Habari za leo Rafiki na mwanamafanikio mwenzangu. Ni matumaini yangu bado unapambana na hujakata tamaa. Ni muhimu sana uendelee mbele usikubali kubaki hapo ulipofikia. Kila unachokifanya kina mchango mkubwa sana katika mafanikio yako hata kama hutaona leo au kesho. Matokeo yanaweza kuonekana hata baada ya miaka kadhaa. Hivyo usife moyo wala kurudi nyuma bado safari ni Mbichi.

Leo tunatazama mambo ambayo yanatuzuia sisi tushindwe kufanikiwa kama watu wengine tunaowafahamu. Mafanikio yapo katika Nyanja nyingi sana kutegemeana na mtu anafanya nini. Tunapozungumzia mafanikio mwalimu akisikia ataelewa na kutafsiri kutokana na ualimu, Mchungaji atatafsiri na kuelewa kwa namna yake pia. Ni vizuri sana uakatambua upo upande gani ili uweze kupata tafsiri na uelewa sahihi kutokana na jambo linalozungumziwa.

Kinachokufanya wewe usifike kule unapotaka sio Rangi yako nyeusi, Sio kwasababu wewe ni Mwafrika Lah! Ni haya hapa yafuatayo:

Weusi katika Ufahamu wako.

Kinachotusumbua wengi sio rangi yetu ya nje bali ni weusi uliokaa ndani ya ufahamu wetu. Kwa namna gani sasa? Inawezekana hujanielewa. Tangu ukiwa mdogo ulikua unaimbiwa nyimbo za historia za mababu zetu walikua watumwa, tulitawaliwa na wakoloni. Waafrika ni maskini, na mengine mengi. Ukitaka uanze kuona wewe ni mtu wa pekee ni pale tu utakapoondoa hali hii ndani ya akili yako. Wewe na mzungu hakuna kitu cha tofauti katika akili. Tofauti ni rangi tu za ngozi zetu hata wewe unaweza kufanya jambo kubwa sana kuliko mtu yeyote duniani. Haijalishi babu yako alikua mtumwa au alitawaliwa. Anza sasa kufuta weusi huo unakuonyesha kwamba kwenu ni maskini na hamuwezi kufanikiwa. Mabadiliko yanaanzia ndani ya ufahamu wako.

SOMA: NGUVU YA TAARIFA KATIKA MAONO NA NDOTO ZAKO

Maneno uliyonenewa.

Tangu unazaliwa hadi ulipofikia umri wa kujitambua, kuna maneno mengi yalisemwa sana juu yako. Mengine ni mazuri na mengine ni mabaya. Yanayokukwamisha ni yale mabaya, nakumbuka nikiwa mdogo sana niliona wazazi wakiwaita watoto wao ni wajinga, wapumbavu, hawana akili, na mengine mengi yasiyofaa. Na haya hutokea pale mtoto anapokosea. Hii ni hatari sana kwani maneno haya huenda kujijenga katika ubongo wa kumbukumbu wa mwanadamu hivyo kila anapokua maneno yale huanza kufanya kazi ndani ya maisha yake. Anapofeli darasani au kwenye maisha hukumbuka kwamba yeye hana akili. Kama ulipitia hali hii anza leo kujitengenezea upya ufahamu wa mafanikio. Kila siku asubuhi ukiamka jinenee maneno ya ushindi. Sema mimi ni Mshindi, ninakwenda kufanikiwa. Ninatimiza ndoto zangu, na mengine mengi. Unaposema hivi akili yako itakupa nguvu hata pale unapopitia magumu.

Kutokujikubali.

Kutokujikubali kunachangiwa Zaidi na yale maneno uliyonenewa tangu ukiwa mdogo. Maneno hasi yanakufanya ujione wewe hufai, hustahili vitu Fulani. Hustahili kufikia mambo Fulani makubwa na mengine mengi. Pale unapoona bado hujaweza kufanya jambo Fulani huna uzoefu wa kutosha na kadhalilka. Acha kuanzia leo tabia hii ya kutokujikubali inakurudisha nyuma sana na inakuzuia wewe kufikia mafanikio. Mara nyingine unaweza kufanya jambo lako zuri sana lakini ukashindwa kulitoa mbele za watu kwa hofu ya kukataliwa unaogopa kwamba watu watakukosoa. Inawezekana una kipaji kizuri sana lakini unaogopa watu watakuonaje. Watu watakucheka kwasababu bado hujajua vizuri. Acha mara moja na anza ukichekwa endelea mbele ipo siku utaweza kufanya vizuri. Ukisema ukae usubiri hadi siku utakapokua bora haitakaa itokee. Kila mmoja anakua bora kwa kukosea. Unapofanya jambo ukakosea ndipo unapata nafasi ya kujifunza na kurekebisha makosa yako.

Uvivu

Uvivu unakusababisha wewe usifikie mafanikio yako hasa pale unapoanza kuahirisha mambo kidogo kidogo. Leo umesema utafanya jambo Fulani mara linatokea jambo lingine ambalo halikuwepo kwenye mpango wako unalifanya. Unaamua kufanya jambo Fulani badala ufanye ufikie mwisho unachagua mambo marahisi unayafanya yale magumu na ya muhimu unayaacha. Lazima utabaki hapo hapo ulipo. Amua leo kuachana na tabia ya uvivu ili uweze kufikia mafanikio.

SOMA: KUJITETEA NA KUTOA SABABU

Kuridhika na Maisha.

Hili ni jambo ambalo hua napenda kulipigia kelele sana kila siku. Watu wengi hatuna mabadiliko katika maisha yetu sio kwasababu ya ugumu wa maisha ila ni kwasababu tumekubaliana na hali tulizonazo. Kwa kuwa tayari mtu ana uhakika wa chakula, malazi na zile huduma za muhimu za familia yake basi anaacha kufikiri Zaidi anafikiri maisha ndio yamefika mwisho. Bado dunia inahitaji ufanye kitu kabla hujaondoka. Hutakumbukwa kwa nyumba nzuri uliyojenga, gari lako zuri ulilonunua au chochote kizuri ulichokimiliki hapa duniani. Utakumbukwa kwa yale uliyoyaacha kwenye maisha ya wengine wengi. Anza leo kutambua kwanini upo duniani na usikubali kuondoka hivi hivi.

Afrika ni yetu sote na tunatakiwa tupambane kwa pamoja ili kuleta mabadiliko.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading