Mojawapo ya vitu vinavyowafanya watu waishi maisha ya magumu sana hapa duniani ni kukosa namna bora ya kupangilia na kuendesha maisha yao. Kingine ni kwamba wengi wanapenda kuishi maisha ya kuiga, kwasababu umeona jirani yako ana maisha Fulani hivi na wewe unataka uanze kuishi hivyo.

Sio vibaya kutamani vitu vizuri kwenye maisha yako lakini ni vyema ukatambua kwamba chochote kile unachokitaka kuna mchakato wa kukifikia. Kama utaruka mchakato umeona kitu leo na unakitaka le oleo utaishia kuwa na maisha magumu sana.

Lazima utambue pia kuna gharama za kulipa wakati unaelekea kwenye kile unachokitamani. Ukishindwa kulipa gharama hizo ukakimbilia njia fupi baadae maisha yako yatakuja kukulazimisha kulipa gharama zote ulizokwepa.

Watu wengi maisha yao yamegeuka kuwa madaraja ya pesa na kila wanchokifanya wamekuwa kama wanawafanyia wengine kazi. Kila pesa unayoipata inakuwa inapotelea kwenye matumizi na hakuna unachokifanya cha maana kwenye maisha yako.

Unajikuta hakuna maendelea yeyote pesa unayopata inaishia kwenye matumizi yako ya kila siku. Mwingine unapata pesa nyingi kabisa lakini hakuna cha maana ambacho kinatokea kwenye maisha yake kwasababu ya maisha ambayo anayaishi ya kuwaridhisha wengine. Maisha Fulani hivi ambayo watu wa nje wakikutazama wanasema una pesa kumbe ni mateso tupu.

Hali zote hizo zimesababishwa na watu ambao uliwaruhusu wachukue pesa zako mfukoni. Watu hawa uliowaruhusu maisha yao yanakuwa mazuri sana kwasababu umekuwa kama unawafanyia kazi.

MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA.

Kuna matumizi mengi sana ambayo kila mtu anaweza kuwa nayo lakini hayana ulazima wowote kwenye maisha yake. Nikiwa na maana kwamba endapo hutafanya au hutatumia hivyo vitu bado hakuna kitakachoharibika kwenye maisha yako.

Mfano unajua kabisa kipato chako sio kikubwa au hata kama ni kikubwa kuna mambo mengi ya muhimu unatakiwa uyatekeleze kwanza. Lakini umezoea kupanda taxi kila safari unayofanya hata kama kuna uwezekano wa kupanda daladala. Kwasababu umeshajijengea tabia hii utaona kurudi kwenye daladala ukatumia tsh 400 ukaokoa elfu 4000 nzima utakuwa umejishushia hadhi. Lakini ukweli ni kwamba kama utakuwa unapanda na huko uendako hakuna uharaka wa kupanda taxi ni bora tu ukaanza kupanda daladala. Ndani ya siku 30 utakuwa umeokoa tsh 120,000 ambayo ungeweza kuifanyia mambo mengine au kuweka akiba.

Kupanda taxi ni mfano nimetoa kuna mengi sana ambayo unaweza kuyatazama utaona kuna pesa zinapotea bila ya sababu na hakuna ulazima wa kufanya hivyo wakati bado kuna sehemu unataka kufika. Naamini kabisa kuna sehemu utafika utakuwa unatumia kila unachokitaka kwasababu tayari una uhuru wa kifedha. Kama hujafika kule unapokwenda usiishi kama tayari umeshafika.

HATUA ZA KUCHUKUA.

Kamwe usikubali kununua kitu kwasababu tu umekipenda bali nunua kwasababu unakihitaji. Ukiwa na tabia ya kununua vitu kwasababu umevipenda utajikuta umebeba mizigo mingi ambayo huna matumizi nayo nyumbani.

Jua matumizi yako ya kila siku, wiki, na hata mwezi mzima. Tengeneza bajeti na uifuate kila siku. Hakikisha bajeti yako hailingani na haizidi kipato chako. Matumizi yako yanatakiwa yawe chini ya kipato chako ili uweze kukua na kuongezeka. Hata kama unapata kipato kikubwa usikubali kutumia chote.

Hata kama unao uhakika wa 100% ya kuendelea kupata hicho unachokipata usiache kuweka akiba.

KUTAKA KUONEKANA.

Watu wengi wamekuwa watumwa wa hii tabia ya kutaka kuonekana kuwa wana maisha mazuri na wale watu ambao wamewazunguka. Inakuwa haina maana yeyote kama utaonekana una maisha mazuri lakini ndani yako unateseka.

Unatamani sana watu wajue una maisha Fulani badala ya kuigiza embu fanya kazi kwa bidii uyatengeneze yale maisha yawe kweli.

Unatakiwa utambue kwamba pesa yako ni ile unayobaki nayo uloweka kama akiba na sio ile unayokwenda kununulia vitu.

Huwezi kuhesabu vitu ulivyonunua ukasema ndio utajri ulionao kwasababu hata utajiri unapimwa kwa zile mali ambazo ulizonazo zinazokuzalishia. Kama wewe utakazana na mali ambazo zinakufanya uonekane ni tajiri utakuwa unapotea kabisa.

HATUA ZA KUCHUKUA.

Acha maigizo ishi maisha yako ya uhalisia. Vile unavyotaka watu wakuone anza kutengeneza sasa hivi ili miaka michache ijayo uweze kuishi hivyo.

Andika vile unavyotaka kuwa, unavyotaka kuonekana, unavyotaka kumiliki. Jua ni kipato kiasi gani utahitaji ili uweze kuishi maisha hayo bila ya wasiwasi wala msongo wa mawazo kwasababu ya kukosa pesa.

Anza kufanyia kazi kila siku kuongeza kipato chako kikue hadi kifikie kiwango hicho.

ZOEZI LA KUFANYA:

Siwezi kuandika kila kitu hapa kila mmoja anajijua yeye mwenyewe na maisha yake anayoishi. Sasa nikupe zoezi la kufanya.

Chukua kalamu yako na notebook yako uandike chini mambo yoote unayofanya kila siku na yanahitaji pesa.

Andika yale yanayotokea kama dharura na yale yanayojirudia mara kwa mara.

Katika mambo yoote hayo chambua mambo ya muhimu sana ambayo usipoyafanya maisha yako yatakuwa ya hovyo sana na unaweza kushindwa kuishi. Mfano hapa ni kula, lazima ule kila siku. Haya yape herufi A

Chambua mambo ambayo sio ya muhimu sana lakini ni ya lazima mfano kupanda daladala unapokwenda mjini. Usipopanda daladala huwezi kufa lakini ni lazima upande daladala ili uweze kufika mjini. Yape herufi B

Chambua mambo ambayo sio ya muhimu na wala sio ya lazima lakini huwa unayafanya tu kwasababu ulikuta wengine wanafanya. Mfano unarudi nyumbani kwasababu tu umechoka unapanda toyo ili uwahi kwenda kupumzika wakati ungeweza kupanda daladala tu na bado ungefika kwa wakati. Utatumia elfu tatu au elfu mbili kwa ajili tu unawahi kwenda kupumzika. Yape herufi C

Haya sasa ni wakati wako kuona kwamba hapo kwenye herufi C ukiacha kufanya hayo mambo ni pesa kiasi gani utaokoa na zitakwenda kufanya nini kwenye maisha yako. Watu wengi tumekuwa tunayapa vipaumbele mambo yaliyopo kwenye herufi C kuliko hata A. Mtu hajali afya yake lakini yupo tayari kufanya mambo mengine ambayo hayana umuhimu sana kwenye maisha yake.

Rafiki Yako Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

2 Responses

Leave a Reply to DorisCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading