Kungekuwa hakunaga kufa kwa namna ninavyoona wanadamu hasa wa Africa wangekuwa wavivu sana kuliko viumbe wengine wote. Nadhani kungekuwa hakuna ambaye anajishughulisha sana kwasababu hakuna kinachomfanya afikirie mbali. Kifo kipo ili kuongeza thamani ya uhai wa mtu. Kama kungekuwa hakuna kifo thamani ya uhai ingekuwa ni ndogo sana. Wandamu wangekuwa hawajali sana kama ambavyo sasa hivi baadhi wanajali na kufanya mambo makubwa. Mfano unaumwa na unajua utapona tu, una njaa lakini unajua ipo siku utapata chakula, hakuna ambaye angejali sana. Lakini mtu akizidiwa atakimbizwa hospitali ili kuokoa Maisha yake. Ukikosa chakula utafanya bidi kukitafuta ili usije kufa njaa.

Kifo kipo kutufanya kufikiria ni aina gani ya Maisha tunataka yaendelee kuwepo hapa duniani baada ya sisi kufa. Watu waliokosa matumaini ya Maisha ndio hawajali chochote kuhusu kesho yao wala ya baada ya wao kuondoka hapa duniani.

Kama kila binadamu angeweza kutambua kile ambacho kipo ndani yake na akaweza kukiishi katika uwezo wake wa juu sana basi dunia hii ingekuwa sehemu nzuri sana ya kuishi kuliko hapa tulipo sasa. Nikiwa na maana kwamba kuna watu wengi sana wameondoka duniani na vitu vingi sana vizuri mno vilivyokuwa ndani yao.

Kuna matatizo tunayapitia sasa hivi kumbe kuna mtu mmoja alishazaliwa ili aje kuleta suluhisho lakini akaondoka bila ya kutambua. Kuna changamoto nyingi watu wanapitia maeneo mbalimbali duniani inawezekana kabisa wewe unaesoma Makala hii kuna kitu kipo ndani yako ukiweza kukigundua utaleta msaada mkubwa kwa wengi.

Kila jambo ambalo unalifanya kila siku lina matokeo yake kwa baadae. Matokeo yanaweza kuwa ni kusahaulika kabisa kama uliwahi kuwepo hapa duniani ama kukumbukwa daima. Wapo watu wengi sana ambao historia zao zinatumika kama mifano kutokana na aina ya Maisha waliyoishi. Wapo waliofanya maovu kupindukia na wapo waliofanya mambo mema.

Mojawapo ya watu ambao wameweza kuendelea kuishi pamoja na kwamba miili yao hatunayo tena hapa duniani ni Wanamuziki waliofanya kazi zao kwa ubora wa hali ya juu mfano ni Bob Marley, Wapo wagunduzi wa vitu vingi ambavyo tunatumia sasa. Wapo viongozi wa kisiasa, waandishi, wanafalsafa, waigizaji, wachezaji na wengine wengi ambao unawafahamu. Ukweli ni kwamba hata wewe unaweza kuja kuwa mmoja wa watu ambao kazi zao hazitasahaulika hapa duniani.  Unachotakiwa kufanya ni kugundua ni nini kipo ndani yako na uanze kukiishi na kufanya kwa ubora wa hali ya juu.

Kila mmoja ana uwezo mkubwa sana ndani yake. Wanadamu pekee ndio tuliopewa uwezo wa kugundua vitu mbalimbali. Kwa kutazama kule ulipotoka hadi ulipo sasa unaweza kugundua kwa urahisi vitu gani ambavyo ulikuwa unapenda kuvifanya na ukivifanya vinakuwa na matokeo mazuri sana na moyo wako unasikia furaha.

Hakikisha Unafanya Vitu Hivi.

Jigundue Wewe ni nani.

Ili uweze kupata kitu ambacho utakisimamia na kukipigania hadi unakufa lazima ujue wewe ni nani, ulikuja hapa duniani kufanya nini, na unatakiwa ufike wapi. Huu ndio mwanzo wa wewe kuweza kuishi milele kwa kupitia yale ambayo yaliyowekwa ndani yako.

Chochote Unachokifanya Kifanye kwa Ubora wa Hali ya Juu Sana.

Ukikutana na fursa ifanye kwa ubora wa hali ya juu kiasi kwamba watu wakija waweze kujua hii kazi imefanywa na wewe. Popote unapopita hakikisha kunabaki na alama yako. Kwasababu wewe ni wa pekee basi upekee wako uonekane kwenye kazi za mikono yako.

Usijiweke Wewe Mbele Weka Mbele Kazi Zako na Kuwasaidia Wengine.

Kikubwa ili uweze kubakia na kumbukumbu ya kudumu wekeza nguvu zako katika kuwasaidia watu na sio kwa maslahi yako wewe binafsi. Wapo wengi sana wanahitaji hicho kilichopo ndani yako, endelea mbele ipo siku wengi wataanza kuona thamani ya kile kilichopo ndani yako.

Anza na Mtu Mmoja na Hakikisha Kile Unachokifanya Kimeweza Kumsaidia Hadi Akaridhika.

Usikimbilie kutaka kila mtu aanze kukujua mapema sana, anza na mtu mmoja hakikisha umeweza kumsaidia matatizo yake. Huyu mmoja ndio atakuwa zao la watu wengine wengi nyuma yake. Kama unaimba basi embu imba mtu mmoja akuelewe, kama unaandika andika hadi mtu mmoja akuelewe na asaidike na maandishi yako. Kama unafundishia fundisha mtu mmoja ahadi aweze kufanikiwa. Kama unatatua tatizo tafuta mtu mmoja mtatulie tatizo lake hadi aridhike kisha uanze na wengine na wengine.

Fanya Kila Siku

Ukishajua unatakiwa kufanya nini hapa duniani basi hakikisha kila siku kuna kitu unafanya ambacho kinaongeza thamani yako. Iwe ni kujifunza, kufanya utafiti, na mengine ambayo utayafahamu.

Jifunze Sana Kuhusu Kile Unachokifanya.

Hakikisha unachimba sana kwa undani kile unachokifanya hakikisha unajua wengi waliofanikiwa wamepitia njia gani. Ni vitu gani hasa ukivifanya vinaleta matokeo, ni mambo gani wengi walifanya na wakafeli. Usikubali kujua vitu vichache wakati una uwezo wa kujua vitu vingi.

Usipoteze Muda wako kusikiliza Kelele za Nje.

Duniani kuna kelele nyingi kuna watu wengi ambao wapo tu wao hawajatambua kwanini wapo hapa duniani. Kazi yao kubwa ni kufuatilia watu wanafanya nini ili wawavunje moyo. Wengine wanaweza kuwa marafiki, ndugu, na wengine hata usiowajua kabisa, watakuja tu na kuanza kukuelekeza jinsi ya kufanya. Wataanza kukukosoa na kusema hata wasioyajua. Usipoteze muda wako weka nguvu zako kwenye kile ambacho umeamua kufanya.

Jambo ambalo unatakiwa kutambua ni kwamba ili uweze kutengeneza historia ambayo itaishi milele hapa duniani unapaswa kuweka nguvu nyingi sana katika kuwasaidia watu. Usijifikirie wewe wafikirie wengine. Kwenye Biblia kuna neno linasema “Yeyote atakaekubali kuyapoteza Maisha yake kwa ajili ya wengine atakuwa ameyaokoa. Na yule atakaejaribu kuyaokoa Maisha yake atakuwa ameyapoteza” yaani mtu mbinafsi peke yake ndie anajiwaza yeye mwenyewe, na kila analofanya anafanya kwa ajili yake. Mara zote mtu ambaye anawaza Zaidi juu ya wengine hufikia mafanikio makubwa sana.

Lazima ukubali kujitoa sana kwa ajili ya wengine. Kila ulifanyalo waweke wengine mbele matokeo yake ni makubwa sana na yanagusa Maisha yako moja kwa moja.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

2 Responses

  1. AHSANTE KWA JUMBE ZAKO NZURI NAUHAKIKA KWAMBA UFAHAMU WANGU UNAFUNGUKA SANA . OMBI LANGU NI HICHO KITABU CHA SHILINGI ELFU MBILI, NITAKIPATAJE NA MIMI NIKO MOROGORO.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading