415; Huwezi Kuwa Kamili Jikubali Ulivyo.

Siku zote kama unaishi na watu ambao unaona kama wamekuzidi vitu vingi, utakuwa unajiona wewe ndio hujakamilika. Unaweza kuona wengine wanavaa vizuri kuliko wewe, wanakula vizuri kuliko wewe, wanaendesha magari mazuri kuliko wewe, wana wenza wazuri kuliko wewe. Hii inasababishwa na wewe kujisahau kabisa na kutoangalia vile vizuri ambavyo umebarikiwa.

Kama utatumia muda mwingi kutazama vile ambavyo huna utaviona vingi sana. Ukiwaangalia wengine unaweza kusema wana furaha kwenye ndoa yako kuliko ndoa yako. Lakini ukweli upo hivi, hii inatokea kwa watu wengi, inawezekana yule unaedhani ana furaha kuliko wewe hata yeye ana vitu ambavyo havifurahii na akiviona kwako anakuona wewe umemzidi.

Hivyo basi badala ya kukaa na kuwatazama wengine jitazame wewe umebarikiwa vitu gani. Mshukuru Mungu kwa hivyo na uvifurahie sana, kwasababu kuna siku vinaweza visiwepo tena. Kuna msemo unasema “Unalalamika Huna Viatu Kuna Wengine Hawana Miguu” yaani kwasababu huna viatu usijione wewe huna kila kitu mshukuru Mungu amekupa Miguu ambayo unaweza kuitumia kwenda kutafutia viatu kwasababu kuna watu ambao hawana hiyo Miguu yako.

Kuna vitu vingi sana umebarikiwa ana wengine hawana, jikubali, jione umebarikiwa na baraka za Mungu zitadumu kwenye Maisha yako. Kamwe usitumie Maisha ya wengine kama kipimo cha kupimia Maisha yako. Yale malengo makubwa uliyoyaweka ndio yawe kipimo chako. Jitazame miaka kumi ijayo kisha ujione bado una safari ndefu ya kufika huko.

Ukiweza kujikubali utaanza kuona mengi yanakuja kwenye Maisha yako, ukianza kumkubali huyo uliepewa au uliemchagua utaanza kuona vitu vingi vizuri Zaidi ndani yake. Anza kwa kushukuru kwa kile ulichonacho ili upate Zaidi.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading