Watu wamekuwa ni mashujaa sana wa kueneza habari mbaya kuhusu wengine, imekuwa ni desturi yetu pia kutoa vipaumbele Zaidi kwenye habari mbaya kuliko njema. Wafuatiliaji wa habari na watoaji wa habari wote wamekuwa wakipendelea Zaidi habari mbaya.
Kwenye Maisha yako kama unataka kufanya jambo lenye kuacha alama basi chagua kusema kile ambacho kinawasaidia wengine. Habari yeyote inayomhusu mtu kama sio njema basi usiiseme mahali kama unajua haitamsaidia yule unaemwambia.
Jifunze kutafuta yaliyo mema juu ya mtu na kama unataka kumuelezea muelezee kwa mema yake. Kuna watu wanabadilika kwasababu sisi tumeweza kuona yaliyo mema ndani yao hata kama ni kidogo.
Jifunze kuzungumza habari njema kwasababu wengine pia watavutiwa kukusikiliza. Ukiwa mueneza habari mbaya utaanza kujulikana kama Mbeya, na wakati mwingine watu wataanza kukuepuka.
Ukiwa mueneza habari njema watu watapenda kukueleza mambo yao kwasababu wanaamini huwezi kwenda kusema popote.
Kama huna sifa yeyote nzuri basi anza na hii ambayo ni rahisi sana na wala haikuhitaji uwe na mtaji wowote. Wewe anza tu kuzisema habari njema kuhusu watu wengine na mwisho wa siku utakuwa umelitengeneza jina lako vizuri na utawasaidia wengine pia.
Habari njema zinajenga.
Habari njema zinatia moyo.
Habari njema ni hamasa ya kusonga mbele.
Habari njema zinawasaidia waliokata tamaa.
Habari njema zinaleta tumaini jipya kwa wale waliotaka kurudi nyuma.
Kuna wale wapelelezi waliotumwa kwenda kuipeleleza nchi ya Kaanani kati yao wote wawili tu ndio walioleta habari njema. Wale walioleta habari mbaya za hofu na za kukatisha tamaa waliuwawa. Hivyo basi Rafiki yangu embu amua kuwa mueneza habari njema kwa wengine. Habari za matumaini na za kuwafanya waone duniani bado ni mahali pazuri kuishi.
Njia rahisi ya kuacha kuwa mtu wa habari mbaya ni wewe kuanza kubadilisha chanzo kinachokupa habari mbaya. Usifuatilie habari mbaya kabisa. Usisikiliza habari mbaya za wengine, ukikuta watu wanawasema watu vibaya waulize hivi hakuna jambo lolote zuri tulijadili hapa? Au unaachana nao unaondoka zako.
Sijasema watu wanaofanya mabaya waachwe hapana, kama mtu kafanya yaliyo mabaya ukimsema au ukaeneza mabaya yake hayatamsaidia yeyote hata yeye mwenyewe. Hivyo basi tafuta namna ya kumsaidia kama unataka kumsaidia. Mfate mwambie au tumia njia nyingine yeyote nzuri na ambayo ungependa wengine waitumie kwako unapokosea.
Kuwa mueneza habari njema kwa kuanza kupokea habari njema.
Ubarikiwe sana,