Shida kubwa haipo kwenye biashara mara nyingi shida kubwa ipo ndani yako. Unajua kwanini nasema hivyo? Kama biashara unayoifanya wewe kuna mwingine anaifanya vizuri kuliko wewe na ana mafanikio shida haipo kwenye biashara shida ipo kwako. Shida ipo kwako kwasababu hutaki kufuata hatua unataka kuruka ufike kule unakotaka.

Unataka kukimbia wakati bado hujakomaa kwenye kutembea. Unatamani uanze kuajiri wakati wewe mwenyewe bado ni mzembe. Unataka mtaji mkubwa na huo ulionao sasa umeshindwa kuukuza kila siku unakula hadi mtaji.

Wanasema huwezi kuwapa mimba wanawake tisa utegemee mtoto ndani ya mwezi mmoja. Ule ni ukuaji lazima ufuate taratibu za asili. Ndivyo ilivyo kwenye biashara ukikimbilia kumiliki kikubwa kabla hujakomaa kwenye hichi kidogo ulichonacho utashindwa kuendesha kikubwa.

Huwezi kujifunza gari ndogo kabla hujaiweza unataka lori ukaendeshe kwa fujo barabarani. Lazima utahitaji mtu wa kukaa karibu na wewe maana lori linahitaji nguvu yake na ujasiri mkubwa Zaidi.

Endelea kukua kidogo kidogo hadi utaweza kufikia kile unachokitaka. Usione wengine wana kubwa ukatamani ukajidharau na kidogo ulichonacho.

Njia nzuri ya kukuza biashara yako ambayo ni ndogo unatakiwa kwanza uhakikishe unajua faida unayoipata. Faida unayoipata kama hutegemei kikubwa kwenye Maisha yako ya kila siku iongezee kwenye mtaji. Ongeza vile vitu unavyozani vimepungua kwenye biashara au bidhaa zinazouliziwa mara kwa mara.

Ukifanya hivyo mara tatu utakuwa umeukuza mtaji kwa kiasi kikubwa. Unapopata faida hata kama unaitumia usikubali kuitumia yote. Hakikisha kuna asilimia inarudi katika kukuza mtaji wa biashara yako. usikimbilie kukopa kama bado biashara ni ndogo. Hakikisha kwanza biashara imekuwa kiwango cha kuweza kukopa. Kiwango ambacho unakuwa na uhakika wa kipato cha kurejesha mkopo na ubakiwe na faida nyingine.

Ukiona hujapitia changamoto zozote zile ujue kuna vitu vya tofauti bado hujajaribu. Endelea kujaribu vitu ambavyo unaona vitaleta mchango wa tofauti kwenye ukuaji wa biashara yako. unapopitia changamoto usikate tamaa bali tafuta ni somo gani umepata. Ukipata hasara usikimbilie kulalamika au kusema unaacha biashara. Tafuta somo ulilojifunza kwenye changamoto uliyopitia.

Unapopitia changamoto zinakujenga na kukufanya uwe na ukuaji imara ambao hutakuja kuyumba tena baadae. Ni sawa na mtoto anaekua kama hajawahi kuanguka unakuwa na mashaka naye kwasababu akija kuanguka ukubwani ataumia sana. Changamoto unazopitia sas hivi zinakufanya ukomae.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading