Habari Rafiki, leo tena tunakutana kwenye Makala yetu ya MBINU ZA MAFANIKIO. Tunaangalia mambo ambayo yamekuwa ni sababu ya watu wengi kukwama kimaisha. Ninaposema kukwama namaanisha vile mtu anakuwa kwenye hali moja kwa muda mrefu.
Pata Kitabu: SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO
Kama ni kazi anafanya basi anakuwa hana mabadiliko yeyote ya nje au hata ya ndani. Kama kuna mambo alikuwa anafanya yanakuwa hayaendi yako vile vile. Kama ni biashara basi biashara inakuwa haikui iko pale pale yaani imedumaa.
Inawezekana kabisa na wewe kuna sehemu ambayo umekwama, zipo sababu chache kati ya nyingi nimekuwa naziona zinajitokeza kwa watu ambao nazungumza nao. Jifunze nami ili uendelee kukua usikwame wala kudumaa.
- Kukosa Maono Makubwa.
Kukosa maono makubwa ndio sababu ya kwanza kabisa kwenye Maisha ya watu kukwama. Watu wengi wanataka vitu kwenye Maisha yao lakini ni vidogo sana kiasi kwamba hawaweki hata juhudi yeyote kuvipata. Yaani vitu ambavyo wanaviona wana uwezo wa kuvipata hata kama hawataweka nguvu kubwa sana.
Kama unataka kufika mbali basi ona mbali, tengeneza picha kubwa ambayo itakusukuma wewe kupambana hadi itimie. Acha kuogopa kuwa jasiri na kile unachokionamktakwenda kutimia. Hakuna mafanikio yaliyowahi kuja yenyewe. Unapoweka maono madogo unakuwa mvivu kwasababu yenyewe hayakuhamasishi hata kidogo.
Pata Kitabu: Usiishie Njiani, Timiza Ndoto Yako
Unapokutana na changamoto unaweza kuzikimbia kwasababu hujaweka maono yeyote makubwa kwenye Maisha yako. Andika maono makubwa kwenye Mahusiano yako, Afya Yako, Kazi/Biashara na Fedha. Andika kwenye kitabu chako cha maono na anza kuyafanyia kazi kidogo kidogo hadi yatimie.
- Kutokufanyia Kazi Maono Yao.
Ni kweli unaweza kuwa na maono makubwa lakini unafika mahali unakuwa hufanyi chochote kwenye ile picha yako kubwa uliyonayo. Usiishie kuhamasika na maono yako halafu ukakaa tu bila kufanya chochote. Kama unataka kuwa Mjasiriamali mkubwa hapa Africa basi anza na kitu kimoja leo, kikuze hadi kifike mahali hata mkoani kwako wakijue.
Kutokufanyia kazi maono kunaweza kuletwa na pale mtu anapokuwa anafanya jambo jingine ambalo halihusiani na maono yake. Mfano wewe una maono ya kuwa mfanyabiashara mkubwa halafu bado umeajiriwa. Unaweza kujikuta kila siku unasema nitaanza nitaanza hadi miaka inakatika bado upo pale pale. Sasa ndugu yangu nitaanza haijawahi kukusaidia, tafuta kitu cha kufanya taratibu uanze kuona matunda yake.
- Kutaka Kufanya Kila Kitu.
Huwezi kuwa kila kitu, huwezi kufanya kila kitu. Chagua vitu vichache ambavyo utavifanya hadi vikutambulishe. Mfano mimi binafsi nimeamua kuwa Mwandishi, Mjasiriamali na Mwigizaji. Hivi ninaweza kuvifanya na kila kimoja kina wakati wake wa kuanza kufanyiwa kazi. Kwa sasa unanijua kama Mwandishi na Mjasiriamali lakini miaka michache ijayo utaanza kuzitazama na filamu nitakazoigiza.
Unakuta mtu yeye kila kitu kinachokuja anataka afanye, leo limemjia wazo Fulani anajikuta amehama na kukimbilia wazo jipya. Mwisho wa siku unakuta hafiki mahali popote. Sasa Rafiki embu niige hata mimi kidogo chagua kitu kimoja au viwili ambavyo utawekeza muda wako na nguvu zako zote hadi ufikie Hatua kubwa kwenye Maisha yako.
Usiwe mtu ambaye huelewi mwelekeo wako wa Maisha. Tengeneza picha halafu anza kuishi kwa kuifuata hiyo picha. Kila jambo linawezekana kinachokukwamisha ni kutaka kufanya kila kitu mwisho wa siku unajikuta nguvu zako zimepotea kwenye mambo ambayo ulikuwa unagusagusa kila wakati.
- Kuiga Wengine.
Hii tabia ni mbaya sana, umeona watu Fulani wamefanikiwa kwenye jambo ambalo hujawahi kufanya unataka na wewe uanze kufanya lazima utakwama. Wewe tafuta mtu mmoja au wawili ambao wamefanikiwa sana kwenye kile unachokifanya na ujifunze kwao. Usikubali kuwa nakala ya watu wengine. Tumia muda mwingi kujitengeneza miaka michache ijayo watu wataanza kujifunza kutoka kwako. Ulizaliwa wewe mwenyewe na una kila nafasi ya kufanikiwa kwenye dunia hii.
- Kuishi Maisha Ya Maigizo.
Kamwe usije ukafanya kosa hili yaani kuigiza Maisha, kuwadanganya watu una Maisha Fulani mazuri kumbe ni uongo. Unajua unajidanganya mwenyewe, unajitesa mwenyewe, kuwa wewe ishi Maisha yako vile ulivyo.
Utakuwa unapoteza muda kama utaendelea na Maisha ya maigizo. Kuna mahali utashindwa kuingia kwasababu unaigiza Maisha. Tengeneza aina ya Maisha ambayo inakupa furaha na uiishi uswe mtumwa wa kuiga.
Umeanza biashara juzi tu lakini leo unataka uishi Maisha kama ya mtu ambaye alikuwa kwenye biashara miaka kumi iliyopita, lazima utafeli. Amini na fuata mchakato, mchakato ndio utakupeleka kule unakotaka kufika. Kabla hujawa bosi kubali kuwa mfanyakazi wako kwanza.
Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi
#UsiishieNjiani