Njia Bora Ya Kuishi Kwenye Ulimwengu Huu Wenye Masumbufu Mengi

By | September 29, 2018

Tupo kwenye ulimwengu ambao kama usipokuwa makini unaweza kujikuta miaka inakwenda na hakuna cha maana ambacho umekifanya katika kuitimiza Ndoto yako. Ulimwengu huu wenye masumbufu ya kila aina ambayo yanatutoa kwenye mstari na kutufanya tuwe na matokeo hafifu kwenye kazi zetu.

Dunia ya sasa unaweza kufanya jambo lako na baada ya dakika chache unajikuta umekata tamaa kwasababu ya kitu alichoweka mtandaoni mtu mwingine hata usiemjua juu ya kazi yako. Kila mmoja anatoa maoni yake, kila mtu anaweza kujaribu kukushauri jinsi ya kufanya kazi yako na mwisho wa siku unajikuta hakuna unachokifanya.

Dunia hii ya sasa imekuwa ni ya kukimbizana yaani kuangalia mwingine anafanya nini ili na wewe ufanye. Mwisho wa siku unajikuta hujafika mahali popote bali umekuwa unafukuzana na watu ambao wanafanya vitu.

Hii dunia imetufanya tuwe watu wenye huzuni kwasababu ya kutaka kukubalika kwenye kila tunachokifanya. Tumewekewa batani za likes kwenye vitu tunavyoweka mitandaoni hivyo kila mmoja anajaribu kuweka vitu ambavyo vitawafanya wengine wabonyeze like.

Wengine wanadiriki hata kuweka picha zao za utupu ili tu wapate like Nyingi. Hii imekuwa kama kilevi kama madawa ya kulevya, nikiwa na maana ya kwamba mtu anapoweka kitu mtandaoni na hajapata like Nyingi kama wengine anajisikia vibaya, anajiona kama vile hana thamani.

Inawezekana na wewe umekuwa mmoja wa watu wa aina hii. Unafanya jambo na unapoona watu hawajalikubali unajisikia vibaya. Inawezekana umekuwa mtumwa wa kutegemea maoni ya wengine ndipo uchukue hatua yaani mpaka wengine waseme ni wazo zuri sana hilo ndipo unaanza kuchukua hatua.

Hali hii imeondoa ufanisi katika mambo mengi na hivyo kusababisha mambo mengi kuwa ya hovyo. Wengi wanafanya kwa haraka haraka ili tu wakubalike na wengine.

Ipo dawa ya kujiondoa kwenye tatizo hilo, na dawa hiyo nimekutengenezea wewe Rafiki yangu. Naamini itakwenda kukusaidia kweli. Uache kutumia kilevi hiki cha kisasa kinachotolewa na mitandao ya kijamii, kilevi cha likes na comments.

  • Njia unayoweza kuepuka kuwa mlevi wa kilevi hichi ni wewe kujua una majukumu yapi hapa duniani. Jitambue kwanza wewe mwenyewe, anza kuwajibika katika kulijua kusudi la wewe kuwepo hapa duniani.
  • Ukishajua kwanini ulizaliwa anza kuishi kusudi, kuwa wewe, jikubali kwanza kabla hata hujapewa sifa yeyote na mtu mwingine.
  • Tengeneza maono makubwa sana ambayo utakuwa unayaishi kila siku. Hakikisha kila siku kuna kitu unachokifanya ambacho kinaonesha uwepo wako hapa duniani.
  • Tumia vizuri muda wako, usikubali kupoteza muda wako hovyo kwa kuishia kupitia pitia kwenye mitandao ya kijamii kuona wengine wameweka nini.
  • Itumie mitandao ya kijamii kwa lengo la kujifunza au kibiashara.
  • Tumia muda mwingi kwa familia na marafiki kuliko mitandaoni.

Kama mpaka sasa unasua sua na hujui ufanye nini basi omba msaada kwa wanaofundisha. Bahati nzuri upo na mimi hapa, na nimejitoa kukusaidia. Ukiwa na uhitaji wowote unaweza kuwasiliana nami tukasaidiana.

“Usikubali kuwa mtumwa/mlevi wa kitu chochote ambacho hakikufanyi kuwa bora.”

Usisahau kujiunga na MasterMind Coaching hapa >>> www.jacobmushi.com/kocha

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

www.jacobmushi.com/huduma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *