Watu wengi huchukulia maisha ni kitu cha kawaida sana mpaka wanaamua kuishi kula, kuzaa na kusubiria siku ya kufa basi. Ukweli ni kwamba kama ulikua unawaza hivyo umeshapotea na kama umeweza kusoma hapa leo basi ni wakati wako wa kutafuta njia sahihi, ni wakati wako wa kujitafuta wewe mwenyewe.

Kama kuna kazi ambayo ni ngumu na hakuna mtu ataweza kuja kukusaidia ni kujitafuta wakati ulijipoteza wewe mwenyewe. Lakini leo kama umeweza kusoma Makala hii ni wakati wako wa kugundua kama mahali ulipo ni sahihi au la kama njia unayoiendea ni sahihi au ulishapotea. Kuna watu wengi wamepotea lakini hawaelewi kama wamepotea na bado wanaongeza bidii kuelekea kwenye njia zile ambazo sio sahihi.

Jinsi ya kuweza kujitafuta ni kujichukua na kujipeleka siku yako ya mwisho siku ambayo ndio upo kwenye jeneza na unaagwa na watu mbalimbali na ndugu na marafiki zako wanaokupenda sana. Jaribu kufikiria je ni kitu gani hasa kitakua kinawafanya watoe machozi? Ni kitu gani hasa kitawafanya wasikusahau? Je watalia kwa kua ulikufa kifo kibaya? Watalia kwa kua umeondoka mapema? Watalia kwa kua umeacha watoto wadogo? Siku hizi kuacha watoto sio alama tena ndugu yangu wako wengi wameondoka hawajaacha watoto lakini wameacha historia kubwa sana na ambayo haitasahaulika.

Kitu cha kufanya sasa ni kukaa chini leo peke yako sehemu ya utulivu kabisa na andika mambo gani unataka siku ukiondoka dunia ibaki inayatazama na kulikumbuka jina lako? Ni mambo gani upo tayari kuyafanya ili yawe alama hapa duniani? Ni historia gani unataka isomwe kwenye mazishi yako? Ni wakati wa kuandika historia ya maisha yetu kabla hatujafa. Ni wakati wa kuacha alama kwenye dunia hii. Hujazaliwa kwa bahati mbaya umezaliwa kwa kusudi maalumu. Ni wakati wa kulitimiza kusudi hilo hapa duniani.

Kumbuka hatuishi mara mbili hakuna wakati unaojirudia kama wewe ni kijana kumbuka kwamba ujana wako hautarudi utumie vyema ujana wako kwa ajili ya lile kusudi ambalo limekuleta duniani. Kama wewe ni mzee na uko hai bado sio wakati wa kusubiria siku ya kufa ni wakati wa kufanya yale ambayo hujayakamilisha. Unaweza kutumia mwaka mmoja, mwezi , au hata siku moja kufanya jambo ambalo halitakaa lishaulike katika dunia hii.

Kama unahisi umeridhika na maisha uliyonayo na huna haja ya kufanya kingine wewe una kila kitu una fedha za kutosha, una mali za kutosha, una watoto wa kutosha, naomba jiulize swali moja tu leo, JE UPO TAYARI KUFA LEO? Kama jibu ni ndio hongera sana umeweza kulitimiza kusudi, kama jibu ni hapana anza sasa hujachelewa nafasi bado ipo ya kuacha alama ndio maana bado unapumua. Wako wengi wameshaondoka lakini wewe bado upo sio bahati mbaya una jukumu hujamalizia duniani.

Asante sana na karibu sana
Jacob Mushi 2016

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading