HITAJI MSAADA KUTOKA KWA MUNGU PEKE YAKE

jacobmushi
By jacobmushi
7 Min Read

MAHALI SAHIHI PA KUPATA MSAADA WAKATI WA SHIDA AU TATIZO.

Na Steven Mshiu I.

Kipindi fulani niliazimia kufanya kufanya biashara fulani, na kwa kuwa ilikuwa ni biashara nikaamua kumshirikisha mmoja wa aliyekuwa rafiki yangu katika lile eneo nililokuwepo.

Baada ya kumshirikisha tu, akaniambia nyie ndio wachaga mliotumwa pesa mjini. Kwa kweli utatoboa tu. Nilifurahia kwa namna alivyonitia moyo na kunihamasisha kufanya biashara ile.Siku iliyofuata akanifuata asubuhi na mapema sana. Nikaanza kuwaza kuna nini mbona amenifuata asubuhi na mapema hivi? Ikabidi nimsikilize. Akaanza kuniambia, “Sasa we mchaga sikia, kabla hujaanza kufanya twende nikupeleke kwa mtaalam mmoja hivi yuko pale Mlandizi. Yaani huyu Bibi ni balaa. Atakupa dawa yani ukianza hiyo biashara we mwenyewe utaona maajabu yake”

Nilitumia kama dakika mbili hivi kumtafakari yule rafiki kabla ya kumjibu chochote. Huku nikimsihi Mungu anipe neema ya kuongea naye. Baada ya ukimya wa dakika chache Nikamjibu tu kwa ufupi kuwa sijawahi na sitakaa nijaribu kwenda kwa mganga. Yesu wangu ananitosha kabisa na siwezi kuweka tumaini wala kutegemea msaada wa namna ya kibinadamu. Biblia inasema Mungu wangu ni MUNGU anaenifundisha kupata faida na wala si hasara.

Aliondoka huku akiwa ameweka mikono nyuma na kwa kuwa alikuwa ni dereva bodaboda tangu siku hiyo hakuwahi kunipa lift tena hadi naondoka katika mji ule.Kuna watu ambao wanategemea msaada wao katika vitu.

Kuna watu wanaamini msaada upo kwa wachawi na waganga wa kienyeji. Siku tu bundi akilia nyumbani kwako umeshawaza tofauti.

Unafanya biashara lakini unategemea hirizi. Kana kwamba kupitia hilo hirizi biashara yako itaenda vizuri. Kuna mwingine ametafuta kazi kwa muda mrefu sana lakini amekosa. Amepoteza tumaini kabisa. Hivyo anafikia hatua ya kwenda kwa waganga ili kutafuta msaada. Lakini kiukweli huwezi kupata msaada wa kutosheleza kutoka kwa waganga wa kienyeji au wachawi.

Kuna mtu mwingine ameweka tumaini lake kwa ndugu au kikundi cha watu fulani. Pale anapokuwa na shida au uhitaji anaamini kuwa atapata kutoka kwa watu hao. Ni kweli wataweza kukusaidia lakini msaada wao hufikia ukomo.

Katika kitabu cha 2 Nyakati 20;1-10, Kipindi hiki waliinuka maadui zaidi ya mataifa matatu ili kupigana na Israel chini ya mfalme Yehoshafati. Walikuwa ni Wamoabu, Waamoni na Wameuni. Mataifa haya yalikuwa yamejipanga kuipiga Israel Kwa pigo takatifu.
Biblia inaniambia baada ya Yehoshafati kupata taarifa hizi kuwa kuna mataifa yamejipanga kuipiga nchi yake, Inawezekana nae alikuwa na jeshi imara, silaha imara, Pia labda alikuwa na marafiki wa nchi jirani na Israel ambao angeweza kuwaomba msaada ili nae aingie vitani kupigana na maadui hao waliopanda ili kupigana naye.

Yehoshafati anafikia mwisho wa akili zake kabisa. Hakuliona jeshi lake. Hakuziona silaha alizokuwa nazo. Hakuweka tumaini kwa nchi jirani kwamba angeweza kupata msaada kutoka kwao. Akatambua kuwa hata kama angehitaji msaada kutoka kwa wanadamu ungefika kikomo tu.
Katika mstari wa tatu Biblia inasema kuwa Yehoshafati aliogopa sana, Akauelekeza uso wake ili amtafute BWANA. Nataka uelewe kitu kimoja hapa kuwa aliuelekeza uso wake kumtafuta BWANA na sio bwana. Yani alimtafuta MUNGU. Akatangaza mbiu ya kufunga na kuomba ili kuhitaji msaada kutoka Kwa BWANA.

Huu haukuwa wakati wa kuandaa majeshi, Haukuwa wakati wa kupanga silaha. Haukuwa wakati sahihi wa kuomba msaada wa majeshi kutoka nchi jirani. Kipindi hiki yeye pamoja jeshi lote na Israel yote walielekeza nyuso zao katika kutafuta msaada kutoka kwa MUNGU.
Yehoshafati anaomba maombi ya ajabu ya kuzidai ahadi za Mungu juu ya taifa LA Israel. Mstari wa tisa, “Yakitujia mabaya, upanga, hukumu au tauni au njaa tutasimama mbele ya nyumba hii na mbele zako(maana jina lako limo katika nyumba hii) na kukulilia katika shida yetu nawe utasikia na kuokoa. Hapa ndipo lilipokuwa tumaini la Yehoshafati.

Yapo mambo kadhaa yanayotokea pale unapotambua kuwa ni Kwa MUNGU tu panapatikana msaada.

Kwanza. Kwa MUNGU unapata msaada wa Uhakika. Msaada wa Mungu ni tofauti na msaada wa wanadamu.

Pili, Kitendo cha kuhitaji msaada toka kwa Mungu ni dhahiri kuwa umetambua wewe huna uwezo wa kuweza kujisaidia peke yako. Akili yako haina uwezo wowote wa kutengeneza msaada. kama inavyosema Warumi 1:28

Tatu, Mungu huwa anafanya au kutoa msaada tofauti na matarajio yetu. Wakati Naamani amekwenda kwa Elisha ili amponye alidhania kuwa angetoka aanze kuvishika vile vidonda vyake na kupokea uponyaji, lakini anaambiwa akaoge mto Yordani mara saba.

Ukiendelea kusoma sura yote ya ishirini utaona MUNGU anavyotoa msaada wa ajabu kwa Yehoshafati na taifa la Israel. Mungu anaingilia kati na kupanga majeshi yeye mwenyewe. Anawaambia hakuna haja ya kujipanga kwa vita. Hakuna haja ya kuandaa silaha. Yehoshafati panga watu waanze kuimba kwa ustadi tena wimbo rahisi tu, MSHUKURUNI BWANA KWA MAANA FADHILI ZAKE NI ZA MILELE.
Wakati wakiwa wamejipanga huku wakiimba, Wakimsifu BWANA wa msaada. Mungu aliweka waviziago juu ya Waamoni na Wamoabu. Vita ikabadilika. Wale maadui hawakuona tena taifa la Israel. Wakapigana na nchi nyingine kabisa. Hivi ndivyo Yehoshafati na taifa la Israel walivyosalimika.

Kama unataka kustareheshwa wewe hitaji msaada toka kwa Mungu. Wakati mwingine hufanya mateka kwa wale wanaohitaji msaada toka kwake. Daudi nasema katika Zaburi kuwa hakuna popote ppale anapoweza kupata isipokuwa atayainua macho yeka na kutazama juu kwa MUNGU maana ndipo panapopatikana msaada.

Unaweza ukawa na kila kitu, UKawa na mamlaka, Ukawa tajiri, lakini bado unahitaji msaada toka kwa MUNGU. Ukiwa tajiri au ukawa na kila kitu usipomuweka MUNGU kuwa ndiye chanzo cha msaada wako. Hesabu kuwa una hasara, Unafananishwa na yule mkulima aliyelima na kupata mazao mengi saana, halafu akaiambia nafsi yake sasa kaa ule unywe na ufurahi. Yesu akamwita mpumbavu. Kwani usiku wa leo wanaitaka roho yako. WANAITAKA.

Rafiki, Kwa chochote kile unachokifanya hebu muweke MUNGU awe chanzo cha msaada wako. Usitegemee akili zako maana nazo hazina akili, Hitaji msaada wa MUNGU katika uwezo wa akili zako. Hakika utayafurahia maisha.

Nakutakia wakati mwema.

Rafiki yako,

Steven Mshiu.

+255 655 882074,

May 10,2018.

Nitafute Facebook kwa jina LA Steven Mshiu.

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading