Kuna mambo machache unatakiwa ujiulize Je eti ni kweli mwaka ujao utakuwa mpya kwako au ni zile kelele tu na hamasa? Una kitu gani unakitegemea kukipata cha tofauti ndani ya mwaka ujao? Umeajiandaa vipi kukipata? Upo tayari kuwa mpya ili upate hayo mambo mapya ya mwaka ujao?
Tuachane na hayo twende kwenye mada yetu ya leo. Nataka nianze na Makala hii kwa ajili yako wewe unaedhani hujaanza biashara hadi leo kwasababu huna mtaji. Kwani mwaka huu tena ukiendelea kulalamika huna mtaji ndio maana hujaanza biashara tutakuacha mbali sana.
Maana ya mtaji ni vitu vyote vya muhimu ambavyo vinahitajika kukusaidia katika kuanzisha biashara yako. Kama ni hivyo basi wewe pia unaanza kuwa mtaji.
- Capital Is not only money (Mtaji sio Pesa Peke yake)
Kuna vitu vingi sana ambavyo vimekuzunguka na unaweza kuanza kuvitumia kama mtaji wa kukuzia biashara yako. Naelewa sio kila biashara unaweza kuanza bila pesa kabisa lakini kama huna pesa na hujapata popote kwa kukopeshwa unafanyaje? Utabaki kuendelea kulalamika umekosa mtaji? Kwanza ukishajua unataka nini au unataka kufanya biashara gani ndio inakua rahisi Zaidi kujua utaanzaje kama ni bila mtaji kabisa au kwa kiasi kidogo. Mtaji wa kwanza ulionao ni wewe mwenyewe. Yaani wewe ndie mfanyakazi wako wa kwanza unatakiwa ujue kujitumia ili uzalishe pesa. Kwa sasa hivi unaweza kumiliki simu nzuri inayokuwezesha kuingia kwenye mitandao ya kijamii lakini usijue namna ya kuitumia kutengeneza kipato. Unatumia mtandao wa Facebook, Instagram na WhatsApp lakini hujui utaitumiaje kutengeneza watu wanaokuamini ili uwauzie bidhaa. Simu yako yaweza kuwa mtaji, kama una computa nyumbani inaweza kuwa mtaji, kama unakitu chochote kinachokuunganisha na watu kinaweza kufanyika mtaji.
SOMA: JINSI YA KUPATA WAZO LA BIASHARA
- Power Nguvu)
Wengi wetu ni vijana tuna nguvu unaweza kujitoa ukafanya kazi za nguvu kwa muda Fulani hadi ukajitengenezea kiasi cha pesa cha kuanzia biashara. Una uwezo mkubwa sehemu ipi? Wengine wana vipaji vizuri vya kuongea unawezaji kuongea vizuri na watu wakawa wateja wako? Wengine wana nguvu ya ushawishi yaani akiongea na mtu dakika chache wanaweza kuwa marafiki. Unaweza kutumia njia hiyo pia kama mtaji wako. Utajikusanyia watu ambao unaweza kuja kuwauzia bidhaa zako.
- Time (Muda)
Muda ndio mtaji mkuu nadhani ningetakiwa niuweke wa kwanza. Unaweza kukosa kila kitu lakini muda utakuwa nao. Unaweza kuwa huna pesa huna simu, huna chochote lakini una muda. Unautumiaje muda wako kama mtaji?
Tuseme wewe ni kijana umemaliza chou na upo nyumbani huna kazi yeyote. Unaweza kutumia muda ule ulioko nyumbani kujifunza sana kisha ukayatumia hayo unayojifunza kama katika kubadili Maisha yako.
Inawezekana wewe unapendelea sana bidhaa tuseme ni mchele. Anza kutafuta watu wanaouza mchele wa jumla jua mchele gani unauzwa bei gani kwa jumla. Nina rafiki yangu ananunua mchele Shinyanga gunia la kilo 100 ni Tsh 130 -140(Laki) kwa kawaida unaweza usiwe na hiyo laki moja ya mtaji wa kununulia huo mchele pia utakosa mahali pa kuuweka. Unaweza kutafuta wateja 10 tu watakaoweza kununua kilo 10 kila mmoja. Hawa wateja wawe ni watu unaowafahamu na wanaokuamini. Waombe wakupe pesa za huo mchele tuseme kilo moja ni tsh 2000/= kwa bei ya reja reja. Kila mteja atatakiwa akupe Tsh 20,000/= kwa kilo kumi. Lakini ukiangalia kwa bei ya jumla ni Tsh 1300/= hivyo faida yako wewe ni Tsh 700/= kwenye kila kilo moja au elfu saba kwa kila kilo kumi. Kama utaweza kuupeleka wote kwa wateja wako hao kumi utakuwa umetengeneza faida ya 70,000/= bila kuweka pesa yako yeyote. Ukirudia hivyo mara kumi tayari una laki saba. Hapo huna ofisi wala hujalipa kodi popote. Sana sana utatumia gharama kidogo sana ya usafirishaji na vifungashio. Ukiongeza idadi ya wateja unaowapelekea tayari umeshakuwa na biashara kubwa sana inayohitaji ofisi. Ukijiongeza hapo pesa ya kuanzia biashara unayotaka kuifanya utakuwa umeikamilisha.
Ukimwambia kijana ajaribu kufanya kitu kama hicho bado atakwambia hawezi au atatoa sababu zisizoeleweka. Unaweza kuchagua bidhaa yeyote unayoona inahitajika kwenye jamii unayokaa ukaamua kutumia mfano huo.
- Knowledge (Maarifa)
Una maarifa juu ya kitu chochote? Unaweza kutumia maarifa hayo kama biashara ukatafuta njia ya kuwapa watu na watu wakulipe. Mfano unaweza kuandika kitabu kinachoelezea kitu unachokifahamu vizuri. Hapa Kuna mengi sana mfano wake ni vitu ninavyofanya mimi mwenyewe.
- People (Watu)
Unafahamiana na watu wangapi ambao ukiwaomba pesa wanaweza kukupatia? Kama unao hao watu nakusihi usiende kuwaomba hela. Tumia mfano niliokupa hapo juu wa mchele uone ni bidhaa gani unaweza kuwapelekea wakakupa pesa.
Kuna kipindi nilipata nafasi ya kutembelea maduka ya simu hapa mjini Arusha kwa siku kadhaa nikajenga mahusiano mazuri na wauza maduka wale. Hivyo nikipita nawapa salamu. Sasa juzi nikapita madukani mwao nikiwanonyesha njia bora ya kuwasaidia waweze kufanya mauzo vizuri bila kupoteza mahesabu. Kwasababu tu nilikua nawafahamu kabla wakanielewa vyema sana. Tukabadilisha na namba za simu ili kuja kufanya biashara baadae. Ila kuna sehemu nilipita sikuwahi kupita mwanzo. Ukweli watu wale walikuwa wagumu kunielewa. Nilichojifunza hapo ni kwamba watu wanapenda kufanya biashara na watu wanaowafahamu na kuwaamini. Wakati huu unaofikiri huna cha kufanya endelea kujenga uaminifu na mahusiano na watu mbalimbali. Kuna wakati utafika unatakiwa kuuza bidhaa au kutoa huduma Fulani iwe ni ajira au umejiajiri lakini ukafanya kwa urahisi sana kwasababu una watu ambao wanakuamini. Watu ni mtaji unawatumiaje?
Unapokutana na mtu mpya wewe unamchukuliaje? Binti umekutana na mwanaume anakuomba namba wakati mwingine huna haja ya kumnyima mpe halafu tafuta kitu cha kuja kumuuzia lakini sio mwili wako.
SOMA: MABADILIKO YA KITEKNOLOJIA YANAVYOWEZA KUKUZA BIASHARA.
- Technology (Teknolojia)
Teknolojia ni mtaji pia. Kwenye teknolojia kuna vitu vingi sana unaweza kuvitumia kama mtaji wako. Je unajua namba au group ulizopo Facebook na Wasap unaweza kutumia kama sehemu ya kuonyesha unachokifanya na ukapata wateja? Je unafahamu simu yako ni Mtaji? Unaweza kuendesha biashara kwa kutumia simu ya mkononi (Smartphone). Kwenye teknolojia kuna mambo mengi ambayo tunaweza kuanza kuchambua moja moja kama somo kabisa. Jinsi ya kutumia blog kibiashara pamoja na mitandao ya kijamii.
Leo ninaishia hapa kama bado hujapata mwangaza juu ya mtaji tafadhali wasiliana nami kwa ushauri Zaidi. Kuna vitu ukinieleza ndio naweza kukupa ushauri kulingana na mazingira uliyopo na watu waliokuzunguka.
Rafiki Yako,
Mwandishi na Kocha wa Mafanikio
Jacob Mushi
Nimejifunza mengi sana
Asante sana kaka Jacob
Karibu sana Rafiki