SEMINA JANUARY 2017
SIKU YA KWANZA
JINSI YA KUEPUKA MADENI MABAYA
Haijalishi upo kwenye madeni makubwa kiasi gani bado una nafasi ya kutoka na kuanza safari ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha. Ili upate mabadiliko kwenye Maisha yako sio mpaka ufundishwe na mtu aliefanikiwa sana. Unachotakiwa wewe ni kuchukua mafundisho yaliyo sahihi na kuyafanyia kazi Maisha yako lazima yatabadilika.
Maisha bila ya madeni ni Maisha ya uhuru ambayo unaishi huku ukifurahia. Jiulize hapo ulipo kama umesongwa na madeni kila pesa unayoipata haina furaha kwasababu inapotelea kwenye kurudisha kwa watu. Kama bado Maisha unayoishi ni ya namna hiyo huwezi kuishi ukiwa huru hata siku moja.
Vipo vitu viwili vya kufanya kuanzia sasa. Kama haupo kwenye madeni ni ujitahidi kuhakikisha hauingii huko hata kidogo. Kama upo kwenye madeni hakikisha unatoka huko kwa namna yeyote ile. Na semina hii itaweza kukusaidia wewe kutoka kwenye madeni au kutokuingia kabisa kwenye madeni.
Mara nyingi vipo vitu ambavyo vinasababisha sisi kuingia kwenye madeni. Na ukichunguza kwa makini unakuta watu wananunua vitu ambavyo sio vya muhimu, wanataka kuishi Maisha ambayo yapo nje ya uwezo wao. Wengine wanataka kuishi Maisha ya maigizo. Zipo sababu nyingine ambazo ni kama mtu alikopa fedha akawekeza kwenye biashara akapata hasara. Mwingine aliugua akakopa sasa anateseka kulipa madeni. Mwingine ni harusi, na mengine mengi unayoyafahamu. Zote hizo ni sababu zinazosababisha watu wengi kuingia kwenye madeni.
Kinachotakiwa hapa kufahamu ni jinsi ya kuzuia sababu hizo zisitokee tena kwenye Maisha yetu na kuondokana kabisa na madeni haya.
Jinsi ya Kutoka Kwenye Madeni.
Yapo mambo machache unatakiwa uyafahamu ili uweze kutoka kwenye madeni yanayokuzunguka haijalishi ni makubwa kiasi gani. Kitu cha kwanza lazima uyafahamu vizuri madeni unayoadaiwa. Tafuta muda nunua daftari lako (Diary) ambayo utaandika huko kila deni unalodaiwa, usiache hata moja haijalishi ni dogo kiasi gani. Hata kama unadaiwa kwenye simu andika. Hakikisha unaandika na majina ya wadeni wako.
Ukishamaliza hatua ya kwanza fanya hesabu yako ujue unadaiwa jumla madeni kiasi gani. Hapa ndipo utaweza kuweka mpango mzuri wa kukuwezesha utoke kwenye kifungo hicho.
Ukishafahamu kiasi cha deni unalodaiwa weka mpango chini wa kuanza kupunguza madeni hayo moja baada ya jingine. Hakikisha umechambua yale madeni ambayo unajua waliokukopesha wanaweza kuleta madhara yeyote kwako ili umalizane nayo mapema.
Tenga 10% – 30% (Kulingana na Ukubwa wa Madeni yako) ya kipato chako upeleke kwenye madeni haya kulingana na unavyopata kipato hicho.
Jaribu na wewe anza hata na kidogo kidogo kuwa na nidhamu na fedha uone nayo itakavyokuheshimu.
SIKU YA PILI
Tabia za Kujijengea ili Kuondoka na madeni.
- Ongeza Uwezo wako wa Kupata Fedha.
Ili uweze kutoka kwenye hali uliyonayo lazima ukubali kuchukua hatua ya kuongeza kipato chako. Kama hali ya kifedha uliyonayo sasa hivi ndio umekuingiza kwenye madeni ukiyalipa madeni yote bado utakuwa na uhitaji Zaidi wa pesa ambao unaweza kuwa sababu yaw ewe kurudi tena kwenye madeni.
Ni muhimu sana kwa namna yeyote ile uwe mwajiriwa au umejiajiri uanze kufanya mpango wa kukuza kipato chako. Kama ni biashara ujue namna ya kuifanya iongezeke kimapato. Kama ni ajira basi uanze mpango wa kujiajiri kwa muda wako wa ziada.
Hatua ya kwanza anza kupata maarifa ya kutosha kwenye upande wa fedha. Jua ni namna gani unaweza kumiliki utajiri wako mwenyewe. Hakuna namna yeyote ambayo utaepuka kukopa madeni mabaya Zaidi ya kuupata uhuru wa kifedha.
Jifunze kuifanya fedha ikutumikie wewe na sio wewe uitumikie fedha. Yote haya yatafanikiwa kama utaamua kuanza kidogo kidogo. Amua leo kuanza kujiwekea akiba. Anza kuwa mbunifu kwenye biashara yako ili uweze kukuza kipato chako.
Anza na kidogo ulichonacho haijalishi ni kiasi gani angalia ni kitu gani unachoweza kufanya nacho ili uzalishe pesa. Kutengeneza elfu moja kwa siku na kutokutengeneza kabisa ni vitu viwili tofauti. Huwezi kuwa sawa na mtu ambaye hana chochote anachofanya.
Kuna watu watakucheka kwasababu umeamua kufanya biashara au kile ulichoamua kufanya. Amua kuwaangalia wao uendelee kubeba madeni au amua kuziba masikio utoke kwenye madeni.
Ongeza mifereji mingi ya kipato ili kuufikia uhuru wa kipesa. Hakuna namna nyingine ya kuondokana na madeni. Usitegemee chanzo kimoja cha pesa.
- Jua Matumizi yako na Tengeneza Bajeti.
Weka bajeti ya matumizi yako, jua ni kiasi gani utatumia kwa chakula na kiasi gani kwa starehe, lakini bajeti hiyo isizidi sehemu ya tisa ya kipato chako.
Tatizo kubwa ambalo wengi wanapitia ni kutokujua matumizi yao. Katika kitabu cha The Richest Man in the Babylon mwandishi anafundisha kwamba lazima tujue matumizi yetu ya kila siku ili tuweze kugawanya kipato vizuri.
Kama huna tabia ya kujua matumizi yako utajikuta unapata pesa lakini hujui zinakwenda wapi.
Ukifahamu vyema bajeti yako unapata mwangaza mzuri wa pesa zinavyoingia na kutoka kwenye mifuko yako. kamwe huwezi kulalamika kwamba hujui pesa zinakwenda wapi.
Kama ukijua unatumia kiasi Fulani cha pesa kwenye matumizi ya kula, kodi ya nyumba(kama umepanga) na mengine madogo madogo unaweza kuipangilia vyema pesa yako.
Kama unapokea mshahara ni rahisi sana kutengeneza bajeti yako ya mwezi mzima.
Kama wewe ni mfanyabiashara na pesa zako hazina ratiba maalumu yaani leo unapata kiasi Fulani kesho kinapungua au kuongezeka unatakiwa uweze kugawanya pesa yeyote inayoingia mfukoni kwako kama faida katika asilimia ambazo tumezungumza kwenye utangulizi.
Hapa unatakiwa uweze kujibana sana hasa kipindi ambacho unapata pesa nyingi ndio kipindi cha kutengeneza akiba nzuri ya mbeleni ya matumizi yako.
Unashauriwa Bajeti yako isizidi asilimia 90 ya kipato chako lakini mimi nakushauri kwasababu ya madeni jitahidi kujibana Zaidi hadi pale utakapoweza kuufikia uhuru wa kipesa na madeni yakiwa mbali na wewe.
SIKU YA TATU
- Uza vitu vyote Usivyovihitaji/visivyo vya Muhimu.
Inawezakana uliingia kwenye madeni kwasababu ya kupenda kuonekana mbele ya jamii wewe ni mtu wa maana sana.
Mfano ulikuwa unapenda kuonekana unamiliki simu au komputa ya ghali sana. Hii ikakusababishia wewe kwenda kukopa ili tu kuwaridhisha marafiki au watu ambao unajumuika nao kila siku.
Sisi binadamu tuna tabia moja ya ajabu sana. Kama ukiwa unatembea na marafiki zako wote wana simu nzuri za Apple halafu wewe huna, moja kwa moja utaanza kujisikia huzuni na kutamani kuwa nayo. Unaweza kuingia tamaa ukakopa pesa popote tu ili mradi ufanane na marafiki zako.
Ambacho utasahau ni kwamba hujui wao wanatoa wapi pesa za kuwawezesha kumiliki simu hizo ulizotamani. Hujawauliza wewe umekimbilia kwenda kukopa.
Wenzako labda walipewa zawadi au wana biashara zao kubwa tu huko wewe hujui.
Sasa badala ya kutamani kitu cha mtu kizuri na kwenda kukopa kaa nae chini au chunguza ujue amekipata vipi.
Kaa chini angalia vitu unavyovimiliki vipi ni vya muhimu Zaidi. Vipi ukivikosa Maisha yako yatayumba. Hivyo ndio vya muhimu sana baki navyo. Vile ambavyo sio vya muhimu viuze pesa utakayopata unaweza kuamua kwenda kupunguza madeni na nyingine wekeza kwenye biashara au kaanzishe biashara mpya.
Inawezekana una nguo nyingi sana ambazo huzivai au hujazivaa huu ni mwezi wa sita, inawezekana una simu ya ghali sana ambayo matumizi yake ni sawa na simu nyingine ambayo ni robo bei ya uliyonayo. Mfano una Iphone 7 ambayo unaitumia matumizi ya kawaida kabisa, halafu huna biashara yeyote, una madeni kibao, uza nunua tecno ya laki mbili pesa nyingine kaanzishe biashara.
- Acha Tabia za Kumiliki Vitu vya Gharama.
“Usinunue kitu kipya wakati unaweza kupata kilichotumika na kikakufaa”
Kama kwa sasa tunavyoongea upo kwenye madeni na bado unamiliki vitu ambavyo ni vya gharama sana jithidi kuvipunguza. Kwenye tabia ya tatu tumezungumza kuuza vitu vyote usivyovihitaji au ambavyo sio vya muhimu. Hapa utatazama vyote ambavyo ni vya gharama lakini huna matumizi ya muhimu navyo.
Kumiliki vitu vya gharama sio utajiri. Kama ulikuwa na mtazamo huo basi unapotea. Utajiri upo kwenye vitu ambavyo vinakutengezea pesa kila siku. Kama wewe umenunua saa ya dhahabu ya thamani ya milioni nne halafu mwenzako akachukua milioni nne hiyo hiyo akawekeza kwenye kilimo baada ya miaka michache anaweza kuwa amekupita kwenye utajiri.
Ili usirudi tena kwenye madeni naamini kwamba kama una madeni yanakusumbua basi wewe hujafikia uhuru wa kipesa bado hivyo ni muhimu sana kuacha kununua vitu hivi vya gharama kwa wakati huu mpaka utakapofikia uhuru wa kipesa.
Kama kuna kitu kinauzwa laki nane kipya dukani halafu kuna uwezekano wa kukipata kwa shilingi laki nne kilichotumika ni bora ukachukua cha shilingi laki nne nyingine inayobaki iwekeze kwenye biashara.
Unapenda kupendeza ndio, watu wanakusifia sawa lakini hawajui madeni uliyonayo. Wakijua wataanza kukusema “ huyu jamaa msimwone anapendeza sana ana madeni kibao” sasa haina maana yeyote. Vaa nguo ya mtumba kwa sasa hadi utakapofikia uhuru wa kipesa labda kuwe na ulazima sana wa kuvaa hiyo nguo ya ghali.
Ukishindwa kuindoa hii tabia unaweza kujikuta mtu ambaye unakwenda kukopa ili upate pesa za kununua vitu vya gharama ulivyozoea.
Haina maana kuvaa nguo ya ghali halafu ni ya mkopo. Sidhani kama unajisikia sawa sawa unapendeza unasifiwa halafu kumbe ulikopa pesa ukaenda kununua.
Tabia yeyote inatengenezwa andika chini tabia hii uanze kuifanyia kazi mara moja. Haijalishi watu watakuonaje watakusemaje, watasema umeishiwa lakini wewe unajua ulipopeleka pesa zako.
SIKU YA NNE
- Kaa mbali na Vitu/Marafiki ambao wanakufanya utamani vitu Visivyo vya Lazima.
Maisha ya sasa hivi lazima uwe makini sana na marafiki unaoambatana nao kila siku. Unaweza kuwa na marafiki ambao kila mkitoka lazima uje unalalamika pesa hujui umetumiaje hao ni hatari sana.
Kama unajijua una madeni, huna biashara yeyote imara, hujafikia ndoto zako bado ni vyema ukapunguza starehe. Punguza matumizi yako ya kila siku hasa yale yasiyo ya lazima.
Najua kila mmoja anatamani aonekane ana Maisha Fulani mazuri hivi hasa kwa marafiki zako wa karibu. Unatamani wajue unaishi Maisha ya raha. Lakini kama ndani yako unaumia haina maana.
Ndoto yako kubwa utaifikia siku moja. Yale Maisha unayoyaota kila wakati ipo siku utayafikia kama tu utaweza kujinyima sasa hivi na kutengeneza mifereji ya kutosha ya fedha kwenye Maisha yako.
Kama unajijua wewe ni sehemu gani unavutwa sana na tamaa ya kutumia pesa basi kaa mbali na sehemu hizo. Mfano inawezekana ukienda kwenye soko la nguo lazima ununue nguo. Pengine ukiona vitu vitamu vitamu lazima ununue. Anza kukaa mbali na sehemu hizo au usitembelee kama huna lengo la kwenda kufanya manunuzi ya hivyo vitu.
Kuna wengine wana tabia kila akishika hela lazima aende matembezi kama supermarket na sehemu ambazo anatumia pesa zote. Halafu mtu huyo huyo anajikuta analalamika pesa hazikai.
Kuna watu wana tabia ya kuja kwako na kueleza shida zao uwasaidie hasa wakati unazo hela. Jaribu kuwasaidia namna ya wao kutatua matatizo yao wenyewe. Huu utakuwa ni msaada mkubwa Zaidi kuliko ukiwapa pesa. Ukiwapa pesa watarudi tena zikiisha au wakipata matatizo.
- Tabia ya Kuweka Akiba.
Kwa kila fedha kumi unazopata tumia tisa na moja weka kwenye mfuko wako.
“Haijalishi unapata pesa kiasi gani, kinachofanya utoke kwenye madeni na kufikia uhuru wa kifedha ni kile unachokweka kama akiba”
Kwenye kitabu cha The Richest Man in The Babylon (Mtu Tajiri kuliko Wote Babeli) mwandishi anasema kwenye kila shilingi unayopata hakikisha tisa unatumia moja unaweka. Anasema kwa kupitia kuweka akiba ndio njia pekee ya kututoa kwenye umaskini na kuishi Maisha ya uhuru wa fedha.
Jijengee tabia hii muhimu sana ambayo waliofanikiwa wengi waliitumia na wakafikia mafanikio makubwa. Inawezekana uliweka akiba inafika kiasi Fulani unaitumia lakini lazima uamue kujijengea nidhamu ambayo hutaweza kuivunja.
Akiba yako ikikua lazima uanze mpango wa kuiweka kwenye kitu ambacho kitakuzalishia pesa na kuifanya pesa yako ikue Zaidi.
Njia rahisi ya kujizuia kutumia akiba ni wewe kuacha kuifikiria, kuacha kuikagua mara kwa mara ili ujue imefika ngapi. Vile vile uione kama pesa ambayo haipo tena mikononi mwako. Ihesabu kama pesa ambayo ulikuwa unayo ila umeshaitumia.
Akiba kwa lugha nyingine tunasema ni pesa unayojilipa wewe. Sasa ukimlipa mtu pesa unaweza kwenda kuichukua tena?
Neno langu la Mwisho ni kwamba, madeni ambayo hujaweka kwenye biashara yeyote au ambayo unadaiwa sasa hivi yanakufanya uwe mtumwa. Mtumwa ni mtu ambaye hata kufikiri sawasawa anashindwa kwasababu wakati mwingine anawaza kukamatwa.
Usikubali kuwa mtumwa wa madeni kwanini wewe usiwakopeshe watu siku moja? Kwanini wewe usiwe una watu unawadai pesa zako ulizowakopesha?
Inawezekana.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi
Mwandishi, Kocha wa Maisha na Mjasiriamali.
Nimejifunza namna ya kuheshimu pesa. Mungu akubariki
Amina , Karibu sana
thanx mkuu
Karibu sana
Barikiwa kwa huduma hii,umenisaidia sana.
Asante sana nimejifunza sana🙏🏾🙏🏾
Nimeipenda sana mafundisho Yako
Ubarikiwe sana