Ulishawahi kutaka kukutana na mtu akakujibu kwamba hana muda? Umewahi kujiuliza ni kwanini anasema hana muda? Je kuna ukweli wowote pale anapokwambia hana muda?

Wanadamu wote tumepewa masaa 24 kila siku na hii ni mojawapo ya vitu ambavyo kila mmoja anacho kwa usawa kabisa. Kinachotutofautisha ni yale ambayo tunatumia kwenye muda wetu kila siku. Kuna ambaye anautumia muda wake vizuri kwenye yale mambo yaliyo ya muhimu kwake na kuna ambaye anatumia muda wake katika yale yasiyo ya muhimu.

Kuna msemo mmoja unasema usipojua kuutumia muda wako vizuri watakuja watu wanaojua kutumia muda vizuri na watakulipa uwauzie muda wako. Wakati mwingine wanaweza wasikulipe na wewe ukawapa bure muda wako kwasababu huna cha maana cha kufanya na muda wako.

Ukiona mtu anakwambia sina muda kabisa, nikipata muda nitakuambia. Ukweli ni kwamba muda anao, ila ana mambo mengine ya muhimu kuliko hilo ambalo unataka kufanya nae. Akikuambia ukweli kwamba hili unalotaka tufanye sasa sio la muhimu kwangu utaumia sana. Sasa ili kukupooza kidogo inabidi akwambie sina muda kabisa.

Ukweli ni huu hakuna asiye na muda ila tunatofautiana vipaumbele. Wakati wewe muda wako unautumia kutembelea mitandao ya kijamii kuna mwenzako anasoma kwa bidii. Wakati wewe muda wako unautumia kuangalia movie kuna mwenzako muda huo anautumia kwenye mambo ya muhimu Zaidi ya kumfanya awe bora kila siku.

Jiulize wewe binafsi umewahi kukosa muda wa kufanya mambo yasiyo na umuhimu? Au wewe kila anaekuhitaji huwa unatokea tu? Umewahi kusema hapana mara ngapi kwa mambo yasiyo na kipaumbele kwenye Maisha yako?

Ni rahisi kuona una muda mwingi sana wa kutosha lakini pale ambapo unakuwa na majukumu mengi ya Maisha ndipo wakati unaona huna muda hata kidogo. Ukifika wakati kila jambo linakuhitaji wewe na karibu yote ni ya muhimu ndipo utaanza kuona umuhimu wa kutumia muda wako vizuri.

Jifunze kutumia muda wako vizuri, jifunze kupangilia muda wako, kuwa na ratiba ya siku na ya wiki. Hakikisha unavijua vipaumbele vya Maisha yako. Hakikisha unafahamu ni wapi unakwenda na hapo ulipo sasa hivi ni wapi.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading