Ndani ya jiji lenye watu wengi kuliko miji mingine ndani ya Tanzania jiji la Dar es Salaam, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya Usafiri. Hivyo basi serikali pamoja na watu binafsi wamekuwa wakiwaza kila siku ni njia gani inaweza kuwa suluhisho la tatizo hili.

Katika kufikiri huko kukatokea watu wawili ambao walikerwa sana tatizo hili la usafiri wa kugombania hasa kwenye daladala. Watu hawa walikuwa hawafahamiani lakini kwa wakati mmoja walipitia matatizo yanayofanana. Kwa wakati mmoja wakawaza kujiondoa kwenye tatizo hili la usafiri.

Kila mmoja alifikiri kwa namna yake, mmoja aliamua kuchukua mkopo akanunua gari ndogo ambayo itamsaidia kufika kwenye shughuli zake kwa urahisi na haraka zaidi, na yule mwingine akaamua kununua daladala yake mwenyewe ili aweze kupunguza adha ya usafiri kwake na kwa watu wengine Zaidi.

Watu wote hawa wana mawazo mazuri ya sana ya mabadiliko na kupanda viwango. Utofauti walionao ni katika fikra tu. Mmoja alijifikiria yeye mwenyewe na akaamua kujitatulia tatizo peke yake, na mwingine aliwaza mbali kabisa akaona hili sio tatizo tu bali ni fursa. Kama watu ni wengi kuliko daladala maana yake nikiongeza daladala zangu hapa nitawasaidia watu na pia nitatengeneza pesa.

Watu wengi tuna fikra kama za huyu jamaa alienunua gari yake binafsi ya kutembelea ili awahi haraka kwenye shughuli zake. Ni wazo zuri sana, ni maendeleo mazuri sana lakini haya ni ya kibinafsi na pia hayatakusaidia sana kama huyu aliewaza kwenda kununua daladala zake.

Kuna matatizo mengi yapo kwenye jamii na watu wanawaza kuyatatua lakini changamoto ipo kwenye aina za suluhisho tunazotaka kuleta kwenye matatizo yetu. Mara nyingi mawazo yanayotujia huwa ni ya kibinafsi Zaidi na ndio maana tunakuwa wengi tuna Maisha ya wastani na hatuendelei na kufikia utajiri mkubwa.

Ukiwa na fikra za kujifikiria wewe mwenyewe tu katika kutatua matatizo sio rahisi kuona picha kubwa kwenye matatizo unayopitia. Lazima ubadilishe mtazamo wako uanze kuwaza namna gani utawasaidia na wengine wanaopitia kwenye tatizo kama lako na sio utafute njia rahisi ya wewe binafsi kuepuka tatizo.

Mfano mwingine tuna wanafunzi wengi waliomaliza vyuo wako mitaani hawana ajira na katikati ya wanafunzi hao kuna watu wenye fikra za kibinafsi na wenye fikra pana Zaidi katika kutatua matatizo ya wengine. Wenye fikra za kibinafsi wanaweza kukimbilia kujiajiri tu mahali ambapo watapata pesa za kuendeshea Maisha yao. Wenye fikra pana za kutatua tatizo sio kwa binafsi tu bali hata kwa wengine wenye tatizo linalofanana watawaza kuleta makampuni ambayo yatapunguza tatizo la ajira. Watawaza kuja na aina mbalimbali za suluhisho ambazo zinatawasaidiwa wengi na wao watafaidika pia.

Rafiki yangu nataka uache fikra za kibinafsi katika matatizo unayopitia.

Anza kuwafikiria wengine kama wewe mnaopitia tatizo linalofanana na uone ni namna gani unaweza kuwasaidia ili na wewe ujisaidie. Ukiishia kufikiria wewe tu kwenye kila tatizo unalopitia mwisho wa siku utaishia kuwa na Maisha ya wastani, hutaweza kufanya jambo lolote kubwa hapa duniani. Watu wote waliofanikiwa na kufikia kuitwa mabilionea waliwaza katika namna ya kutatua matatizo ya watu kuliko kufikiria Zaidi wao binafsi.

Badili fikra zako kuanzia sasa. Tatizo lolote unalopitia sasa hivi kuna wengi wanapitia embu anza kuwatazama katika namna ya tofauti ona zile ni hela, yaani kwamba kila mmoja anaepitia tatizo kama lako ukiweza kulitatua basi atakulipa pesa nzuri. Zidisha hiyo pesa kwa idadi ya watu unaowaona wanapitia tatizo kama lako halafu utaona ni kiasi gani utakuwa unatengeneza.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

#usiishienjiani

www.jacobmushi.com/coach

8 Responses

Leave a Reply to Peter mahunjaCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading