Habari rafiki, leo kwenye ujasiriamali tunakwenda kujifunza juu ya kanuni 10 ambazo unapaswa kuzijua wewe mjasiriamali. Ni imani yangu kwa kupitia makala hii utatoka na mwangaza kwenye kile unachokifanya. Kila mmoja anamtegemea mwenzake, kwa kupitia unachokifanya kuna watu wamerahisishiwa maisha yao. Wewe pia kuna watu wengi sana wanahusika kukufanya wewe uishi kwa urahisi. Ni muhimu kuwa mwema kwa kila mmoja wetu.

1.Kuwa Mtatua matatizo

Ili uweze kuwa Mjasiriamali lazima uamue kuwa mtatua matatizo kwenye jamii uliyopo. Hii ni kanuni ya kwanza kabisa, popote unapokuwa lazima ukumbuke kuwa wewe upo kwa ajili ya kuleta suluhisho kwenye jamii yako. Watu wenye mafanikio makubwa duniani ukiangalia mwanzo wao wameanza kwa kurahisisha matatizo ya watu.

Kila fursa inayokuja mbele yako iangalie kwa jicho la mtatua matatizo, jiulize kwa fursa hiyo unakwenda kuwasaidia vipi watu?

2.Kuwa na maono makubwa

Pamoja na kuwa mtu unaeweza kuona fursa kwenye kila tatizo linalokuja mbele yako lazima uweze kuwa na maono. Maono ndio yatakuwa msaada wako wa kufika mbali. Pasipo ya maono unaweza kujikuta umekuwa mtu wa fursa tu. Kila linalokuja mbele yako unafanya bila kuelewa linakupeleka wapi.

Wajasiriamali ni watu wenye maono na sio wapiga dili, yaani wale wanaotazama tu sehemu ya kupiga pesa za haraka haraka kisha wapotee.

Maono yako yanapaswa yawe juu yako binafsi na juu ya kile unachotaka kuleta mabadiliko kwenye dunia hii. Ni lazima ujenge maono makubwa kwasababu tayari tuna watu ambao ni mfano kwetu waliofika mbali sana.

Usiogope kutengeneza maono makubwa kwenye kile unachokifanya.

3.Kuwa na Vipambele.

Ukiwa na maono unakuwa na nafasi nzuri ya kufanyia kazi kanuni hii ya vipaumbele. Mjasiriamali anaetaka kufika mbali lazima awe amejiwekea vipaumbele vyake. Kutokana na maono yake lazima ajue anapaswa kufanya nini na vitu gani hapaswi kufanya kabisa.

Kuna nyakati zinaweza kuja dili nyingi za pesa kama ukiwa sio mtu wa vipaumbele utajikuta unapoteza mwelekeo au wakati mwingine kuingia kwenye kutapeliwa.

Tambua thamani yako,

Tambua uwezo ulionao.

4.Mfahamu Mteja wako

Unapoamua kuwa mtatua matatizo lazima ukubali kuwafahamu hao unaowatatulia matatizo yao. Hapa haina maana uwajue kwa majina hapana. Unatakiwa ujue tatizo unalotatua linawakabili watu wa aina gani.

Je ni watoto?

Wanafunzi?

Wafanyakazi?

Ni wazee?

Uwezo wao wa kipato ni upi?

Hii itakusaidia ujue hata wakati unapanga bei unaweza kupanga kulingana na uwezo wao wa kipato na mazingira waliyopo. Huwezi kusema wewe ni Mjasiriamali halafu hufahamu bidhaa yako inatumika na watu wa aina gani Zaidi.

5.Siku Zote Bidhaa zako Zitimize Mahitaji ya Wateja.

Mfano wewe unauza nguo, na mara nyingi wateja wako wakija kununua nguo zinakuwa haziwatoshi, wewe unawaelekeza kwa fundi nguo aliepo jirani kidogo na duka lako. Siku yule fundi nguo akipata akili akaanza kuuza nguo ujue utafunga biashara.

Hapa namaanisha kwamba kama unachokiuza hakimridhishi mteja atakwenda kwa mtu mwingine anaeweza kumridhisha. Usikubali mteja aondoke ananung’unika.

Kuna watu wanasema huwezi kumridhisha mteja hata ufanye vizuri bado atalalamika. Mimi nakwambia ukiona hivo basi hujajua vizuri wateja wako. Kama kuna sehemu watu wanaambiana kwamba kunahuduma nzuri basi ujue wameridhishwa na huduma.

Kwa kupitia wateja wako kuridhika wataleta wateja wengine Zaidi na Zaidi. Usikubali kutoa huduma mbovu kwa kigezo cha wewe kunufaika.

6.Tengeneza Mpango Mzuri wa Biashara.

Kama Mjasiriamali ili uweze kutimiza maono yako makubwa lazima uwe na mpango wa biashara yako. Mpango ndio ramani ya kule unakoelekea.

Mpango ndio utavuta wawekezaji wakupe mtaji.

Mpango ndio utafanya upate watu sahihi wa kufanya nao kazi.

Utakuwa unafanya makossa makubwa kama huna mpango wa biashara yako. Ni kama mtu anaefuata njia ambayo hajui inampeleka wapi. Hata kama unajua unapokwenda kuwa na mpango ni muhimu.

Mpango wa muda mfupi na muda mrefu wa biashara yako, mwaka mmoja na kurudi hadi siku moja ni mpango mfupi. Miaka 2 na kuendelea ni mpango mrefu.

 

7.Wajibika kwa Kila Linalotokea.

Lazima uwe mtu ambaye unawajibika linapotokea tatizo kwenye baishara yako. Hutakiwi kulaumu wateja, wawekezaji, wala wafanyakazi. Chukua Hatua haraka pale inapohitajika.

Wewe ndio umebeba maono ya biashara yako lazima ukubali kubeba wajibu pale unapohitajika.

Kama mtatua matatizo lazima uweze kutatua vizuri matatizo kwenye biashara yako.

8.Chagua timu sahihi

Ili uweze kuwa na ukuaji mzuri lazima ujenge timu nzuri ya kukuwezesha kutimiza maono yako. Watu wengi wanafeli kwasababu hawajaweza kuwa na watu sahihi kwenye biashara na maono yao.

Vipo vigezo vingi vya kuangalia unapochagua watu lakini muhimu ni uwe na watu ambao wanaziba mapungufu yako. Sio unachagua watu ambao wanakuja kufanya kile ambacho wewe mwenyewe unaweza kufanya.

Pia lazima uangalie watu wenye tabia kama zako, waadilifu na waaminifu, na mwisho kabisa wawe wanaamini kwenye maono makubwa uliyonayo. Ukiwa na watu wasio kuamini utajikuta kila mara unakuwa peke yako. Maana yake ni kwamba kutakuwa na watu wanaokata tamaa njiani.

9. Wekeza Muda Kwenye Ukuaji na Masoko.

Biashara yeyote yenye mafanikio makubwa ilianza chini. Kilichofanya ifike mbali ni pale waanzilishi wake walipoamua kuwekeza muda kwenye ukuaji wa biashara hiyo.

Ili biashara ikue lazima na wewe ukubali kukua, yaani uwe unajifunza kwa bidii ili uendane na ukuaji wa biashara la sivyo itakuja kukushinda huko mbele.

Lazima ukubali kuwekeza muda kwenye masoko na mauzo. Kama huuzi maana yake biashara yako haina mzunguko. Na kama haina mzunguko inakwenda kufa.

Haijalishi una bidhaa nzuri kiasi gani lazima ujitangaze mara kwa mara. Yapo makampuni makubwa yameanzishwa miaka mingi iliyopita lakini bado kila siku utaona wanatangaza bidhaa ile ile kila siku. Hii ni kwasababu usipotangaza watu wanasahau.

10. Usiishie Njiani.

Jambo la mwisho kabisa wewe kama umeamua kuwa Mjasiriamali usikubali kuishia njiani. Usikubali kukata tamaa. Wajasiriamali wakubwa kama kina Bill Gates waliweza kufika sehemu waliyopo sasa hivi kwasababu hawakukubali kukata tamaa na kuacha yale maono yao makubwa.

Pamoja changamoto nyingi lazima ukubali kuendela kubeba maono yako. Hata kama watu watakuacha endelea kusimamia kanuni hii na usikate tamaa.

Kazi imebaki kwako kufanyia kazi Hiki ulichojifunza.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading