Unaweza kuwa na sababu za kila aina zinazoelezea kwanini hadi sasa huna unachokifanya au hujamiliki biashara yako. Swali langu kwako litakuwa ni unachoweza kufanya ni kipi? Tukiacha hizo sababu unazotoa je hakuna hata kitu kimoja kidogo unaweza kufanya? Hakuna kweli? Hakuna unachojua Zaidi ya wengine hapo mtaani kwenu kweli? Hakuna biashara inayoendeshwa hovyo hovyo hapo mtaani uende ukakae nao ufanye vitu vya tofauti hadi wakuambie ujiunge nao kweli? Sasa utakuwa unafanya nini hapa duniani kama hakuna hata kitu kimoja unachoweza kufanya vizuri Zaidi ya wengine wachache waliokuzunguka?
Inawezekana huna hela kabisa hapo ulipo lakini unaweza kuzungumza na watu vizuri ukawashawishi. Hapo mtaani kwenu kuna mama anauza maziwa ya mtindi lakini hajui kuyauza vizuri wala kushawishi watu. Wewe tumia uwezo wako wa kuongea na watu na kuwashawishi uuze maziwa kama kwenye kila lita moja ya maziwa ukiweza kutengeneza sh 300 hadi 500 sio sawa na ambaye hana kazi ya kufanya.
Rafiki yangu mmoja akaniambia yeye alikuwa chuo kikuu na hakubahatika kupata mkopo. Aliishi kwa shida sana hadi siku moja alipopata wazo la biashara. Pale alipokuwa ananunua chakula kila siku kwa tsh 2,000 aliamua kuongea na yule mama muuzaji. Akamwambia nitachukua sahani kumi kila siku jioni lakini utakuwa unaniuzia kwa sh 1500. Yule mama akakubali mwanafunzi yule akawafata marafiki zake aliokuwa anaishi nao akawaambia nitakuwa nawaletea chakula hapa kila siku jioni.
Wenzake wakakubali ikawa kwenye kila sahani kumi anatengeneza tsh 5000. Akaongeza bidii akaweza kuwahudumia wengine hadi sahani 20 kila siku jioni. Aliendelea na biashara ile kwa ule muda wake wa ziada wa jioni kila siku na akapata pesa ya kuendeshea Maisha na mahitaji mbalimbali aliyokuwa nayo.
Kuanza biashara unaweza kuanza kwa namna yeyote ile inategemea tu na mtazamo wako ulivyo. Kile unachokijua ukiweza kukitumia vizuri kitakutoa.
Jifunze kuuza, ukishajua kuuza tafuta bidhaa ambayo utaijua vizuri sana kisha utafute wateja wake. Hakikisha una uhakika wa upatikanaji wa bidhaa unayotaka kuuza. Tafuta wateja kachukue bidhaa peleka kwa wateja wako. Unaweza kutengeneza faida kidogo lakini sio sawa na mtu ambaye hauzi chochote, au anaelalamika hana kazi wala biashara.
Huo unaweza kuwa mwanzo wako mdogo lakini una malengo makubwa ya kuja kumiliki biashara yako mwenyewe. Mawazo ya biashara yapo mengi sana na unaweza kuanza kwa namna ya ajabu sana lakini hakuna watu wanaoweza kuwa na fikra chanya za kugundua hayo.
Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi
#UsiishieNjiani