Habari za Leo Rafiki, Mwanamafanikio na mpambanaji mwenzangu.  Ni matumaini yangu kwamba unaendelea vyema na safari ya mafanikio. Katika safari hii kujifunza ni kitu cha muhimu sana. Jifunze katika vitu mbalimbali vinavyokuzunguka. Leo tunatazama juu ya mambo 10 yanayotufanya waafrika tubaki nyuma siku zote.
1. Ubinafsi
Ubinafsi ni tabia mbaya sana inayofanya uishi maisha yenye majuto na yasiyo na furaha. Kitendo cha mtu kufanya mambo kwa ajili yake mwenyewe. Kutaka kupata faida zaidi bila kujali umetoa nini.
Ukitaka kufanikiwa acha ubinafsi, jali wengine, jitoe kwa ajili ya wengine. Chochote kile unachokitaka utakipata kama utajitoa kwa ajili ya wengine bila ya kujiangalia wewe unapata nini kwanza.
2. Uchoyo
Hii pia ni tabia ambayo haitofautiani sana na Ubinafsi. Tunaweza kusema mtu mchoyo ni asiyependa kutoa kwa wengine kile alichonacho. Una Maarifa mengi kichwani mwako lakini hutaki wengine wajue kwasababu watafanikiwa zaidi yako. Unataka wewe ndio uonekane uko juu siku zote hutaki kuwapa wengine nafasi. Mungu alipokuumba amekupa vitu vingi ndani yako uchoyo ni wewe kuishi bila ya kuvitumia na huku ukisema ipo siku nitakufa na kuviacha.
Ukitaka kuishi kwa furaha na uache alama basi tabia hii isiwe yako.  Wape wengine nafasi ya kuonekana, toa ulichonacho wengine wanufaike.
3. Kujikweza
Kujiona wewe ni bora kuliko wengine. Kujiona wewe unastahili kuliko wengine. Kujihesabia haki. Pale unapowashusha wengine chini ili wewe uonekane juu. Pale unapotamani Maisha ya wengine yawe mabaya ili wewe uonekane umefanya vizuri. Kama ukisikia mwenzako amefanikiwa kwenye jambo Fulani moyo wako unasononeka basi una tabia ya kujikweza. Unatamani wewe pekee ndio ufanikiwe.  Tabia hii inaturudisha nyuma sana ndio maana hatufanikiwi na tunabaki nyuma.
4. Kudharau walioko chini yako
Hii inatokana na wengi kusahau kwamba pale walipofika sio kwa juhudi zao wenyewe bali ni kwa wengine wengi. Mafanikio yeyote unayopata sio kwa nguvu zako mwenyewe tu Kuna wengi wamechangia. Wengine walikuombea na hujui.
Hata siku moja usiwadharau ambao hawajafika hapo ulipo. Ipo siku utaondoka na watakuja wengine. Jifunze kufanya mambo ambayo yataacha alama Kwenye mioyo ya watu kwa kila hatua tunayopiga.
5. Kuwaona wengine hawawezi.
Ili tuweze kupata mafanikio zaidi ni pale tu tutakapo wawezesha wengine. Tumia muda mwingi kuwatia moyo wengine na sio kuwaonyesha ni jinsi gani hawawezi. Usipende kuona madhaifu ya wengine na kuyatumia kuwaridisha nyuma ona nguvu yao iko wapi na uwatie moyo.  Hata kama hawawezi jaribu kuwatia moyo walioko chini.
6. Kuangalia maslahi zaidi kabla ya kusaidiana
Mara nyingi nimekutana na wengi hasa katika biashara wengi hawawezi kukusaidia bila kufahamu atapata faida gani.
Kama unafika sehemu huwezi kutoa msaada kwa mtu hadi uone ni maslahi gani unapata ujue ni ngumu sana kufanikiwa. Unajua vyote unavyovitafuta sio kwa ajili yako ni kwa ajili ya wengine.
Hawa ni baadhi ya wachache wanaoonyesha namna Ubinafsi na Kuangalia maslahi unavyotutesa waafrika.
Wasaidie wengine bila kujali unapata faida gani.  Kuna watu wako ndugu zako, watoto wako au wadogo zako wanasaidiwa huko na huko na watu wasiowajua.
7. Chuki za wenyewe kwa wenyewe.
Hapa ni pale mtu anapokuchukia kwasababu tu Umefanikiwa kuliko yeye. Umepandishwa cheo basi wengine hawazungumzi na wewe. Umenunua gari basi watu waanza kukuchukia.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe Africa vinasababishwa na watu kutaka kuwepo juu siku zote.
Maendeleo yatakuja pale tutakapokua na upendo.
8. Kumsifia mzungu lakini hujawahi kumpongeza Jirani yako aliefanya vizuri.
Mtu yupo tayari kusifia vitu vya kigeni sana kuliko anavyojali na kusifia vya kwake. Mtu wa kwenu akifanya jambo mnamcheka na kuona hawezi na haitakaa itokee. Lakini akifanya mzungu anaonekana amefanya vizuri sana.
Ili tuendelee tutumie muda mwingi kuangalia ni namna gani tunaweza kuwasaidia watu wetu wanaojaribu badala ya kuwaona ni wanaiga kwa wazungu. Tutumie muda mwingi kuwatia moyo hakuna aliewahi kuanza akiwa anajua kila kitu.
Tukitaka kuendelea tusichukie vya wazungu bali tujikubali pia na sisi. Tuna wengi mno wanaoweza kubuni na kuvumbua vitu.
9. Kulipiza visasi.
Tabia hii inaturudisha nyuma sana. Kutokusameheana ndio kunasabisha tukose maendeleo.
Kama Kuna binadamu mwenzako hadi sasa umesema hutakaa umsamehe, lazima umlipize kwa yale aliokufanyia ujue unajizuia kuendelea mbele. Mungu hawezi kukubariki kwasababu anajua utakuja kutumia baraka hizo kuumiza wengine.
Anza leo ubadilike na uwasamehe wengine. Achana na visasi havina nafasi katika maendeleo.
10. Kutaka kupokea zaidi kuliko kutoa.
Kabla hatujaomba misaada basi tuanze kujifunza kutoa. Hao wanaotusaidia siku zote wao hua wanatoa wapi?  Maendeleo yetu hayataletwa na mtu mwingine yeyote zaidi yetu wenyewe. Chochote tunachokitaka tunatakiwa tuweze kujitafutia wenyewe.
Tujifunze kutoa zaidi ya tunavyotaka kupokea. Hata kama wewe ni maskini kiasi huwezi kukosa cha kutoa.
Kwa leo nitaishia hapa tutaendelea kesho na mengine kumi yaliyobakia.
Karibu sana.
#USIISHIE_NJIANI
Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading