KONA YA BIASHARA: Hiki Ndio Sababu ya wewe Kuanguka Kibiashara

jacobmushi
By jacobmushi
2 Min Read

Kinachoshangaza sana kwa biashara nyingi za kwetu ni kwamba wamiliki au walioajiriwa kwenye biashara ndio wanaongoza kwa kudharau, kuongea vibaya na wateja wao.

Mteja anapoamua kuja kwenye biashara yako sio kwamba ana shida sana, wewe ndio una shida na hela ndio maana ukafungua hiyo biashara, ungekuwa huna shida na pesa ungekaa nazo nyumbani ukatumia.

Mteja ameacha biashara nyingi sana akaamua kuja kwako, usianze kumuangalia kwa nje na kusema huyu sio mnunuaji, hawa wanaulizia tu na kuondoka, ndio wanaulizia na kuondoka lakini pale ambapo walipokelewa vizuri ndio wataweza kuja kununua siku nyingine.

Unajua kama umeanzisha biashara yako mteja ndio boss wako?

Mteja ndio anakuwezesha ulipe kodi, ulipe TRA, na uweze kuendeleza biashara.

Kama hutaweza kuongea vizuri na mteja wako usitegemee kukua.

Jifunze kuwa mpole mbele ya mteja wako la sivyo utarudi nyumbani.

Ifanye biashara yako iwe kimbilio la mteja. Mtu akitaka huduma nzuri awe anafikiria kwako, mtu akitoka nyumbani na stress zake akifika kwenye biashara yako haijalishi ni kitu gani unauza ajisikie faraja.

Mteja ametafuta pesa kwa nguvu akaamua kuja nazo hapo kwako onyesha kumjali, onyesha kujali pesa zake.

Pesa zake ndio zinafanya Maisha yako yaende sio bidhaa zako bora sana. Unaweza kuwa na bidhaa bora mno lakini kama hakuna wateja haina maana.

Jitazame kuanzia unapomkaribisha mteja hadi unapomuelezea bei. Hata kama umebandika bei akiuliza usijifanye wewe ni mkali, kuwa mpole maana unatafuta hela.

Usimlazimishe mteja anunue kitu ambacho hakipendi jaribu kumuonyesha tu kwanini anunue kile unachotaka kumwambia. Tumia lugha nzuri na maneno yenye busara ambayo ungependa wewe ujibiwe unapotaka kununua kitu.

Kumbuka watu hawanunui bidhaa wanakununua wewe. Vile unavyoongea nao, vile unavyoonyesha kuwajali, vile unavyowafanya wawe kama marafiki zako.

Kumbuka kuna wengi tu wanauza unachouza je wewe unatofautiana nao na kipi? Bidhaa bora peke yake haitoshi lazima uongeze ubunifu kwenye kuuza.

Jacob Mushi,

Mwandishi, Mjasiriamali, Kocha wa Maisha, Mshauri na Mtaalamu wa Blogger 

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading