Kwanza nataka ujijengee mtazamo huu kwenye akili yako, tatizo lolote linapotokea kwenye Maisha yako usiwe mwepesi sana kuona wengine ndio wanahusika, anza kuona wewe umehusikaje, imekuaje ukawa katikati ya tatizo hilo. Kuwepo katikati ya tatizo ina maanisha kuna mahali wewe ulikosea hadi ukafika hapo. Ukisalitiwa inamaanisha kuna mahali ulikosea ukajikuta uko kwenye kusalitiwa, ndio unaweza kuona wewe huna kosa kabisa lakini ukikaa chini ukafanya tathimini utajikuta unaona sehemu ambayo ulikosea.

Huenda ulimuamini sana mtu huyo.

Huenda uliingia kwenye mahusiano bila kumjua vizuri.

Huenda kuna tabia mbalimbali unazo zinakera na hutaki kuzibadilisha.

Yote hayo yanaweza kuwa sababu za wewe kujikuta kwenye kusalitiwa na nyingine nyingi. Hivyo usiishie tu kujiona wewe uko sahihi bali kujitafakari na kuhakikisha unajirekebisha kwa upande wako. Kumbuka mtu pekee ambaye unaweza kumbadilisha ni wewe.

Baada ya kujua ni wapi ulikosea wewe mwenyewe, jisamehe usiendelee kuona wewe ni dhaifu, au unadanganyika kirahisi, mwepesi kuamini watu. Jisamehe na uanze upya na nguvu mpya katika kushinda yale ambayo ni udhaifu wako.

Sasa baada ya kusalitiwa au kuachwa kuna tabia nimekuwa naziona watu wengi wanazo na zinaweza kuwa chanzo cha wao kushindwa kuwa tena kwenye mahusiano mapya na kudumu. Hizo tabia nitazielezea kidogo kwa kadiri nilivyojifunza ila wewe binafsi utaona ni kwa namna gani zimekuwa kikwazo kwako mwenyewe na ujirekebishe.

Kuwa Mwepesi wa Kuona na kuhukumu Makosa ya Mwingine Haraka.

Mtu mmoja aliwahi kuniambia kwamba tangu aachwe hataki kabisa mtu wa kumuumiza kichwa hivyo akiwa kwenye mahusiano akaona hueleweki kidogo tu labda hupokei simu kwa wakati au chochote kinachomfanya aanze kuwaza basi anakuacha. Nilisikitika sana kwasababu huu ni kama ugonjwa kwake na amekuwa hadumu kwenye mahusiano hata mwezi mmoja unaweza kuisha amekuwa na wanaume wawili hadi watatu.

Hii ni hatari kwasababu hutaweza kumvumilia mtu, hakuna mtu ataekuja akiwa kamili kwako na asiwe na udhaifu hata kidogo.

Hapa kwenye kuona makossa sio shida, tatizo kubwa lipo kwenye kufikia hadi hitimisho. Mtu hajapokea simu zako kwasababu alikuwa bize na kazi au kwenye daladala basi wewe unafikia hitimisho la kuachana nae kwasababu hutaki usumbufu. Unajikuta unawapoteza watu wazuri kwasababu ya kukosa uvumilivu na kutosikiliza upande wa mwenzako.

Pamoja na kudanganywa sana na wengine hupaswi kuona wengine wote ni waongo, lazima ujifunze kuvumilia na kuamini wengine. Sio mtu anajieleza kwako unaanza kuona hawa ni walewale tu.

Kutaka Kumuumiza Aliemuacha.

“Nataka na yeye aumie kama alivyoniumiza” huwezi kupata faida yeyote kama na wewe una mawazo au mpango kama huu. Endelea na Maisha yako, amekuumiza lakini amekupa funzo kubwa sana. Kupoteza nguvu zako kutaka kumuumiza ni kujiumiza wewe mwenyewe.

Unakuta mtu anakwenda kutafuta mwanaume anaenda kutafuta mwanamke mrembo sana kuliko yule aliemsaliti au mwanamke anaenda kutafuta mwanaume mwenye vitu vilivyozidi yule aliemuacha. Ukweli unaweza kufikiri unamuumiza kumbe wewe ndie unaumia kwa kukosa kile unachokitaka na kwenda kuwa na mtu kwa ajili ya kumuumiza mwingine.

Samehe na endelea na Maisha yako.

Kufikiri Watu Wote Wako Sawa.

Haijawahi kutokea na haiwezekani watu wote wakawa sawa, bado kuna mengi tunatofautiana sana. Kuna baadhi ya tabia zinafanana lakini haiwezekani ikawa ni kwa watu wote. Muhimu ni wewe kujifunza kuendelea kuwa mvumilivu na kutenga muda wako kumjua mtu vizuri. Usimpojua mtu vizuri utaishia na majibu yako rahisi kwamba watu wote wako sawa.

Tenga muda wako umjue vizuri yule unaetaka kuwa nae kwasababu hapo ndipo unaweza kumtofautisha na wengine. Ukiishia kujua zile tabia za juu juu tu utabaki unasema watu wote wanafanana. Kila mmoja ana kitu cha pekee ndani yake ambacho mwingine hana ukiweza kukigundua hicho lazima uweze kumfurahia mtu.

Hitimisho:

Nataka ujiulize unataka kuwa kwenye mahusiano kwa kusudio gani? Je ni ili uoe/uolewe? Je ni ili uwe na Watoto? Je ni kwasababu umechoka kuwa peke yako?  Ni kwasababu ya Upweke? Je ni kwasababu ipo tangu zamani? Je ni kwasababu unaogopa kutenda dhambi ya uzinzi?

Ukiingia kwenye mahusiano kwa kukosa sababu nzuri utajikuta unateseka Maisha yako yote. Kikubwa ni wewe kulijua kusudi lako na uhakikishe yule unaetaka kuwa nae au ulieko nae anaweza kuwa pamoja na wewe katika kulitimiza kusudi la Mungu ndani yako. Kila mmoja awe ni msaada kwa mwenzake katika kulitimiza kusudi la Mungu.

Muombe Mungu akuongeze katika kufanya maamuzi kwasababu hayo ni Maisha yako, na Kama Mungu ni baba yako mpe kazi ya kukuongoza. Akikuongoza huwezi kukosea utampata yule alie wako.

Nakutakia Kila la Kheri;

Rafiki Yako Jacob Mushi

#usiishienjiani.

www.jacobmushi.com/coach

2 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading