NGUVU MPYA 420; Unahitaji Vitu Hivi 3 Uwe na Maisha Yenye Furaha.

Maisha yanajengwa kwa misingi, Maisha mabovu yamejengwa kwenye msingi mbovu, Maisha bora yamejengwa kwenye msingi imara na bora. Ifahamu misingi ya Maisha unayoyataka na kisha uanze kuifanyia kazi kila siku.

Kuna matatizo yanaweza kuwa yanakuandama kwenye Maisha kwasababu tu hujaifahamu misingi na kanuni za Maisha. Na suluhisho ni kuzifahamu kanuni na misingi kisha uanze kuzifanyia kazi kwenye Maisha yako.

Kama mwanadamu unahitaji vitu vitatu vya muhimu kabisa ambavyo ndio msingi wako mkuu. Ukiweza kuvifanyia kazi hivi kamwe huwezi kukosa furaha au kuona Maisha hayana thamani kwako.

Kitu cha Kufanya.

Hapa unatakiwa uwe na kile kitu ambacho Mungu alikuleta duniani uje kufanya. Mfano wewe ni muimbaji basi hakikisha umejua wewe ni muimbaji na unaimba yaani unauishi uimbaji. Kama kile kipaji ambacho Mungu alikuwekea hujaanza kukifanyia kazi hata uwe unafanya kazi inayokulipa kwa kiasi gani bado utaona kuna kitu kimepungua Maishani mwako. Hakikisha unaweza kukifanya kiwe kinatengeneza pesa.

Mtu wa Kumpenda.

Ukishaanza kufanya kitu lazima uwe na mtu unaempenda. Hapa nazungumzia masuala ya mahusiano. Kama wewe ni mwanaume basi uwe na mwanamke umpendaye na kinyume chake pia. Bila kuwa na mtu umpendaye siku zote utayaona Maisha ni magumu na yamepungua. Hata ufanye kazi kwa bidii sana bado kuna nyakati zitafika utajihisi umepungukiwa.

Kitu Unachokitumainia.

Hii ni lazima kwa mtu uwe na kitu unachokitumainia kwenye Maisha yako. Hapa tunazungumzia maono makubwa ndoto kubwa za kile ambacho unakifanyia kazi na nyingine katika masiha yako. Tengeneza maono makubwa kwenye ile kazi yako unayoifanya. Tengeneza maono makubwa juu ya Maisha yako ya mahusiano na wale wote uwapendao.

Unapokuwa unafanya kazi halafu kuna mtu unampenda sana halafu kuna mambo unayategemea kwamba yatatokea na tayari unayafanyia kazi lazima uwe mtu mwenye furaha. Sasa Rafiki acha kusema mimi sitakaa nipende tena, mimi nimeumizwa nimeamua kuwa mwenyewe. Mimi tayari nimeshakuwa na mtoto sitaki tena usumbufu nitalelea mwanangu. Unajinyima vitu vya muhimu sana kwenye Maisha ya mwanadamu.

Nimewaona wengi wanasema nawachukia wanaume halafu baada ya muda unakuja kusikia ameolewa. Kuna wengine wanasema wanawake hawaaminiki ni kweli lakini yupo wako ambaye anaaminika huhitaji kuwaamini wanawake wote yupo wa kwako. Kwa hiyo Maisha yako ili yakamilike unamhitaji mwenzako, unayahitaji maono makubwa na pia kitu cha kufanya.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading