Katika safari ya mafanikio unapoamua kujikana na kusema ni lazima ndoto yako itimie kuna mambo mengi utapitia kwenye Maisha. Zipo aina ya changamoto ambazo hujirudia kama tu ndoto zako ni kubwa na umeamua kufika mbali. Kama umeamua kuwa tofauti na wengine kuna mambo ambayo ni lazima yakutokee tu haijalishi hao watu ni aina gani.

Ni muhimu ukayafahamu ili unapoona yanatokea usiyachukulie kwa uzito sana kiasi cha kukufanya ubadili maamuzi yako tena. Kuna watu baada ya kupingwa, kukosolewa au kupata washauri wengi wamejikuta wanaacha kile walichoamua kufanya na kujikuta wakirudia kule walipokuwa mwanzo au kupoteza mwelekeo wa ndoto na maono yao.

Kukataliwa/Kupingwa/Kukosolewa

Ukweli wa wazi ni kwamba kama umeamua kuwaza Zaidi ya wengine wanavyowaza, kuweka maono makubwa sana kuliko wengine utakataliwa, utapingwa na wakati mwingine kukosolewa sana. Unapoanza mwanzoni kabisa utakutana na watu wengi ambao ukiwaeleza unachotaka kufanya watakwambia haiwezekani. Watakwambia hilo unalowaza halijawahi kutokea hapa duniani.

Utakutana na watu watakwambia ndoto unazoota ni za mchana. Watu hawa wanaweza kuwa marafiki zako au ndugu zako wa karibu sana. Ninachotaka ufahamu ni kwamba yeyote ambaye amezaliwa ili aje kufanya mambo makubwa hapa duniani hajawahi kukubalika kirahisi.

Ukianza kuchukua hatua watatokea wengi wakupinge na kukwambia umechanganyikiwa. Kuna watu watadiriki kabisa kukuzuia na kukuwekea vikwazo. Nikutie moyo kwamba wala usiogope wewe sio wa kwanza kupitia hayo magumu. Songa mbele na usimamie kile unachokiamini na kukifanya.

Kuna mahala matokeo yakianza kuonekana watu wataanza kukukosoa na kutoa maoni mengi sana jinsi ambavyo ingepaswa kuwa kile unachokifanya. Sio vibaya unaweza kuwasikiliza na kuchuja kile kinachofaa unabaki nacho kile kisichofaa unakitupa.

Kujaribiwa

Kama umeamua kufika mbali kubali kujaribiwa kwenye sehemu mbalimbali za Maisha yako. Kuna majaribu utaletewa na watu ambao hukutarajia kabisa. Majaribu haya lengo lake kuu ni kukukwamisha kwenye safari ya mafanikio yako.

Kuna mitego itakuja na ukinasa basi unakuwa umepotea. Sio kila anaekuja kwako anacheka na kukusifia ana nia njema na wewe. Wengine wamekuja wanataka kukuzuia ila wanakuja kwa uso wa kirafiki.

Ukiweza kushinda mitihani hii ya kujaribiwa unapanda viwango vya  juu Zaidi. Kama una maono makubwa na ndoto kubwa za Maisha yako tarajia kujaribiwa na kuwa makini ujue jaribu ni lipi hasa ili uweze kulishinda.

Washauri Wengi

Watajitokeza watu wa kila aina pale ambapo umeanza kuchanua na kuonekana. Wengine walikuwa wanakupinga wakati unaanza watajitokeza sana kwa wingi. Usiogope nataka ujifunze kwamba hiyo ni kawaida mtoto anapozaliwa.

Wapo watakuja na ushauri wa kila aina. Watakwambia kwanini usifanye hivi, au hivi. Wengine ni watu wa karibu sana kwako hivyo ukishindwa kuwasikiliza mtagombana.

Unapaswa kujua kwamba sio kila mtu anaweza kukushauri na ukafanyia kazi ushauri wa kila mtu. Wengine watakuja kukupoteza kwasababu hakuna anaeona kama wewe unavyoona. Sio kila unachoambiwa ni fursa ya kutoka unaifuata bila ya kutumia akilia nyingine ni mashimo ambayo yatakuwa sababu ya wewe kutumbukia.

Chagua vyema watu wa kukushauri na chuja vyema ushauri unaopokea. Sio kila mtu anaona kama wewe unavyoona.

Kusemwa Vibaya.

Kuna nyakati zitafika utaanza kuona mambo mabaya kuhusu wewe yanazuka kila kona ya kweli na yasiyo kweli. Usishangae wala kupaniki hii ni kawaida ukishaanza kuwa juu kila mtu anakuona. Kama kila mtu anakuona kila mmoja atazungumza kile anachokiona.

Kuna ambao ni bora sana katika kutafuta mabaya kwenye vitu na Maisha ya watu. Hivyo utashangaa unasemwa kwa mabaya kila kona. Ukivaa watasema hujapendeza, ukiwa na mpenzi wako wapo watakaosema hata hamuendani.

Usishangae wala kuchanganyikiwa unapokutana na mambo kama haya. Wakati mwingine utazushiwa mambo ambayo hujawahi kuyafanya kabisa. Ukikosa hekima unaweza kuacha kila kitu na kurudi nyuma.

Ninachotaka ufahamu ni kwamba wewe uko juu. Ukiwa juu kila mtu anakuona na ataamua kusema kila anachokiona. Kuna watu wanatazama viatu vyako wataona vumbi hivyo watazungumzia vumbi waliloona.

Yale yanayosemwa kama ni kweli yabadilishe. Kama ni uongo tabasamu kisha songa mbele.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi,

7 Responses

Leave a Reply to Paulina SilasCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading