KINACHOWATOFAUTISHA MATAJIRI NA MASKINI NI HIKI.

By | November 21, 2017

Ili uweze kutoka hapo ulipo sasa na kufika sehemu nyingine walipo watu wenye mafanikio makubwa ni muhimu sana kujua ni kitu gani kinawafanya muwe tofauti. Ni kitu gani kinawatenganisha na kuwafanya muitwe majina tofauti.

Kitu cha ajabu ni kwamba wote tulizaliwa tukiwa na usawa, yaani kuanzia uwezo wa kufikiri, mazingira, na hata wakati mwingine upatikanaji wa elimu unaweza kuwa sawa lakini bado unakuta kuna walioweza kufika mbali Zaidi ya wenzao.

Ukisema ulizaliwa bila viungo Fulani wapo walemavu wenzako walioweza kufanya mambo makubwa kuliko hata wenye viungo. Hivyo hakuna sababu ambayo unaweza kuitoa ikaonekana ni kweli upo hivyo ulivyo na unastahili kuendelea kuwa hivyo.

Yapo mambo mengi sana yanaweza kuwa sababu ya wewe kuendelea kubakia na umaskini lakini hayo hayatakusaidia chochote hata kama utaendelea kubaki nayo. Unachopaswa kujua ni nini unataka anza kuchukua hatua kufanya kazi hadi upate kile unachokitaka maishani mwako.

Matajiri wanatengeneza na wametengeneza mifumo.

Matajiri wote duniani wana mifumo ambayo wameifanyia kazi miaka na miaka na tunapowaona sasa wanakuwa wanavuna kile walichokipanda kwenye maisha yao. Kutengeneza mfumo kunaanzia mbali sana kwanza kupata watu ambao ni waaminifu na waliojitoa kikamilifu kwa yale maono yako.

Watu wengi wanajitahidi na kuishia njiani kwasababu ya kukosa maarifa ya kutosha na wakati mwingine kuwa na watu wasio waaminifu.

Ni jukumu lako wewe kujua unachotaka. Unataka utajiri wa kiasi gani na aina gani ya maisha kisha uanze kufanya kazi kwa bidi zote hadi ufikie hapo.

Hakuna mtu mwingine ataweza kuja kukusaidia kufika bali ni kwa juhudi zako mwenyewe. Sio kazi rahisi unatakiwa kujitoa kweli kweli kwasababu kama ingekuwa rahisi kila mmoja angeweza.

Uwezo unao, nguvu unazo, muda unao na watu wapo ambao mnaweza kwenda pamoja na kufikia ndoto zako.

Ukiweza kuwa tajiri unakuwa umeisaidia jamii yako kwa kiasi kikubwa sana. Kutatua tatizo la ajira, kurahisisha maisha ya wengi. Kama ni bidhaa unazalisha basi unakuwa unakuza uchumi wa taifa lako.

Watu ambao ni wabinafsi kamwe hawawezi kuwa matajiri kwasababu utajiri unakulazimisha wewe uwe mtoaji. Unakulazimisha uwe mtu ambaye anajali wengine.

Mara nyingi kama wewe ni mbinafsi utaishia kuwa na maisha ya kawaida tu yale ambayo wengi ndio wanayataka. Kuwa na nyumba nzuri, gari zuri na kuweza kulipa ada za watoto wako basi. Maisha ya aina hii ndio watu wengi wanatamani kuwa nayo.

Kumbe kwa kiasi kikubwa unakuwa umegusa maisha yako peke yako na hakuna maisha ya wengi uliyogusa. Ukiwaza kuwa na wafanyakazi elfu moja nyumba, gari, na ada za shule zitakuwa sawa na mtu anaekwenda kununua pipi dukani kwasababu kama ni fedha itakuwepo ya kutosha

Matajiri wana nidhamu kwenye kila wanachokifanya, nidhamu ya muda, nidhamu ya fedha, na kadhalika. Huwezi kuendelea kubakia juu kama huna nidhamu.

Maskini wanatafuta kwa ajili ya kuendelea kuishi.

Mtu maskini ni yule ambaye mar azote anawaza juu yake pekee. Unaweza kuwa na uwezo wa kuishi kila siku lakini kama fikra zako zote zinawaza juu yako wewe na watoto wako tu huna tofauti sana na mtu asiye na kitu.

Maskini wote wanapambana kutafuta pesa ili tu waendelee kuishi. Kukosa pesa kwao ni kushindwa maisha.

Toka kwenye mawazo ya kutafuta pesa kwa ajili ya kuishi anza kuwaza vikubwa Zaidi.

Jinsi unavyofikiri ndivyo utakavyokuwa. Kama unafikiri kwamba hakuna njia ya kufanikiwa kimaisha basi ndivyo itakavyokuwa. Kama unafikiri wewe ni maskini kwasababu wazazi wako hawakukusomesha basi utakuwa hivyo.

Ukitaka kutoka hapo ulipo unatakiwa uanze kupambana na fikra ulizozijenga au kujengewa tangu ukiwa mtoto.

Asilimia kubwa ya maskini wanateswa na fikra potofu walizonazo. Kufikiri kwamba matatizo yako yanasababishwa na mtu Fulani huko ni kupotoka kimawazo.

Kufikiri kwamba haiwezekani watu wote wakawa matajiri huo pia ni ubovu wa fikra. Lazima kwanza uanze kupona ndani yako.

Wengi wanaanza na kuishia njiani kwasababu ya kukosa nidhamu. Wanafanya mambo mengi kwa mazoea. Wanafanya kwa uvivu. Juhudi wanaweka kidogo lakini wanataka matokeo makubwa.

HATUA ZA KUCHUKUA;

Tambua ni kwanini umezaliwa duniani (Soma kitabu; SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO)

Jua una uwezo gani ndani yako

Tambua ni wapi unakotaka kufika.

Anza sasa safari ya kuelekea kule unakotaka.

Jitoe kikamilifu kwa ajili ya ndoto yako. Usikubali mtu yeyote Zaidi yako mwenyewe awe sababu ya wewe kuacha. Kuwa na nidhamu katika kila unalolifanya. Weka bidii na juhudi kuliko mtu mwingine yeyote.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *