Utaishia Kuwa mtu wa kuvunjika moyo siku zote kama utakuwa unatarajia mambo yaende kama vile ulivyopanga na unavyotaka. Siku zote tunapanga na tunatarajia lakini mambo yanaweza kuja tofauti.

Mambo kuja tofauti haitakiwi iwe sababu ya wewe kukata tamaa na kuikimbia biashara. Kumbuka kwmaba ndio unapanda mbegu.

Umeanza biashara yako ukajiwekea malengo makubwa na matarajio makubwa lakini ulipoanza mambo yakaanza kuonekana tofuati, unatakiwa ujipe muda.

Umefanya matangazo ya kutosha ukiwa na hamasa kubwa na ukajiwekea kwenye mtazamo wako kwamba watakuja wengi lakini matarajio yako yakakuangusha hajatokea mtu hata mmoja, Jipe muda.

Usiwe mtu ambaye anakata tamaa haraka kwasababu matokeo hayajaja vile ulivyokuwa unataka. Unachotakiwa kuelewa ni kwamba hao waliokukataa ni asilimia ndogo sana ya wateja ambao hujawafikia bado.

Unapokatishwa tamaa jipe moyo kwa kusema huyu hakuwa wa kwangu, wa kwangu yupo mbele. Endelea mbele, endelea kutangaza. Endelea kuwaambia watu kuhusu bidhaa zako huku ukijipa muda wa matokeo.

Nakumbuka kuna kipindi nimekaa sehemu hali yangu ya kifedha haikuwa nzuri sana kipindi hicho. Nikapokea simu ngeni alikuwa ni mteja anataka bidhaa ambazo nilimwambia miezi kama sita iliyopita. Bidhaa zile zilikuwa ni za gharama kubwa kidogo hivyo nikatengeneza pesa za kutosha kwa simu moja niliyopokea.

Siku nyingine nilikuwa nimetangaza bidhaa kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu bila ya kupata mteja. Siku moja nimekaa nafanya shughuli zangu, nikapokea simu ya mteja anasema ameona bidhaa zangu Facebook, nikamwelekeza namna ya kulipia akafanya malipo nikamtumia bidhaa. Alichukua bidhaa nyingi kiasi kwamba niliweza kurudisha gharama zote zilizotumiaga za matangazo nab ado nikabakiwa na fedha nyingine ya kutosha.

Mifano hii miwili inakufundisha kwamba chochote unachokifanya sasa hivi hata kama huoni matokeo yeyotea endelea mbele. Mteja unaeongea nae sasa anaweza kuja kununua miezi mitatu baadae. Matokeo ya kazi kubwa unayoifanya sasa hivi unaweza usiyaone sasa hivi jipe muda wala usiwaze sana juu ya namna watu hawapokei kazi zako.

Jipe muda wa kutosha.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading