Tunaishi kwenye dunia ya watu wenye tabia za aina tofauti tofauti. Wengine wenye kukera, kuudhi, kukasirisha na kila aina ya ubaya. Wengine ni wapole wanaweza kusikiliza watu vizuri na hata kama utawaudhi kamwe hawataweza kukasirika na wewe.

Sasa tukiachana na hao watu ambao tunaweza kuwazungumzia juu ya tabia zao inatakiwa wewe binafsi uanze kujifikiria wewe unaishije na watu? Hii ni kwasababu tunasema huwezi kuwabadili watu lakini wewe mwenyewe unaweza kujitengeneza na ukawa bora.

Mtu akija kwako akakukasemesha kwa ukali na wewe ukamjibu kwa ukali unakuwa hujatofautiana na yeye hata kidogo. Mtu akikutusi na wewe ukarudisha tusi unakuwa huna tofauti na yeye. Hakuna faida yeyote utakayopata kwa kutengeneza ugomvi na mtu Zaidi sana utakuwa unajitengenezea maadui ambao huna kazi nao kwenye Maisha yako.

Kama kazi yako inakuhusisha na kuongea na watu kila siku jifunze sana kuongea na watu vizuri. Kwa mdomo wako unaweza kujitengenea mambo mabaya au mazuri kwenye maisha yako.

Ishi Vizuri Na Kila Mtu, Ongea Vizuri na Kila Mtu Usitengeneze maadui wasio na faida kwenye maisha yako. Hujui ni lini au ni kwa jambo gani utakuja kumhitaji huyo mtu unaegombana nae leo bila ya sababu yeyote ya msingi.

Ni kweli huwezi kumridhisha kila mtu lakini haina maana uwachukie na kuwaona kama maadui wale ambao hawajaridhika na kile unachokifanya.

“Kijana mmoja alikuwa ametafuta kazi kwa muda mrefu sana tangu amalize elimu yake ya chuo kikuu. Ilipita takribani miaka miwili mtaani akizunguka na bahasha kwenye ofisi za watu bila ya kupata kazi yeyote.

Siku moja baada ya kuzunguka huko na huko akapigiwa simu na sehemu moja aliwahi kupeleka barua na kuitwa kwa ajili ya usaili. Alifurahi sana ana akaishia kumshukuru Mungu kila saa.

Kesho yake asubuhi akajiandaa haraka na akatoka kwa ajili ya kuwahi foleni barabarani. Akiwa kwenye bodaboda ghalfa alikoswa koswa kugongwa baada ya kuingia mbele ya gari iliyokuwa inakuja kwa kasi.

Gari ile ilisimama na dereva wa bodaboda akaanza kumtukana yule mwenye gari.

Cha kushangaza na kijana yule aliekuwa anatafuta kazi nay eye akaingilia ugomvi wa wenzie akaanza na yeye kurusha maneno na matusi makubwa kwa mtu yule mwenye gari.

Dereva mwenye gari akasema “samahanini sana vijana wangu nilisimama kujua kama nimewaumiza nyie. Sijasimama ili tugombane.” Akapanda kwenye gari na kuondoka.

Baada ya muda kidogo kijana yule akafikishwa kwenye ofisi alizoitwa kwa ajili ya kazi. Kuingia kwenye chumba cha usaili anakuta bosi ni yule aliekuwa anamtukana barabarani.

Alitetemeka sana hadi akashindwa kujibu vizuri maswali aliyokuwa anaulizwa, mwishoni kabisa yule bosi akampatia kazi na akamwita pembeni na kumueleza “ Wewe ni kama mtoto wangu, ningeweza kukuadhibu kwa kukunyima kazi tu na ingetosha kuwa funzo kubwa kwako. Lakini nimeona nikufundishe kwa kukutendea wema.

Kijana wangu jifunze kuishi vizuri na kila mtu, usitengeneze maadui ambao hawana faida yeyote kwenye Maisha yako. Ishi vizuri na kila mtu.”

Natamani ujifunze kitu kwenye kisa hiki, kuna mambo yanaweza kuwa yanatokea kwenye Maisha yako leo, kumbe ni namna tu uliongea siku moja vibaya na mtu. Kila neno linalotoka mdomoni mwako ni kama mbegu linakwenda kupandwa mahali na kuna siku utakula matunda yake.

Otesha mbegu ambazo unajua utakuja kufurahia matunda yake huko baadae. Unaweza kufurahia wewe au watoto wako na wajukuu wako.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading