HATUA YA 375: Na Hiki Pia Umeamua Wewe.

jacobmushi
By jacobmushi
2 Min Read

Unajua kwamba umeamua mwenyewe kufungua Makala hii na kuisoma? Hivyo basi Maisha ya kila siku ni mkusanyiko wa maamuzi ambayo unayafanya kila dakika na kila saa. Kila inapopita dakika kuna jambo umeliwaza na ukafanya maamuzi.

Unaamua kukaa kwenye mitandao ya kijamii masaa kadhaa ukipitia mambo ya ajabu ajabu. Ulianza kwa kukumbuka vitu vya jana ukasema ngoja nipitie mara moja.

Hata mimi nimekaa nikafikiri kisha nikafanya maamuzi ya kuandika Makala hii na sasa umeanza kuisoma pia. Kama ningefanya maamuzi mabovu basi ningepata matokeo mabovu, lakini hapa ni wewe unasoma na Maisha yako yanakwenda kuwa bora.

Kabla hujafanya maamuzi fikiria kwanza. Kwasababu usipofikiri utakwenda kufanya maamuzi ambayo yataathiri Maisha yako. Kama maamuzi yakiwa mabovu basi Maisha yako ndipo yataanza kuwa mabovu.

Chochote kinachoendelea kwenye Maisha yako kwa sasa una mchango Mkubwa sana wa kutokea kwake. Kiwe kibaya au kizuri una mchango Mkubwa sana. Na pia bado una nafasi ya kubadilisha endapo ulikosea kwenye kufanya maamuzi.

Ninachotaka upate hapa ni kwamba ili uweze kuwa na maamuzi bora lazima uanze kuwa na mawzo bora kwenye akili yako. Akili bora inapatikana kwa wewe kujiendeleza na kujifunza kila wakati. Akili yako ikiwa imejaa maarifa basi utaweza kufanya maamuzi bora kwa Maisha yako.

Tengeneza utaratibu wa kuijaza akili yako mambo ambayo yatakusaidia kwenye kufanya maamuzi. Kwenye familia yako, kazi yako, biashara yako, na Maisha kwa ujumla kuna vitu vingi unapaswa kuvijua ili uweze kufanya maamuzi ambayo yatakufanya uwe bora.

Unaamua kula chakula kibovu na unasababisha afya mbovu lakini ukiwa na maarifa kidogo juu ya afya lazima utafanya maamuzi bora wakati wa kuchagua chakula. Unakuwa na ndoa yenye mgogoro kwasababu umekosa maarifa ambayo yangekusaidia kuelewa ni namna gani ya kuishi vyema na mwenzako. Hivyo unajikuta kila maamuzi unayofanya yanasababisha mgogoro kila siku.

Badilisha fikra zako kwa kusoma Vitabu, Makala, sikiliza video nzuri ambazo zitakufanya upate uwezo mzuri wa kufanya maamuzi.

Maisha yako ni mkusanyiko wa maamuzi na Matendo madogo madogo ambayo unayafanya kila siku. Amua vyema upate Maisha mema.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading