Habari za leo Rafiki yangu, ninatumaini unaendelea vyema na mapambano ya kufikia mafanikio makubwa. Ni muhimu utambue kwamba maisha hayatakaa yawe marahisi hivyo basi unachohitaji ni wewe kuwa na ujuzi wa namna mbalimbali ili uweze kuzikabili changamoto unazokutana nazo. Kazi yangu kubwa ni kukupa wewe mbinu mbalimbali ambazo utazitumia zikuwezeshe wewe katika changamoto hizo na uweze kupiga hatua kila siku.
Kwanini nazungumza na wewe kuhusu tabia? Unaweza kua na ujuzi mkubwa sana, unaweza kua na vipaji vizuri na vya pekee sana, unaweza kukutana na fursa nzuri sana. Lakini tabia zako zikakuangusha na ukashindwa kufikia kile ulichokitaka. Kama utaweza kubadili tabia ambazo zinakurudisha nyuma taratibu. Hivyo ni muhimu sana wewe kupambana na tabia ndogo ndogo ambazo zinakurudisha nyuma.
Kusikiliza ni tabia ambayo wengi hatuna mara nyingi tumekua ni watu wa kufanya haraka sana katika kuchukua maamuzi, kuhukumu, kukosoa, kuonyesha watu nini wafanye kabla hatujawasikiliza. Unapojijengea tabia hii ya kusikiliza utajikuta unajifunza mambo mengi sana katika maisha ya wengine.
“Being a good listener can help you to see the world through the eyes of others.”
Kua msikilizaji mzuri kunakuwezesha wewe uweze kuiona dunia katika macho ya wengine. Ukiweza kua msikilizaji mzuri utaweza kuongeza uwezo wako wa kuelewa mambo na kuweza kuwashauri watu vizuri. Itakuwezesha wewe uweze kujiunganisha na wengine na kukuza uwezo wako wa kuwasiliana na wengine. Kama unataka uwe mtu mzuri kwenye kuwasiliana na wengine unatakiwa uweze kua msikilizaji mzuri. Unapozungumza unasema yale unayoyajua tayari lakini unaposikiliza unajifunza vitu vingine vipya.
“Good listening habits include paying full attention not only to what is said but also to the person speaking.”
Tabia nzuri ya kusikiliza inajumuisha katika kuweka umakini sio kwa kile kinachosemwa tu bali hadi kwa anaezungumza. Kwa kua makini kusikiliza utaweza kujua ni maneno gani ya kutumia wakati unamshauri mtu kitu na yapi ambayo hayafai kutumika. Kumbuka kwamba una masikio mawili na mdomo mmoja ndio maana unatakiwa usikilize Zaidi kuliko unavyoongea.
Mambo ya Kuzingatia unapomsikiliza mtu.
Jiweke wewe kwenye tatizo lake (Vaa Viatu Vyake)
Jaribu kujiona wewe ukipitia yale anayopitia unaemskiliza, ona maumivu anayopata. Hii itamfanya aone unamjali sana na ataendelea kufunguka Zaidi kwako. Wengi tunakimbilia kuwaona wenye matatizo ndio wameyasababisha wenyewe na kuwahukumu bila kuwasikiliza. Uzoefu ulionao wewe katika kutatua matatizo usiufananishe na wa mwingine. Yeye anabaki kua yeye.
Mwangalie Machoni,
Wakati unamsikiliza mtu ni vyema kumuangalia machoni. Hii inamfanya aone umempa umakini wako wote hivyo hatakereka kuendelea kuongea na wewe ataona unamjali sana na atakua tayari kukueleza chochote utakachotaka. Epuka kuingilia katikati ya mazungumzo na kuuliza swali. Anapokua anakuueleza jambo la muhimu sana hakikisha umekaa kimya na ujue sehemu nzuri ya kuulizia swali.
Achana na vitu ambavyo vitapoteza umakini wako wa kusikiliza. (simu,tv, radio,).
Wakati unazungumza na mtu ni bora uweke simu yako bila mlio, kama upo sebuleni kwako ni vyema sana ukazima Tv au radio, au chochote kile kitakachoweza kuingilia mazungumzo yenu. Hii itakusaidia wewe uwe makini Zaidi na itamfanya unaemsikiliza ajisikie fahari sana.
Usikimbilie kutoa suluhisho,
Usikimbilie kumpa suluhisho hakikisha umejua yeye anataka nini. Mara nyingine watu hutueleza vitu sio kwamba ili tuwape suluhisho bali ni ili tuwasikilize na tujue yanayoendelea ndani yako. Hivyo ni muhimu sana kufahamu unaemsikiliza anataka nini.
Mkumbushe.
Unapomaliza kumsikiliza mtu kama kuna jambo alikueleza linaloendelea kwake baada ya muda unaweza kumpigia simu na kumjulia hali. Jua anaendeleaje na maisha pia muulize kuhusu alichokueleza. Labda alikueleza kuhusu ndoa yake basi muulize hali ikoje kwa sasa. Hii itamfanya aone unamjali na ulichukua tatizo kama la kwako. Na itamfanya aendelee kubaki kwako na kukueleza vitu vingi sana.
Inawezekana ulikua unakosea sana kwenye namna ya kumsikiliza mtu na ukawa unasababisha mahusiano yako na wengine yasiwe na bora ni wakati wako sasa kujifunza na kuongeza ujuzi wako. Hii itakusaidia sana hasa katika familia mahusiano yako na mpenzi, mke, watoto, marafiki, na jamii nzima kwa ujumla. Hapa nimezungumza mambo machache sana ila yapo mengi mno tutaendelea kujifunza pamoja.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi
#UsiishieNjiani