Katika Maisha mwanadamu anapitia mambo mbalimbali sana, kuna mengi mtu unakuwa umeyafanya mengine ni ya aibu sana. Kikawaida mambo haya yanaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa wewe kusonga mbele kwasababu yanakuwa kama yanakurudisha nyuma.

Unaogopa watu watajua wewe ulishatoa mimba ndio maana unashindwa kufanya mambo makubwa. Unaogopa watu watajua kuwa ulibakwa ulipokuwa mdogo na ndio maana mpaka sasa hujachukua hatua yeyote kwenye ile ndoto kubwa uliyonayo.

Unaogopa watu watasema wewe umeshatembea na wanawake wengi sana hivyo unadhani ukifikia mafanikio makubwa basi watu watajua na utaaibika.

Labda ulishawahi kuiba au kutelekeza Watoto, ulishawahi kuumiza wengine, ulishawahi kufanya vitendo vya aina mbalimbali ambavyo ukifikiria unajiona wewe hustahili kuwa mtu Fulani.

Naomba nikwambie Rafiki amua kuachilia mizigo hiyo. Hayo ni Maisha yako yaliyopita cha muhimu ni wewe tayari umeshabadilika. Jitie nguvu usione aibu kwasababu hakuna aliekamilika.

Usikubali aibu hii iendelee kukuzuia kutimiza ndoto zako. Usikubali aibu hizo ziwe sababu ya wewe kukata tamaa na kuona kwamba haiwezekani tena. Wewe sasa ni mtu mpya tua mizigo yako.

Yakubali kwamba yale yalikuwa ni Maisha yako ya zamani na uwe tayari kujibu bila woga kwamba huogopi kuwashauri wengine wasiwe na Maisha kama yale ya zamani. Yakubali kabisa na wala usikatae kwasababu hata ukikataa wanaofahamu watasema cha muhimu wewe ni kuwa jasiri sana na lile ambalo ungetaka lijulikane wala usisite tu kulisema na ikiwezekana kwamba yamesemwa na kuna ulazima wa kujibu jibu lako liwe yale ni Maisha yangu ya zamani ambayo kila mtu anaweza kuwa nayo.

Haimaanishi wewe ni yale makosa yako, kila mmoja ana historia ambayo hangependa ijulikane mbele za watu hivyo hata wewe usijione labda uliyoyafanya yanakutenganisha na binadamu wengine. Kila mmoja ana aina ya Maisha ambayo alishawahi kuyaishi na yanaweza kuwa ya aibu cha muhimu ni wewe kuwa umeyaacha.

Naamini Rafiki hutakubali tena aibu hii kuwa sababu ya wewe kuogopa. Usione ni kitu cha ajabu wewe ni kama wanadamu wengine, usijione hufai, usijione ulifanya mambo maovu sana, usijione hustahili tena kufanya makubwa. Anza sasa kusonga mbele, unastahili makubwa mno.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading