Habari za Leo Rafiki na Mwanamafanikio mwenzangu. Ni furaha yangu kusikia kwamba unapiga hatua na kusonga mbele kila siku kwenye kile unachokifanya.

Leo tunajifunza Jinsi ya Kuanza jambo unalotaka kulitimiza maishani mwako. Inawezekana umehamasika sana, umejifunza mengi sana humu lakini bado hujaanza. Bado unajishauri na kusema mwakani nitaweka malengo nianze kuliishi kusudi langu, mwakani nitaanza kuitimiza ndoto yangu. Ukweli ni kwamba haitakaa uanze. Zipo njia au namna chache sana nimeorodhesha hapa namna ya Kuanza chochte kile na kuendelea mbele jifunze nami pole pole.

Wakati wa Kuanza ni Sasa

Hakuna wakati mwingine ulio sahihi Zaidi ya sasa. Unavyoahirisha ndio unazidi kupoteza muda. Kubali kwamba hakuna siku utakuja kupata nafasi ya kufanya hilo jambo unalolisogeza kila siku. Chagua namna rahisi ambayo itakuwezesha uanze kidogo kidogo hadi ufikie mafanikio. Inawezekana ukiamua hata leo ukaanza kuliishi kusudi lako na ndoto yako. Hakuna namna ambayo itakuja kuwa rahisi kwako Kuanza. Inawezekana unasubiria nyakati rahisi bahati mbaya ni kwamba huko tuendako hali ndio inaweza kuwa ngumu Zaidi ya ulivyowahi kufikiri.

Tengeneza Malengo na Mipango.

Andika malengo yako juu ya vile vitu unavyotaka kuvitimiza. Malengo ya muda mfupi na ya muda mrefu. Weka mipango ya kutekeleza kila siku kidogo kidogo. Hata kama huna muda jaribu kutenga hata lisaa limoja kila siku kufanya kile unachotaka kukitimiza mchango wako huo hautakuwa bure. Kama unataka kuandika Kitabu chenye maneno 30,000 (elfu thelathini) unaweza kuandika kwa siku 30 tu endapo kila siku utatenga masaa mawili ya kuandika maneno 1,000 (elfu moja). Kama wewe sio mwepesi kuandika sana unaweza kuandika kwa miezi miwili kwa kuandika maneno 500 (mia tano) kila siku. Huo ni mfano tu wa jinsi ya kuandika Kitabu unaweza kuutumia kuweka mpango wako wa kufanya chochote kile kwa Kuanza kidogo kidogo mwisho ukamaliza kabisa.

SOMA: KUBALI WANAYOFANYA WENGINE

Anza na Ulichonacho,

Kile kile kidogo ulichonacho ndio cha kuanzia, inawezekana unatamani sana uwe na vitu Fulani ndio uweze kufanya mambo makubwa na ukasahahu vile ulivyonavyo pia vinaweza kukusaidia kufikia malengo yako. Unaweza kumkuta mtu ana kila kitu kizuri ambacho kinamwezesha yeye kupiga hatua lakini bado analalamika. Kitu cha kwanza ulichonacho ni ufahamu, Mungu amekupa huo ili uutumie wekeza maarifa ya kutosha kwenye ufahamu wako sasa. Fikiri na buni njia mbalimbali za wewe kutoka kimaisha. Maisha yanapokua magumu sana ndipo watu hugundua njia mbalimbali za halali na zisizo za halali za kujitafutia kipato. Utumie ugumu wa maisha kama njia ya wewe kubunu wazo zuri la biashara na lifanye maisha yako yawe bora Zaidi. Una watu waliokuzunguka, una vifaa vizuri ambavyo vinakunganisha na watu wengi Zaidi kila siku tumia njia hizo kupata wazo zuri na namna ya Kuanza ili ufikie mafanikio yako.

Utandawazi.

Utandawazi umetuwezesha watu wa mataifa mengi kuwa karibu sana. Jana asubuhi nilikua nazungumza na rafiki yangu alieko Indonesia kwa kupitia simu yangu ya mkononi. Inawezekana sio kitu cha ajabu hicho kwako lakini je wewe unajua namna ya kukitumia ili uweze kufikia ndoto zako? Kama tunasema dunia ni kijiji sasa mbona unashindwa kufikisha kile unachokifanya kwa watu wengi Zaidi!

Teknolojia.

Teknolojia pia imerahisisha mambo mengi sana ambayo miaka michache tu hayakuwepo. Kwa sasa hata kama unafanya kazi porini kusiko na binadamu unaweza kuwafahamisha wenzako kinachoendelea muda huo huo uko ulipo. Ukiweza kutumia vyema teknolojia unaweza Kuanza kabisa chochote unachokitaka na kuwafikia wengi sana. Unajiunga kifurushi cha internet kila siku kwa ajili ya kujifunza lakini tazama na upande wa pili namna ambavyo unaweza kutangaza jina lako la kibiashara. Kama unachokifanya unaweza kukibadilisha kikaja kwenye maandishi unaweza kufikia ulimwengu kwa haraka sana. Haijalishi hata kama huna mtaji wa fedha unaweza kutumia vifaa hivi kama mtaji wako na ukaanza pole pole kuwafikia watu.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading