Leo kwenye kona ya biashara tunaangalia makossa matatu ambayo unafanya na yataua biashara yako siku si nyingi. Kama kawaida ni mambo madogo sana ambayo yanaweza kusababisha ukapoteza kila ulichonacho hasa kama yatakuja taratibu na kuleta madhara bila ya wewe kujua na ukaja kutambua madhara yakiwa makubwa kabisa.

Kuna baadhi ya makossa unayafanya yanakuwa kama kansa yanaharibu taratibu ndani kwa ndani ukija kuona matokea kwa nje ujue hakuna namna tena ya kutatua. Kwenye maisha huwezi kuzuia tena ila kama ni biashara itakubidi uanze tena upya.

Kuridhika na matokeo Unayopata sasa.

Mojawapo ya tabia ya binadamu ni kuridhika na matokeo ambayo anayapata hasa kama anakuwa hana changamoto yeyote. Na changamoto zinapoanza kuja ndipo mtu hugundua na kuanza tena kuchakarika. Sasa na kwenye biashara kuna nyakati utaanza kuona faida vizuri na ukaanza kusahau kwamba kuna mahali ulikuwa unakwenda. Kama ni ndoto ya kumiliki biashara kubwa basi ukaanza kuisahau kwasababu ya faida kidogo ulizoanza kuona.

Ni muhimu sana ujue unapokwenda haijalishi mambo yako vipi. Uwe unatengeneza pesa au hutengenezi jua unapokwenda na uwe unapatazama kwa makini sana. Kuna nyakati unaweza kujisahau ukaona ya nini tena kujisumbua mbona hizi ninazopata zinatosha kabisa. Lakini siku yakija mambo mabaya utaanza tena kukimbizana.

Huna Ukurasa/Blog ya Biashara Yako.

Dunia inabadilika sana kama hadi sasa unavyosoma hapa huna ukurasa wa biashara yako kwenye mitandao ya kijamii halafu unaniambia una ndoto ya kumiliki biashara kubwa utakuwa unanitania. Unajua ni kwanini? Dunia sasa ipo kiganjani kama wewe utasahau kwamba watu wakitembea barabara wanatazama simu zao Zaidi kuliko hata mabango yaliyopo barabarani utakuwa umeanza kupotea.

Watu wanawasha Tv lakini huku macho yapo kwenye simu zao. Sasa hivi mtu akipata shida yeyote anakwenda google kuuliza sasa wewe hadi leo huna mitandao hii ya biashara yako utakuwa haupo makini na hicho unachokifanya kwakweli.

Anza leo kutengeneza ukihitaji msaada tuwasiliane.

Kuiga kwa Mshindani wako/Kupambana Nae.

Kosa jingine kubwa unalofanya ni kuiga kwa mshindani wako badala ya kuangalia ambacho unafanya cha tofauti. Ni kweli unapaswa kujifunza lakini sio kuiga kila kitu. Boresha kile unachokiiga ili wengine waone utofauti wako na yeye.

Usipoteze muda wako kupambana na mshindani yeye sio sababu ya wewe kuwepo kwenye biashara. Upo kwenye biashara ili kutatua matatizo ya wateja wako na sio mshindani wako. Usitumie muda wako kumsema vibaya mbele ya wateja wako. Kama utakosa cha kuongea ni bora ukae kimya. Unapomsema kuna wateja watajaribu kwenda kuona kama ni kweli. Bahati mbaya unakuta na wewe maneno yako ulijaza chumvi mteja atakuhama.

Usipoteze hata sekunde yako kumsema mshindani wako. Kwanza huyo sio adui yako. Hata akiiga unachokifanya wewe huna haja ya kuchukia jione kwamba wewe ndio uko juu hadi wanakosa ubunifu wanakuja kuiga kwako. Tafuta kitu ambacho hawataweza kuiga na uweke nguvu hapo.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading