“Nakumbuka siku moja nikiwa hapa Arusha kabla sijaoa nilipanda daladala kuelekea Tengeru kwenye shughuli zangu za kila siku. Ninaishi Arusha Sanawari hivyo magari mengi ya Tengeru huja yakiwa matupu ili yapakie abiria kwenye kituo cha Sanawari.

Siku hiyo kulikuwa na kimvua kidogo ambacho kiliwafanya watu wakimbilie kwenye magari haraka yanapofika tu kituoni. Na mimi nilikuwa mmoja wao, wakati naingia kwenye daladala na kukaa akaja kijana mmoja ambaye sikumfahamu wala sikuwahi kukutana nae kabla na akakaa pamoja na mimi.

Baada ya kwenda mbele kidogo tukafika kituo cha Kwa Mrefu, na yule kijana akashuka. Sehemu aliyokaa ikabaki tupu kwasababu hapakuwa na mtu aliesimama. Aliposhuka tu na gari ikaanza kuondoka kuangalia vizuri alipokaa nikaona Tsh elfu kumi, ooh nikasema hii ni bahati yule kijana kadondosha pesa na ameshashuka, nikaibeba na kuweka mfukoni.

Moyoni mwangu nikawa nimeipania sana ile hela na hivyo nikaona ngoja nikaitumie yote nikishuka kwenye daladala. Mungu ni mkuu tukafika Tengeru salama na mimi cha kwanza baada ya kushuka nikaingia kwenye mgahawa na kuanza kuchagua chakula kizurin a supu nzito nzito kwa ajili ya kuondoa baridi, nitumie ile pesa. Kwakweli nilikula nikashiba na kisha nikaendelea na shughuli zangu.

Baadae jioni nikarudi nyumbani kama kawaida nikiwa nimechoka sana kwa kazi za siku hiyo. Kufika tu nikafatwa na wapangaji wenzangu nilipie hela ya umeme nilikuwa nadaiwa, nikakumbuka kuna hela niliacha mezani nikasema ngoja niichukue nilipie hela ya umeme ninaodaiwa. Kwenda mezani sikuona chochote. Nikajaribu kufikiri nimeiweka wapi pesa ile kuja kukumbuka vizuri kumbe asubuhi niliibeba na kusema chochote kinaweza kutokea Njiani. Kuja kushtuka kumbe ile hela niliyodhani ni yule kijana kaidondosha ni mimi mwenyewe niliidondosha wakati natoa nauli.

Looh nikaumia sana ikanibi nitoe pesa nyingine nilipie umeme. Nikajifunza vitu vingi sana na nikaapa kutotumia pesa vibaya hata kama sio yangu.” Alimaliza kusimulia Rafiki yangu Baraka.

Kwenye hadithi hii yenye uhalisia wa Maisha yetu ya kila siku wewe umejifunza nini Rafiki?

Ni vizuri chochote ambacho hujakitolea jasho usikitumie kama yule aliekutafuta jaribu kuwa na kiasi, badala ya kukitapanya jaribu hata kukitoa kama msaada au kukiweka akiba ya baadae. Hebu tujaribu kuwaza huyu Rafiki yetu ile pesa angeitoa kwa mtu mwenye shida ingekuja kumuuma endapo angegundua ni yake? Je angeiweka akiba halafu akaja kugundua ni yake si bado ingekuwa ni faida?

Chochote unachowafanyia wengine kinaweza kukurudia wewe wakati wowote.

Wale unaowaumiza kwa makusudi ujue kabisa na wewe unaweza kuumizwa wakati wowote ule na mtu mwingine pia. Je utaweza kuvumilia?

Kabla hujamfanyia mtu yeyote ubaya labda ni kumuibia, kumsaliti, kuua, kutesa, kuumiza kwa namna yeyote ile, jaribu kuona kama unamfanyia mtu unaempenda sana, labda ni mwanao, mke wako, mdogo wako, mama yako, baba yako naa kadhalilka. Je utafurahia kuona wakifanyiwa hivyo? Je wewe utaweza kuvumilia uone umpendae anafanyiwa kitendo cha namna hiyo? Je itakuaje kama hao ndugu za huyo unaemfanyia ubaya wakipanga kukufanyia ubaya wewe au wale unaowapenda?

Ni vizuri kuyatazama matendo yetu ya kila siku kwasababu mara nyingi ndio yanatengeneza watu wabaya tunaowaona kila siku.

Matendo yetu ya kila siku yanatabia ya kutuletea matokeo kwenye Maisha yetu. Unaweza kutenda ubaya ukasahau na mabaya yake yakaja kukurudia wakati ulishasahau kabisa. Chochote unachokifanya kitazame kwa jicho la tatu ona kama ni mbegu ambazo unazipanda na ipo siku utakuja kuvuna matunda yake.

Usichoke kutenda mema.

Nakutakia kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

#usiishienjiani

www.jacobmushi/coach

4 Responses

Leave a Reply to Jacob MushiCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading