Mojawapo ya vitu vinavyofanya biashara nyingi zikwame au zifike mahali zikose mwelekeo ni wengi kutokujua kwanini wapo kwenye biashara wanazofanya. Wakati mwingine unaweza kujua kwanini lakini hicho kinachokufanya uwepo kwenye biashara kikawa ni kikwazo kwa biashara yako kukua.

Kama utaanza biashara kwasababu umesikia kwa watu kwamba inalipa jiandae kuishia njiani.

Kama utaanza biashara kwasababu kuna shida zako unataka kutatua kuna nyakati hizo shida zitakwisha na utashindwa kuendelea.

Kama shida yako kubwa ni kupata pesa kwenye biashara ukishaanza kuzipata unaanza kuacha kuweka juhudi, unaacha ubora na kila kitu kilichokufanya ukafikia hapo kwenye pesa.

Unachopaswa kutambua ni kwamba wateja hawaji kwenye biashara yako kwasababu ya matatizo yako bali ni kwa matatizo yao wenyewe. Ijapokuwa utawatafuta wewe lakini watafanya maamuzi wakiona kuna tatizo lao linatatuliwa na biashara yako.

Kila biashara yenyewe ina kusudi lake na kusudi kuu la biashara karibu zote ni kutatua matatizo ya watu. Ukishindwa kujua kusudi la biashara yako utakuwa unakaribisha kifo cha biashara mapema.

Kinachofanya biashara nyingi zinakufa ni kwasababu waanzilishi wengi wanakuwa wanatazama yale matakwa yao Zaidi. Hivyo kama mtu anaona hakuna anachopata katika yale aliyotarajia anakata tamaa kabisa.

Ukishajua kwanini biashara yako inatakiwa iwepo kwenye jamii na sababu hiyo ikazidi sababu zako binafsi ukaanza kuzifanyia kazi utafika mbali kuliko hata ulivyokuwa unataka.

Shida zako binafsi ni ndogo sana kuliko ukubwa wa biashara unayoifanya. Matajiri wakubwa duniani wangekuwa wanatazama shida zao binafsi nadhani ni siku nyingi wangekuwa wameacha biashara kwasababu kama ni pesa wanazo za kuwatosha hadi siku wanakufa nab ado vizazi vyao vitaendelea kufaidi.

Angalia sana sababu kuu inayokusukuma wewe kufanya biashara kama ni matatizo yako binafsi basi badili mtazamo wako ili uweze kupata makubwa kuliko uliyokuwa unatarajia.

Watu wote walioweka maisha ya wengine mbele kuliko ya kwao ndio wamefikia mafanikio. Wengine wote wanaojitanguliza wao wanaishia njiani siku zote. Ukishaanza kuangalia ni faida gani unapata mapema kabla hata hujafika popote unapotea.

Tazama mbele Zaidi na njia nzuri ya kuona mbele ni kuangalia namna unavyowasaidia wengi kupitia biashara yako.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading