Ugumu wa Maisha wa Kujitakia.

Ni vizuri ukatambua kwamba ili uweze kufika viwango vya juu Zaidi ya hapo ulipo sasa hivi lazima ukubali kufanya maamuzi magumu. Maisha yako hayatakiwi kuwa magumu Zaidi ya inavyotakiwa, wewe mwenyewe kuna sehemu umesababisha kuongezeka kwa ugumu. Kushindwa kufanya maamuzi magumu lazima itakugharimu ugumu Zaidi wa Maisha yako.

Upo kwenye mahusiano ambayo binafsi unayaona ni mabovu kila siku mnagombana ukishindwa kufanya maamuzi magumu mapema. Jiandae kabisa kuja kuwa na Maisha magumu Zaidi kwenye ndoa. Ni lazima ukubali kufanya maamuzi magumu ili kutengeneza Maisha ambayo sio magumu kuliko inavyotakiwa kwenye ndoa yako.

Hautaki kuweka akiba, kila fedha unayopata inaingia kwenye matumizi yote jua kabisa unajitengenezea ugumu wa Maisha yako muda ambao sio mrefu sana. Lazima ukubali kujenga tabia ya kuweka akiba na uweze kupunguza matumizi ya hovyo ya pesa.

Umekubali mwenyewe kujiingiza katika michezo mibaya ya kubeti halafu unategemea Maisha yako yaje kuwa kama ya mtu mmoja hivi maarufu. Ndugu yangu unapoteza muda, ili Maisha yako yawe na unafuu lazima ukubali kuwekeza katika vitu ambavyo vinazalisha. Lazima ukubali kuwekeza katika vitu ambavyo vinaongeza thamani kwa wengine.

Ugumu wa Maisha ndio ni kipimo cha akili kwasababu hapo ndipo unatakiwa ujue kufanya maamuzi sahihi ya kukutoa huko kwenye ugumu. Kama utaendelea kubaki kwenye ugumu huo wa Maisha maana yake ni kwamba wewe akili yako ndio umeipima sasa ilivyo. Lazima ukubali kufika mahali unasema sasa basi, hii hali siitaki tena kwenye Maisha yangu. Aina hii ya shida sitaki tena kuisikia, sitaki tena kukopa pesa za kula, sitaki tena kukopa pesa nikalipe madeni. Lazima useme sasa basi nataka nitoke nisogeee viwango vingine.

Ugumu wa Maisha wa kujitakiwa ni kuamua kuingia kwenye Maisha ya kuiga wengine. Mfano wewe una marafiki zako wote wakiona simu mpya imetoka lazima wanunue cha ajabu ni kwamba wewe hujui hata pesa wanatoa wapi lakini wewe upo tayari ukakope ili ufanane nao. Ndugu yangu hapo unajitengenezea ugumu wa Maisha mwenyewe.

Ugumu wa Maisha wa kujitakia ni pale unapoishia kusema sina mtaji, sina mtaji wakati unajua kabisa hilo neno sina mtaji haliwezi kukupa mtaji. Unaona aibu kuanza biashara kwa shilingi elfu 20 kwasababu itaonekana ni ndogo sana. Maisha yakiwa magumu hapo umejitakiwa mwenyewe, ni bora upate faida ya shilingi elfu mbili uliyotafuta mwenyewe kuliko elfu kumi uliyopewa bure.

Ugumu wa Maisha wa kujitakia mwingine ni pale unaposhinda kwenye mitandao ya kijamii kutwa kuchwa ukitoa maoni kwenye kurasa za udaku bila kujua hakuna anaejali Maisha yako wewe. Huna biashara yeyote unayofanya lakini kila siku unapata hela ya kununua vifurushi vya kufuatilia udaku. Makala kama hizi za kukufungua ukikutana nazo hausomi hata kidogo. Lazima ujitengenezee ugumu wa Maisha.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Chukua Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading