Mahali ulipo sasa hivi na hayo unayopitia unaweza kuyaona ni magumu sana. Unaweza kufikia hatua ya kujutia hata kwanini ulizaliwa kwasababu unajiona kama wewe pekee ndie mwenye mateso na majaribu makubwa sana duniani.

Ukweli ni kwamba hayo unayopitia ni majaribu kweli ni magumu pia. Ila kwasababu hapo ndio sehemu uliyofika ndio maana unayaona kama ni magumu mno. Ukitaka kufahamu ukweli jaribu kupitia hadithi za Maisha ya wengine uone mambo makubwa na magumu wengine wanayopitia na hapo ndipo unaweza kuhisi kumbe hata yale unayopitia sio magumu sana.

Ninachotaka kukwambia hapa acha kulia, acha kulalamika inuka katafute suluhisho la hayo magumu yako kwasababu kuna wengine wanapitia mazito kuliko wewe halafu hawana hata hiyo nafasi ya kulalamika.

Kama mepata nafasi ya kuliongelea tatizo lako kwa wengine hiyo pia ni nafasi ya kipekee ambayo wengine wanaitafuta hawaipati. Kuna watu wanapitia magumu sana na hawana hata mtu wa kumueleza hivyo kama wewe umepata mtu ukamhadithia yale magumu yako hilo ni la kumshukuru Mungu.

Sio kwamba nayalinganisha mapito yako na ya wengine hapana, natamani tu uone kuwa kama bado upo hai na u mzima basi hilo ni jambo kubwa sana. Hiyo ni nafasi ya kujaribu tena, hiyo ni njia ya kurekebisha pale ulipokuwa unakosea.

Usikubali kukata tamaa kama bado upo hai, umepata nafasi basi itumie vyema. Usikubali kutumia muda mwingi kujitazama na kufikiria vile ulivyo na matatizo mengi kwani utakuwa unazuia uwezo wako wa kujua suluhisho. Ifanye akili yako ione uwezekano kwenye kila ugumu unaopitia, usikubali kuiambia akili yako kuwa wewe una matatizo makubwa sana, usiiambie akili yako wewe una mikosi, umelogwa huna bahati kwani utakuwa unaizuia isifanye kazi yake ya kutafuta suluhisho.

Usikubali kuzuia uwezo wako wa kufikiria suluhisho la matatizo yako kwasababu ya kulalamika na kujiona wewe ndio mwenye matatizo mengi. Siku zote kuwa mtu anaewaza namna ya kufanikiwa au kuvuka pale ulipokwama.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading