Ni vyema kwa kila mmoja akaweza kutambua ni wapi ana mapungufu na kuyafanyia kazi kabla hayajaleta madhara kwenye kazi. Kila binadamu ana mapungufu yake ndio maana haupo mwenyewe huku duniani.

Kuna sehemu unateleza na yupo mtu ataweza kuwa msaada wako.

Unapoyajua mapungufu yako unajipa nafasi ya ushindi mzuri kwenye biashara yako. Ukae ukijua kwamba mapungufu yetu ndio mara nyingi yanakuwa sababu ya sisi kushindwa vitu mbalimbali hivyo unapoweza kutambua wewe ni dhaifu sehemu gani utaweza kuandaa mazingira mapema.

Biashara yako inakuwa kutokana na wewe ulivyo. Kama utashindwa kujijua vizuri na kujitengeneza utajikuta unatengeneza kitu ambacho kimebeba mapungufu yako yote. Ukiweza kujitambua vizuri unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujua ni nafasi gani inapasa kujazwa na wengine.

Usipojua mapungufu yako unajikuta hujui ni sehemu gani ya kuboresha. Ni sawa na chungu kinachovuja usipojua palipotoboka kuendelea kujaza maji sio suluhisho. Suluhisho ni kuziba palipotoboka.

Unajua nguvu zako nyingi utawekeza kule ambapo unaweza vizuri na kule ambapo una mapungufu utatafuta watu wa kuziba mapungufu yako. Hapo ndipo unaweza kufikia mafanikio ya biashara yako.

Usipojua jua mapungufu yako unaweza kujikuta unadumaza biashara bila ya kujua chanzo ni nini.

Leo andika yale mambo ambayo unayaweza vizuri sana na yale ambayo yanakupiga chenga. Angalia ni hasara kiasi gani unapata kwa kutokuyafanya kwa ubora yale ambayo yanakupiga chenga. Ona ni watu aina gani ukiwaweka kwenye hizo nafasi wanaweza kuleta ufanisi wa hali ya juu na kusababisha biashara yako ikaongezeka katika ukuaji.

Rafiki Yako

Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading