Kuku, Kunguru na Tai.

By | April 14, 2016

Ukiona tai na kuku wapo pamoja wanatafuta chakula ujue tayari tai ameshapoteza mwelekeo. Mwanamafanikio mwenzangu ni kwamba kuku hana msaada wowote kwako juu ya kupaa kwako juu ya kwenda juu zaidi.

Wewe kama mtu unaetaka kufika mbali unaetaka kupaa juu kama tai tafuta tai wenzako kuku atafundisha mbinu za kukaa hapa hapa chini, kuku atakufundisha jinsi ya kufukua chini. Hana cha kukusaidia juu ya safari yako ya mafanikio. Kua makini na jaribu kutambua kuku ni yupi na tai ni yupi.

Wakati unatafuta tai wenzako usisahau kuna kunguru pia kunguru wanatamani kufika juu lakini wanavutwa na vitu vilivyopo huku chini jaribu pia kua makini maana unaweza kumkimbia kuku ukajikuta umetua kwa kunguru. Kunguru tabia zake zinafahamika anapenda kula majalalani.

Unaweza ukawa unajidanganya kwamba unaweza kuwabadilisha wakawa kama wewe ila ukweli ni kwamba wewe ndio utakaebadilishwa jitahidi kukaa mbali nao haijalishi utakua na mpweke kiasi gani ndio mafanikio yalivyo.

Pia wanasema ndege wafananao wanaruka pamoja,  tukikuona na kuku tunajua wewe ni kuku, tukikuona na kunguru tutajua wewe ni kunguru,  tukikuona na tai tutajua na wewe ni tai mwenzetu.

Tai hakati tamaa kirahisi hata kama kuna upepo mkali na mawingu havimfanyi arudi chini.

Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba kipindi hiki tuna tai wengi ambao bado hawajajitambua kama wao ni tai. Ni imani yangu kwamba kama umeweza kusoma hapa uko kwenye kundi la Tai hongera sana na endelea kupambana safari bado ni ndefu.
 Asante sana na Karibu
©Jacob Mushi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *