Kufanikiwa Au Kufa 1/11/2018

By | November 1, 2018

Ukitaka vitu vya tofauti ni lazima ukubali kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya. Kama unataka kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya lazima ukubali kufanya maamuzi magumu ambayo hata watu wa karibu wanaokutazama wanaweza kuogopa.

Kama utaendelea kubaki hivyo ulivyo na ukafanya unayoendelea kufanya kila siku maana yake utapata matokeo yale yale na hutasogea mbele hata kidogo. Wanajeshi wanapoenda vitani huwa akili mwao wanakuwa na chaguzi mbili tu yaani kushinda au kufa. Hawawezi kwenda na mpango wa kushindwa au matarajio ya kushindwa. Kushindwa maana yake kwao ni kuuwawa.

Wewe unapoweka malengo yako makubwa lazima ukubali kujitoa kwa kiwango cha juu sana kuliko mtu yeyote. Lazima ukubali kuweka makubaliano kati yako wewe nna ndoto zako. Kubali kwamba hatua ambazo unakwenda kuchukua sio za kawaida japokuwa watu wengine wasioelewa wanaweza kukuona kama umechanganyikiwa lakini kwako binafsi wewe unajiona kule unakotaka kufika.

Usipokubali kujitoa sadaka wewe mwenyewe ili ndoto zako zitimie hakuna mtu mwingine atakuja kufanya hivyo. Rafiki naomba nikwambie watu wote unaowaona wamefikia hatua kubwa sana za mafanikio walijiambia kwamba lazima wafanikiwe na wakaanza kuchukua hatua kubwa sana za yale ambayo wanayataka.

Kama wewe utaendelea kuwa mtu wa kujitetea basi utaziua ndoto zako. Ukiziua ndoto zako unakuwa huna tofauti na mtu ambaye amekufa. Kama mwanadamu hana ndoto wala hana jambo lolote analolipigania hapa duniani hana maana ya kuwa hai.

Kufa kwa ndoto zako ni sawa na wewe umekufa ni yule mtu ndani yako amekufa, usikubali kukata tamaa au kukubali kuendelea kuishi kama wengine waliokata tamaa. Kaa mbali kabisa na watu wanoalalamika na waliokwisha kufa ndani yao.

Kaa mbali kabisa na watu ambao hawana malengo makubwa ya Maisha yao kwasababu watakuambukiza ule udogo walio nao. Chagua watu ambao unafanana nao na uanze kuruka pamoja. Haijalishi mtu ni Rafiki yako kiasi gani linapokuja suala la Maisha yako unapaswa watu wasiokupa nafasi ya kusonga mbele uwaweke pembeni.

Fanya maamuzi magumu Rafiki, amua kufanikiwa au kufa. Kufa ni kuendelea kubaki hivyo ulivyo, kufa ni kuziua ndoto zako. Kufa ni kuyaacha yale mawazo makubwa yaliyokuwa ndani yako yapotee.

Mimi binafsi nimechagua kufanikiwa na chochote kitakachojaribu kunizuia ni labda kitapotea hicho ili mimi nisonge mbele au ni mimi nitapotea ili kisiweze kunizuia tena. Haijalishi kitakuwa ni kitu gani au ni nani mimi sitakuwa tayari kuvumilia mtu au kitu kinachojaribu kunizuia.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

9 thoughts on “Kufanikiwa Au Kufa 1/11/2018

 1. Christopher mwijage

  Asante sana kwa makala bora ya kutufanya tuweke juhudi kufikia mafanikio makubwa tunayotaka ktk maisha yetu.
  God bless you brother.

  Reply
 2. kabendera de byser

  binafsi nashukuru sana kiongozi kwa makala nzuri zinazozidi kutuhamasisha kuacha uwoga na kuchukua hatua kubwa zaidi kuelekea mafanikio yetu….yani mafanikio ni lazimaa ??

  Reply
 3. Christopher mwijage

  Jacob asante sana napata sana hamasa ya kusonga mbele kwa makala hii, yaani nifanikiwe au kipotee kizuizi

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *