Mwaka ndio huoo unakwisha umefikia wapi na malengo yako? Yaani ndio hivyo mwaka unaishaga ni sekunde moja inacheza na kutengeneza dakika na dakika nayo inakwenda hadi masaa 24. Kunakuwa asubuhi, mchana, jioni na hatimaye usiku siku inapita. Hivyo ukidhani kuna kitu cha tofauti kwenye mwaka mpya utakuwa unakosea. Utofauti wa mwaka unaweza kuwa ni majira tu hasa vipindi vya mvua na jua. Jua linaweza kuwaka sana ua mvua ikanyesha sana hayo ndio mambo yanayoweza kuwa mapya. Maisha yako yatakuwa mapya kama wewe mwenyewe utaamua kubadilisha vile vitu ambavyo unavifanyaga kila siku. Na vitu hivi vinabadilishwa kwa kubadili fikra zako. Ukibadili unavyofanya kila siku utabadili matokeo yako. Utatengeneza mfumo mzuri wa Maisha ambao utakuletea matokeo bora Zaidi kwenye kila sehemu ya Maisha yako.
Tuachane na hilo tuje kwenye mada husika ya leo. Tunazungumzia jinsi gani ambavyo unaweza kufikia mafanikio unapoanza na biashara ikiwa ndogo kabisa. Hapa watafiti wanasema biashara nyingi ndogo hufa sana mara nyingi baada ya kuanzishwa. Hivyo ni muhimu ukajifunza vyema somo hili ili ujue ni namna gani utaweza kuepuka kufa kwa biashara yako.
“Wealth is largely a result of habit.”
Jack Astor
Utajiri ni Matokeo makubwa ya tabia – Jack Astor
Kama unataka kufikia mafanikio kwenye biashara uliyoianzisha jua ni tabia gani unazotakiwa uzitengeneze na kuzifanyia kazi kila siku hadi zikuletee matokeo ya mafanikio makubwa au utajiri.
- Start Again (Anza/Rudia tena)
Haijalishi umeshindwa mara ngapi haimaanishi ndio mwisho. Bado ukisema uache kufanya biashara Maisha hayatakuwa marahisi. Hakikisha unaivuka changamoto hii ya kushindwa na kuacha. Hapo unapoachia ndipo sehemu itakuwa inakusumbua kila wakati na hata ukifanya kingine hutaweza kuendelea mbele utakwamia pale pale ulipokwamia kwenye biashara ya mwanzo.
Kitu cha kufanya hakikisha umeweza kulitambua vyema tatizo la kushindwa kwako liko wapi. Halafu hakikisha umejua ni nani huyo anaesababisha hilo tatizo. Mara nyingi 90% mchangiaji mkubwa wa matatizo kwenye biashara yako ni wewe mwenyewe. Malizia kwa kutafuta suluhisho, utavukaje hapo ulipokwama? Kama shida ni madeni yamekuwa mengi basi tafuta suluhisho. Kama hakuna wateja tafuta suluhisho, kama ni kingine chochote tafuta suluhisho. Hakuna tatizo lisilokuwa na suluhisho.
Ukipata suluhisho hakikisha unaitumia vyema uvuke hapo. Uendelee na safari yako ya mafanikio.
Rudia, Rudia Rudia Tena
- Learn through mistakes (Jifunze Kupita Makosa Yako)
Ili kutofanya makosa ya kujirudia hakikisha unajifunza. Kila changamoto unayoipitia hakikisha unapata somo ambalo halitafanya urudie tena kosa. Siku zote naamini mtu anapovuka changamoto Fulani kwenye Maisha anakuwa mtu wa tofauti anabadilika anapanda viwango.
Mfano: (Huwa nawashangaa sana wale watu wanakata tamaa kabisa kwenye mahusiano wanapoachwa au kutendwa. Ni kweli moyo unauma lakini lazima ujue kwamba kwa hilo ulilopitia hutakiwi uwe mtu wa kawaida kwasababu ni changamoto umeivuka. Imekufumbua macho ukajua kumbe kuna haya natakiwa niwe makini Zaidi.
Sasa wewe ukisema haya mapenzi sitaki tena. Utakuwa unakosea sana maana huku duniani haupo mwenyewe. Kama umeumizwa tumia nafasi hiyo kuwa mtu bora Zaidi usiwe tena legelege. Jua udhaifu wako uko wapi. Jifunze jifunze jifunze. Hata ukiwa na mwingine hauwi tena mtu wa kawaida. Ukiishia kuwachukia watu na kuona sijui hawafai utateseka tu bure maana hata hawajali kwanza hawajakuumiza wao. Mara zote ninapokutana na mtu ameachwa hua napenda kujua amejifunza nini kupitia changamoto hiyo. Na siku zote huwa na mwambia usije kusema ndo mwisho sitopenda tena maana bado upo duniani na haushi peke yako huku duniani. Jifunze jua makosa yako wapi. Wewe unahusikaje katika tatizo. Kuwa makini kosa lisijirudie tena. Hata kama utaumizwa tena isiwe kwa changamoto ile ile kwasababu ulishajifunza.)
Hivyo kwenye biashara waweza kutumia mfano huo kujifunza kwa makosa yako.
- Be Persistent (Kuwa Sugu/endelea Kufanya)
Energy flows to where the concentration goes.
Nguvu siku zote huelekea sehemu ili unapoweka mkazo wa kufanya. Kama una mambo kumi unafanya kuna moja utakuta unalifanya vizuri Zaidi kwasababu ndio unalipa mkazo Zaidi.
Ili uweze kuwa mtu wa kufanya mambo kwa muendelezo ni muhimu sana ukaifahamu biashara yako kwa undani Zaidi. Ifahamu kuliko mtu yeyote. Hii itakupa nafasi ya kuifanya vizuri. Hujawahi kuona mama akiona mtoto analia tu ameshajua tatizo ni nini? Mtoto hawezi kusema lakini kwa vile mama anamfahamu mwanawe vyema anajua huyu ni tumbo linamuuma. Na biashara yako unatakiwa uielewa kwa kiwango cha juu sana ili linapotokea tatizo lolote uweze kulitatua mapema kabla halijawa kubwa na kuja kukushinda.
- Be positive (Kuwa Chanya)
Matatizo unayopitia unatakiwa uyafikiria katika mtazamo chanya. Ukifkiri kwa mtazamo hasi ndio yataharibu ile nia yako. Yatakufanya uchoke. Akili chanya siku zote huleta matokeo chanya. Kila unalopitia lipo kwasababu maalumu. Na sababu hiyo ni njema sana. Kuwa chanya kwenye kila linalokuja ili uweze pia kuishi kwa furaha.
- Build a support network (Tengeneza Timu ambayo Intakusaidia)
Katika maisha tuna marafiki na watu wa aina mbalimbali. Kuna watu waliotuzidi vipato na umri pia. Hawa ni watu ambao unatakiwa ukae nao vyema ili uweze kupata msaada pale yanapotokea mambo magumu.
Tafuta watu waliokuzidi kwenye kile unachokifanya. Tafuta watu wanaofanya kama wewe ambao mnaweza kushauriana.
Mfano mdogo: wewe ni mwimbaji wa nyimbo halafu una marafiki wa karibu ambao sio waimbaji kabisa. Hawajui chochote kwenye uimbaji wao wanapenda tu kusikiliza nyimbo. Ukitoa wimbo halafu ukawatumia kwanza wasikilize wakupe maoni wanaweza wakausifia wimbo tu maana hawajui chochote juu ya wimbo. Lakini ukimtumia mwimbaji mwenzako akausikiliza anaweza kukushauri mengi. Atakwambia hili neon ungetamka hivi. Huu mziki umekuwa mkubwa sana. Na mengine mengi ambayo wale marafiki wasio waimbaji wasingeweza kujua.
Maana yangu hapa ni lazima uwe na watu aina zote wanaokushauri na wanaopokea kile unachotoa. Ukiwa na wapokeaji tu unaweza kukosea na wasijue Na wewe pia usijue kama umekosea. Kila mtu ana sehemu yake kwenye Maisha yako. Tengeneza mtandao wa watu ambao ukikwama watakuwa pembeni yako.
- TAFUTA KIONGOZI.
Huyu ni Mtu ambaye atakuwa karibu yako na utakuwa unampa taarifa zako zote za biashara unazofanya. Kuna tabia ni ngumu sana kuacha bila kusimamiwa. Mfano tabia ya kuweka akiba na kuwekeza.
Kubali kuwa chini, kubali kuwa mwanafunzi ufundishike ndio utafikia mafanikio. Nimesoma vitabu vingi katika vitabu unakutana na mwandishi anasema aliongozwa na mtu Fulani akafikia mafanikio aliyonayo. Sasa wewe ni nani usioongozwa? Mimi hapa nakuandikia lakini nina mtu anaenifuatilia na kunishauri. Nikipitia changamoto ananishauri kwa kila hatua ninayopiga.
Tatizo kubwa tulilonalo tuna watu wengi wanaodhani wanajua kila kitu wanafikiri labda wao wanaweza wenyewe. Kama ingekuwa rahisi hivyo kusingekuwa na vitabu vya kusoma ili ugundue maarifa na kuyatumia.
Jacob Mushi
USIISHIE NJIANI
“Piga Hatua”