507; Yanapotokea Usiyoyatarajia.

jacobmushi
3 Min Read

Ni kweli mtu unaweza kuwa na fikra hasi juu ya Maisha yako lakini hakuna mtu hata mmoja anaetaka zile fikra hasi zitokee. Kinachomfanya mtu ajikute anawaza sana ni kwasababu ya hofu. Kila mtu huogopa pale anapowaza mambo mabaya yatatokea siku moja, kila mmoja anaweza kusita kuchukua hatua pale anapohisi kuna jambo baya litatokea kwenye kile anachotaka kufanya.

Maisha kwa ujumla hayatabiriki kuna mambo mengi sana huwezi kuyatabiri yatakuwaje kwa kuangalia hali iliyotokea jana. Vipo vitu vichache ambavyo twaweza kuvitabiri kulingana na kwamba huwa vinatokea kwa kujirudia rudia siku zote. Lakini yapo matukio mengi ambayo huwezi kutabiri yatakuwaje.

Nataka uelewe kwamba linapotokea jambo lolote baya kwenye Maisha yako usikubali kufa moyo kwasababu ni hali tu zinatokea kwa kila mtu. Ni matukio ambayo kila siku yanatokea kwenye Maisha ya wanadamu. Kuna sehemu watu wanalia na kuna sehemu watu wanashangilia.

Kuna mtu amefukuzwa kazi yupo katikati ya majonzi na kuna mtu amepandishwa cheo au kapata ile kazi aliyokuwa anaitafuta kwa muda mrefu sana. Hivyo basi chochote kinachotokea sio mwisho wako, kama kimekuacha hai basi sio mwisho wako kuna nyakati zinakuja na mambo makubwa yataanza kutokea kwenye Maisha yako.

“Juzi kuna mzigo nilipeleka kwa mteja na nikajikuta nimetumia gharama kubwa sana ya usafiri kutokana na kuwa mgeni kule nilipopeleka mzigo. Sasa nikasema hii hasara itakuaje, nikajipa moyo kwamba pamoja na nimepata hasara ya pesa, nimepata pia funzo, nimefika sehemu ambayo sijawahi kufika, na pia nimejifunza kuwa mwangalifu. Sikulalamika wala kumdai yule mteja gharama zilizoongezeka. Sasa siku chache mbele nikapokea simu maeneo yale yale niliyoona nimepata hasara mteja mwingine akawa anataka mzigo mara 10 ya ule niliopeleka mwanzo. Ile hasara niliyokuwa naiona mwanzo ikawa imefukiwa kabisa na yule mteja wa pili. Ule mzigo nikaweza kuupeleka kwa urahisi na gharama nafuu Zaidi kwasababu tayari nilishafahamu njia vizuri Zaidi.”

Nataka ujifunze nini? Chochote kibaya kinachotokea usiwe mwepesi wa kulaumu wala kulalamika sana. Unapolalamika unazizuia baraka nyingine kubwa kuja. Mfano ningemshikilia yule mteja wa mwanzo anilipe gharama nilizopoteza kwa kutokujua njia huenda huyu mteja mwingine nisingempata kwasababu yeye ndie aliemwelekeza. Labda angeniona huyu kijana ana tamaa sana na ni msumbufu, nikabeba hasara lakini ikaja na faida kubwa Zaidi.

Usikubali yanapotokea mambo mabaya usiyoyatarajia yakusababishe uharibu yale mazuri ambayo yangekuja mbele yako. Unapopatwa na jambo lolote baya usilolitarajia jua kwamba kuna zuri kubwa Zaidi linakuja usilolitarajia. Usiwe unalalamika angalia upande mzuri uliofaidika na lile jambo baya,

Rafiki yako,

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
6 Comments

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading