu jamaa na marafiki wengi siku moja nikapitia kwa ndugu mmoja ambaye hatukuonana muda mrefu sana.

Huyu ndugu baada ya kunipokea alinisisitiza sana nile chakula. Nilimkatalia kwasababu nimepita nyumba nyingi na nimeshakula.

Lakini kwa maneno yake matamu nikajikuta nakubaliana nae. Akaniwekea chakula kingi kweli.

Tulikuwa tumekaa nje chini ya mti mkubwa wa mwembe, pembeni yangu nilizungukwa na kuku mwenye vifaranga aliekuwa anatafuta chakula.

Wakati nasubiria mwenyeji huyu aniletee maji ya kunawa ili nile chakula kile nikaona si vibaya nikiwatupia hawa vifaranga chakula kidogo tu (ulikuwa wali).

Wakati naendelea kusubiria maji ya kunawa akapita mtu kwenye njia iliyopakana na nyumba ya mwenyeji wangu. Akanisalimia nilikuwa nimemsahau kabisa. Kumbe nilisoma nae shule ya msingi.

Nikaondoka chini ya mwembe ule kwenda kumfata kwa karibu, wakati huo mwenyeji wangu hajaleta maji sijui ni nini kilimchelewesha.

Kumbe wakati naondoka yule kuku mwenye vifaranga akarukia juu ya kiti nilichoweka chakula akakimwaga na akaendelea kula na wanawe. Nikageuka kurudi kumfukuza lakini chakula chote kilimwagika.

Nikasema labda huyu kuku ndie alitakiwa ale hiki chakula. nikaendelea na kusalimiana na yule ndugu. Akaondoka, wakati narudi na mwenyeji nae alikuwa anakuja na maji. Kumbe chakula kuku ameshakimwaga.

Akasema anakwenda kunipakulia kingine, nikamkatalia nikamwambie ulinilazimisha sana ndio maana kimemwagika.

Tukaagana nikaondoka.

Kumbe Baada ya kuondoka masaa kadhaa baadae nakuja kuambiwa yule kuku pamoja na vifaranga wake wote walikufa.

Chakula nilichotakiwa kula kiliwekwa sumu ambayo ingeniua taratibu.

Mungu ni mkubwa sana akaniokoa na kifo, kwa namna ya ajabu.”

Nataka ujifunze hapa kitu kikubwa katika maisha yako rafiki.

Kuna amengi hutokea kwenye maisha tunayaona kama ni mabaya au ni mikosi lakini wakati mwingine ni mipango ya Mungu kutuokoa na tusivyoviona.

Unaweza kuachwa na gari kumbe uliokolewa na ajali mbaya.

Unaweza kuachwa na mpenzi kumbe umeokolewa na tatizo la maisha.

Unaweza kutengwa na ndugu kumbe ni ili uweze kukutana na watu watakaoweza kukusaidia.

Hakuna kitu kinatokea kwa bahati mbaya, yule mwenyeji wangu hakuchelewa kuniletea maji kwa bahati mbaya japo ningeweza kumlaumu.

Yule ndugu niliesoma nae aliepita akasababisha chakula kumwagwa na kuku hakupita tu kwa bahati mbaya. Alipita kwa kusudi maalumu. Huenda alikuwa apite mahali pengine lakini akasukumwa kupita njia ile bila hata yeye kujua.

Yule kuku na vifaranga vyake sio kwamba walishindwa kwenda kutafuta chakula shambani, hapana walikuja pale chini ya mwenye kwa kusudi la Mungu la kuniokoa.

Lolote baya linalotokea kwenye maisha yako usiwe mwepesi kulalamika, tafakari jiulize ni kwanini haya yanatokea. Ni kwa kusudi lipi?

Kuna mengine yatatokea leo ili tu uje utimize kusudi miaka 20 ijayo.

Musa hakuwekwa kwenye kisafina bahati mbaya, alikuwa anaandaliwa.

Yusufu hakuchukiwa na ndugu zake bahati mbaya yalikuwa ni makusudi maalumu ambayo yalikuja kuonekana miaka kadhaa mbele.

Wewe unapitia ugumu leo unakata tamaa, unapitia changamoto fulani leo unakata tamaa. Ndoto zako unaacha kuzifuatailia kumbe yale yanayotokea yanakuandaa kuelekea kwneye ndoto na kusudi lako.

Nataka Ujifunze kwenye kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako kila siku.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
4 Comments

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading