Habari Rafiki yangu, leo ni siku ya pekee sana kwangu, kwani ndio siku nilizaliwa, naikumbuka hii tarehe na ninafurahi pamoja nawe. Nimekuandikia Makala hii uifurahie pamoja nami katika kukumbuka siku hii.

Siku moja nilikuwa napita kwenye jingo lililokuwa linajengwa maeneo ya Mlimani City, jingo lile ni refu san ana linatamanisha. Wakati natafakari nikapata mawazo ambayo nimekuwa natamani nikuandikie siku moja ujifunze, hatimae leo nimeweza kukuandikia Makala hii ujifunze yale niliyojifunza wakati napita jirani na jingo lile.

Niliwaza kwamba kuna watu wengi kama wanapita maeneo yale au wanaweza kuona jingo lile kwenye picha na wakalitamani kama mimi niliyoona linavutia. Nikawaza Zaidi hivi watu hawa watakuwa wanawaza nini ndani ya vichwa vyao baada ya kuliona jingo hili zuri? Nikajiwa na majibu kama manne hivi ambayo nakwenda kukushirikisha.

a/ Wapo watakaowaza Kwamba Haya ni Mambo ya Matajiri Tu Mimi Maskini Nitaishia Kutazama kwenye Picha….

Ukweli haya mawazo huenda ulikuwa unawazaga vinapoPita mbele yako vitu mbalimbali ambavyo huna uwezo navyo au unaviona ni vya gharama sana.

Umekuwa unajiweka kwenye kundi la watu ambao hawastahili vitu fulani kutokana na hali uliyonayo.

b/ Wapo ambao watatamani sana wangepata ajira kwenye ofisi mbalimbali ambazo zitakuwa ndani ya Jengo Hili.

Ndio kuna ambao akili zao kitu cha kwanza watawaza au watatamani endapo wangeajiriwa hapo ili kila siku wawe wanapandisha kwenye lifti ?.

c/ Wapo wengine watawaza kufungua biashara zao kwenye hili Jengo.

Ndio nikwambie ukweli hata mimi pia niliwaza hivi nikasema nitakuja kuuliza bei za vyumba vya juu juu kabisa.

d/ Wapo kundi la mwisho ambalo na mimi nilikuwepo, hawa watawaza hivi kumiliki Jengo kama hili nitahitaji kuwa na pesa kiasi gani? Gharama za hili Jengo zima ni Tsh ngapi?

Watajiuliza hivyo na ipo siku watapata majibu ya maswali yao au ya kile walichokuwa wanatamani.

Naomba nikuulize swali Rafiki wewe upo kundi gani? Unatamani kuwa sehemu ipi? Je mawazo yako yameishia wapi?

Ni mambo mangapi umekuwa unajiwekea ukomo wa kufikiri kuwezekana? Je umekuwa unajiona wewe ni kiwango Fulani hivi hivyo huwezi kuwaza hayo mambo ni makubwa sana.

Inawezekana hata ukisikia zile ndoto za kuwa bilionea unazikataa kabisa unasema mimi bado sijafikia kuwaza hayo makubwa hivyo.

Nataka nikwambie mtu atapata kile ambacho anakipigania, kile ambacho umeona unastahili ndicho haswa utakipata. Ikitokea umeenda Zaidi basi itakuwa ni bahati tu.

Usijipimie viwango kutokana na hali uliyonayo sasa hivi.

Usijiwekee kwenye kundi Fulani kwasababu eti sasa hivi hela ya kula ni shida.

Usione wewe huwezi kuwa bilionea kwasababu tu eti sasa hivi hujaweza kumsaidia mtu elfu kumi.

Usione kwamba ni vibaya kuwaza mambo makubwa ambayo hujayafikia.

Ndio ni kweli unaishi kwenye nyumba ya kupanga mpaka sasa lakini hiyo sio sababu ya wewe kuacha kuwaza kumiliki ghorofa refu kuliko yote hapa nchini. Hali uliyonayo sasa hivi haitabaki milele, chochote kile unachotamani kuwa usiogope kuwaza au kuandika.

Ndoto za wengi zimekuwa zinazimwa kwa woga wa kuwaza, unaogopa hata kuwaza kufikia level za kina Moo Dewji eti kwasababu tu sasa hivi kula ni shida. Sasa kwani ukiwaza kufikia level za Moo utaishiwa hela ya kula? Si ndio juhudi za kutafuta zitaongezeka? Acha woga Rafiki yangu. Pandisha viwango vyako vya Imani.

Hakuna ambaye amewahi kutimiza kitu ambacho hajakiwaza kwenye kwenye akili yake. Anza kutengeneza mawazo makubwa nenda mbali Zaidi ya wengine wanavyowaza.

Usiogope Ndoto Yako Inawezekana. Kile unachotamani kitokee kwenye Maisha yako, kinawezekana badili tu fikra zako. Vile viwango ulivyokuwa unasema hivi sio level zangu bado zinaweza kuwa level zako badili tu unavyofikiri. Ona kuwezekana kwenye chochote kile unachokitamani.

MWANZO WA MAMBO YOTE NI KWENYE FIKRA ZETU.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

4 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading