Moja ya jukumu kubwa nililojipa kwa mwaka huu 2017 ilikuwa ni kujifunza kwenye Maisha yaw engine, na hapa ni kuona namna gani wanavyoendesha Maisha yao kuanzia ndani hadi nje. Yapo mengi sana kama binadamu unaweza kujifunza kwenye Maisha ya wenzako kwasababu tumeumbwa tofauti, tumekulia kwenye mazingira tofauti na kila mmoja ana kusudi la yeye kuwepo hapa duniani.
Huwezi kueleweka na Kila Mtu.
Changamoto zipo nyingi sana kwenye Maisha ya wengine. Ni ngumu sana kama unataka watu wakuelewe unaweza kujikuta hujaishi Maisha yako hapa duniani umebaki ukifanya vitu ili wengine waelewe unafanya nini.
Maisha ya wengi yamekuwa magumu kwasababu wanaishi Maisha ya kutaka kuonekana na kueleweka. Maisha ya wengi yanaharibika kwasababu badala ya kufanya kile ambacho mioyo yao inapata faraja wanakuwa wanafanya mambo ambayo yatawafurahisha wengine.
Sio ajabu sana mtu kununua nguo ya ghali sana ili tu aonekane amependeza ili hali kwenye Maisha yake hana chanzo chochote cha fedha.
- Soma: USIRUDIE KOSA HILI 2018
Ukitaka kuishi Maisha bora acha kuwaelewesha watu, ishi Maisha yako wanaoelewa wataelewa wasioelewa achana nao.
Ukosefu wa Vipaumbele.
Maisha ya wengi hayana vipaumbele, na wengi hawawezi kuweka vipaumbele kwasababu hawajui wanataka nini, hawajui wanakwenda wapi, hawajui ni kitu gani Mungu ameweka ndani yao.
Kama hujui unapigania nini hakuna maana ya wewe kwenda kupigana, kwa maana hata ikitokea umepata ushindi hutajua umeshindia kitu gani.
Tuna watu wengi wapo vitani lakini hawajui kwanini wanapigana. Wewe kwenye Maisha yako unapigania nini? Ni kitu gani ambacho hakuna mtu mwingine anaweza kuja kukuondoa kwenye hicho?
Maisha yako yanakwenda kwa kufuata misingi ipi?
Je ni siasa?
Ni Dini?
Ni Kusudi La Mungu?
Ni Maisha Bora?
Ni kuacha alama?
Ni kipi hasa unachokipigania?
Ukishindwa kutambua utajikuta Maisha yako yote unakimbizana na lolote linalokuja mbele yako. Utashindwa kujua adui yako unaepigana nae ni nani? Utashindwa kutambua ushindi wako uko kwenye nini.
Kabla hatujamaliza mwaka huu hakikisha umeshajitambua unapokwenda. Hakikisha umejua ni vitu gani hasa unapaswa kuvifanya hadi unaondoka hapa duniani na asitokee yeyote akakutoa humo.
Binadamu wanabadilika.
Watu wengi hawana misimamo na wanaogopa sana kujitoa (commitment) kwenye mambo. Binadamu wengi wakisema hapana unaweza kukuta wanamaanisha ndio na wakisema ndio unaweza kukuta wanasema hapana.
Aina ya watu ambao mara zote naogopa kufanya nao kazi ni watu waliokosa misimamo. Mtu asiye na msimamo anaweza kukuangusha vibaya sana. Unapojitoa kwa asilimia mia moja kwa ajili ya jambo na yeye akawa anatazama pembeni hamuwezi kufika mwisho.
Unapofanya maamuzi yeyote yanayounganisha watu wengine ni vyema ukatambua kwamba watu wanabadilika sana tena bila ya wewe kujua. Ni vyema sana ukajipa muda wa kutosha na kumpa majaribio mbalimbali kupima namna mtu alivyojitoa kwenye jambo mnalotaka kufanya pamoja.
Unaweza kufanya jambo na mtu wewe unawaza miaka 20 kumbe yeye anawaza miaka miwili tu lazima mtu huyu mtashindwana.
Unachopaswa kujua binadamu wanabadilika hata yule uliemwamini kwa asilimia mia moja hujui moyoni mwake anawaza kitu gani.
Sio kila anaezungumza anamaanisha anachokisema.
Sio kila Ahadi unayopewa ni ya Kweli, nyingine ni za kukufanya uendelee tu kuwa na subira.
Jacob Mushi,
Mwandishi, Mjasiriamali, Kocha wa Maisha, Mshauri na Mtaalamu wa Blogger .