Kuna utafiti ulifanyika wa kidunia ukaja na majibu ya nchi zinazoongoza kwa kukosa furaha duniani. Mojawapo ya nchi iliyotajwa ilikuwa ni nchi ya Tanzania, kwasababu mimi ni mtanzania sikuwa na majibu sahihi wala utafiti wa kupinga hili ila ninaweza kukuandikia wewe mambo machache ambayo unaweza kufanya na yakakuletea furaha binafsi.

Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba, furaha inaletwa na vitu au watu. Kumekuwa na dhana hii ambayo imejengeka katika fahamu za wengi kwamba mtu ukiwa na fedha au mali nyingi ndio unakuwa na furaha. Ukweli mara nyingi furaha zetu haziletwi na vitu vinavyoonekana kwa macho. Ile hali ya kufurahia vitu au yale mambo ambayo umefanikisha mara nyingi haidumu.

Ipo namna moja ambayo unaweza kuitumia na ukajitengenezea furaha yako mwenyewe na ukaishi Maisha marefu na yenye Amani. Utamu wa Maisha sio kuishi muda mrefu bali ni vile ulivyofurahia ule mdua ambao umeishi hapa duniani. Unapojua kusudi la wewe kuwepo hapa duniani na ukaanza kuliishi hicho ndio kiini cha furaha yako. Kama wewe ni mwimbaji kamwe huwezi kujisikia Amani ukiwa wodini kama daktari, utakuwa na hofu. Unapokuwa kwenye jukwaa ndio unajisikia furaha na Amani ya moyo.

Tafuta Utulivu mara kwa Mara (Peace of Mind)

Furaha inatoka ndani je wewe unapata muda wa kutulia na kusikiliza ndani yako? Unajua ni kitu gani hasa unataka? Watu wengi kwasababu hawana muda wa kukaa na kujisikiliza wao hujikuta kila wafanyalo linatokana na yale waliyoona kwa watu. Mwisho wa siku unajikuta mtu huna furaha kwa kila ulichonacho na kwa kila unachofanya.

Ukiwa na tabia ya kutafuta utulivu na wewe mwenyewe utagundua ni nini moyo wako unahitaji ili uweze kuwa na furaha. Mara nyingine inawezekana ni kwa kusikiliza mziki tu ndio unapata faraja sasa wewe unakwenda kunywa pombe. Wakati mwingine inawezekana ukienda mbali sehemu ambayo haina watu wala kelele ndio raha yako sasa wewe unakwenda kushinda disko siku zote utakuwa mtu aliechanganyikiwa.

Fikiri Chanya Kwa Kila Hali Inayotokea.

Mambo mengi yanatokea kila siku unapaswa kujua kwamba kila jambo linasababu ya kutokea. Fikiri chanya tu, kuna nafasi yako kubwa inaandaliwa mbele. Usipoteze mud ahata kidogo kufikiri hasi kwasababu utakuwa unajiumiza moyo.

Furaha inakuwepo hata wakati unapitia matatizo endapo tu utaweza kuyaelewa mambo na kuyachukulia vile yalivyo. Limekupata jambo baya elewa kwamba wewe sio wa kwanza, hivyo ni kwa mipango ingeweza kutokea kwa mwingine lakini imetokea kwako.

Usiwe Mtumwa wa Kujilinganisha na Wengine.

Maisha yako ni yako, kujilinganisha na wengine ni kujitukana. Maisha uliyonayo wewe hayapaswi kulinganishwa na mtu kwasababu kila mtu ana upekee wake. Tafuta vile vitu ambavyo vinaleta Amani ya moyo vifanye.

Usipoteze muda wako kuwatazama wengine kuliko unavyojitazama. Jiulize mara kwa mara hivi ni namni anaenifuatilia? Ni nani anaetamani kuwa kama mimi endapo nitaendelea kutamani kuwa kama Fulani? Ukweli ni kwamba hakuna atakaepoteza muda wake kukufuatilia au kukuiga wewe ambaye unaiga Maisha ya wengine.

Tengeneza Maisha Rahisi.

Kitu ambacho watu wengi huchanganya ni hiki, wanapofikiria kuhusu furaha wanadhani labda ukiwa na Maisha ya starehe ndio furaha. Wengi wanaostarehe sio kwamba wana kitu cha tofauti sana kinachoitwa furaha hapana, tena wanaweza kuwa wanateseka sana kwenye zile starehe wanazofanya. Ukiona mtu analewa sana, anafanya anasa sana ukifuatilia Maisha yake unakuta ana msongo wa mawazo anafanya yale yote ili kujisahaulisha matatizo anayopitia.

Ni vizuri utengeneze aina ya Maisha ambayo wewe mwenyewe unayafurahia na sio ili uonekane na watu. Mmoja wa mabilionea wakubwa duniani Bwana Warren Buffet anaisha Maisha rahisi sana kama mtu wa kawaida wa hapa kwetu. Ukifuatilia matajiri wengi wanaishi Maisha ya kawaida sana. Kinachotufanya tunakosa furaha ni kwamba tunaishi Maisha ya kutaka sifa kwa watu na huku mioyo yetu ikiteseka kwa ndani.

Usinunue vitu kwasababu unaweza kununua hapana, nunua kwasababu unahitaji. Usifanye starehe kwasababu una muda wa kufanya starehe jiulize kuna umuhimu wowote wa kufanya hivyo? Pesa nyingi hupotea kwenye matumizi mengi yasiyo ya lazima kwenye Maisha ya watu. Unaweza kutengeneza Maisha marahisi sana na ukajikuta unaishi bila ya msongo wa mawazo. Tafuta pesa zifanyie mambo ya maana na sio starehe.

Usiwe Mlevi wa Mitandao ya Kijamii.

Ulev wa mitandao ya kijamii unawafanya wengi wanakosa furaha, kuna jarida moja lilitoa utafiti wake likasema kuwa watu wengi walioko kwenye mitandao ya kijamii hutumia muda mwingi kufuatilia Maisha ya watu. Yaani unakuta mtu yeye akiingia anaenda kumtafuta mtu aangalie ameweka picha gani, amefanya tukio gani.

Sasa kile kitendo cha kuwatazama wengine kila wakati unajikuta unajiona unaishi Maisha duni sana. Bahati mbaya ni kwamba hakuna anaeweka picha zenye kuonyesha Maisha mabaya. Kila anaeweka picha ataonyesha akiwa na furaha sana na akicheka, wewe kwasababu huku kwako umekula ugali dagaa ukioma mwenzako katupia picha ya kuku unaumia na kuanza kupoteza furaha yako.

Tenga muda maalumu wa kutumia mitandao hii labda tu uwe unafanya biashara. Mambo mengi unayotakiwa kufuatilia yawe ni ya kukujenga na kukufundisha.

Tafuta Rafiki Mmoja Unaemwamini Uwe Unazungumza Nae Yanayokusibu.

Kuna mambo mengi tunapitia kama kuumizwa kwenye mahusiano, ugumu wa Maisha na mengine mengi. Hakikisha wewe kama binadamu una Rafiki mmoja ambaye ni wa karibu kwako na mna aminiana. Mtu huyu ni yule ambaye unaweza kuwa wazi kwake hasa unapopitia mambo yanayoondoa furaha yako.

Mara nyingi watu wengi wanaofikia Hatua ya kujiua au kufanya ukatili wa aina mbalimbali wamekuwa wanakosa watu wa kuwaeleza yale wanayopitia. Usiishi kama mtu asiye na watu hapa duniani, ishi kwa furaha Maisha yako sio ya kuishi huku una maumivu.

Ishi Maisha ya Furaha.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

6 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading