Kama kijana una nafasi kubwa sana ya kufanikiwa endapo utakuwa umejitambua mapema. Kutokana na namna jamii zetu zilizvyotulelea inakuwa ngumu sana mtu kutambua yeye ni nani. Lakini kwa kipindi hiki tunajitahidi kwa namna mbalimbali ili vijana wengi waweze kujitambua na kuleta mabadiliko kwenye Maisha yao na kwenye jamii nzima.

Jamii yenye vijana wanaojielewa ni mara chache sana inaweza kuwa na maovi na uhalifu wa mara kwa mara. Jukumu langu na lako wewe ambaye tayari umeshajitambua ni kuhakikisha kila unaemfahamu anapata maarifa ambayo yanaweza kumsaidia akafanikiwa kimaisha. Tunapozungumzia mafanikio sio upande wa fedha pekee bali ni Maisha kwa ujumla. Mtu aweze kuishi Maisha bora, kuanzia kwenye afya yake, mahusiano yake, fedha na mali kwa ujumla.

Jua Kusudi Lako

Jambo la muhimu sana ambalo unaweza kuona linarudiwa mara kwa mara lakini ni kwa ajili ya kuonyesha umuhimu wake. Mtu anapogundua kusudi lake anakuwa amepiga hatua kubwa sana kwenye maisha yake. Ni muhimu sana kwa kijana yeyote atambua mapema sana kwanini yeye yupo duniani. Aliumbwa aje atimize nini.

Kaa Karibu Sana Na Mungu.

Mungu ndie anaweza kuwa msaada mzuri kwenye Maisha yako ya ujana. Kaa karibu na Mungu wako. Mwombe Mungu, soma neno, nenda kwenye ibada. Ubora wa Maisha yako hapa duniani ni vile ulivyoweza kuishi na vyema na Mungu wako. Biblia inasema Mkumbuke Muumba wako Siku za Ujana wako. Wakati wa ujana ndio wakati wa kujitoa kwa Mungu, kufanya kile alichokuumbia kufanya.

Beba Majukumu Ya Maisha Yako Mapema

Ni muhimu kwa kijana atoke kwenye Maisha ya kulelewa na kwenda kujitegemea. Maana yake awe ameweza kujilisha, kujivalisha na ikiwezekana awe na mahali pa kuishi mwenyewe. Hii inaweza kuwa njia nzuri ya kujua unapoelekea na unachokitaka kwenye Maisha yako. Unapobeba majukumu ya Maisha yako unakosa mtu wa kumtupia lawama, na badala yake unakuwa mtu wa kuchukua hatua.

Chukua Maamuzi Magumu Na Mapema

Kuna maamuzi unatakiwa uweze kuyafanya mapema ukiwa kijana kwasababu umri unavyozidi kukimbia ndipo na ugumu wa kufanya maamuzi unaongezeka. Mfano unataka kuamua ni mahali gani unataka kuishi Maisha yako ni rahisi sana ukiamua ukiwa kijana na ukaenda kuishi kuliko ukiwa tayari una mke/mume na watoto. Kuhama na familia inaweza kuwa mzigo mkubwa Zaidi pia unaweza kukuta una watoto wanaosoma shule hivyo ukashindwa kufanya maamuzi.

Yapo mambo mengi sana unapaswa kuyafanyia maamuzi mapema kabla ya wakati haujasonga.

Amua Kuishi Ndoto Yako.

Ni muhimu uwe una kitu ambacho una kitumainia mbeleni, hiki ni ndoto zako kubwa. Ukiwa mtu mwenye ndoto na unazifanyia kazi basi utafurahia ujana wako. Maisha yako ni lazima uyatengeneze ukiwa kijana. Tengeneza ndoto kubwa za Maisha yako na anza kuzifanyia kazi ukiwa kijana.

Fanya Kile Unachokipenda

Fanya kile unachokipenda bila kujali watu wanasema nini. Ukweli ni kwamba hakuna anaejali sana juu ya Maisha yako kama unavyofikiri. Ninaposema fanya unachokipenda namaanisha ufanye vitu sahihi na sio starehe na anasa za dunia hii. Ukipotelea kwenye starehe na anasa ujana wako utapotea kama maua yanyaukayo wakati wa jua.

Tengeza Afya Yako Soma Sana/Lisha Akili Yako Maarifa

Ili uwe mzee mwenye busara na hekima inategemea ujana wako uliishi vipi. Unaweza kuwa na ujana mbaya lakini ukakupa somo zuri ambalo unaweza kuja kuwaambia wajukuu zako wasipite njia gani na wapiti njia gani. Lakini uzee wako utakuwa bora Zaidi kama ujana wako utautumia kujifunza vitu vingi. Jaza maarifa kwenye akili yako yatakusaidia sana siku za mbeleni.

Tengeneza Mahusiano Mazuri

Tengeneza mahusiano mazuri kwa wale unaowapenda, na jamii inayokuzunguka. Ili uweze kufurahia vitu hapa duniani ni lazima uwe na mahusiano mazuri na watu. Kama watu wanakuona kama adui huwezi kuishi kwa Amani.

Ili watu wafurahie kazi zako na kile unachokifanya ni muhimu uwe na mahusiano nao mazuri. Ili uweze kutengeneza jina lako zuri hapa duniani lazima uwe na mahusiano mazuri na wengine. Wapo watakao kuwa msaada kwako kwa ajili ya kuinuka.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

4 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading