Nipo natazama nyimbo YouTube nimekutana na wimbo uliwekwa mwaka 2009. Huo wimbo kwa mimi kuutazama leo pamoja na wengine wengi huyo mwimbaji atalipwa na YouTube (Google) mamilioni ya pesa. Nilichojiuliza ni kwamba huyu mwimbaji wakati anatunga wimbo huenda hakuwahi kuwaza kama mwaka huu 2019 huo wimbo wake bado ungeendelea kuingizia pesa.
Nataka niseme na wewe unaefanya kitu chako sasa hivi, huenda ni kitabu, nyimbo, igizo, au chochote ambacho kinaweza kuendelea kutumika hata baadae. Nataka nikwambie endelea kufanya kwa ubora wa hali ya juu. Tumia uwezo wako wote ulionao sasa hivi.
Miaka kumi ijayo hatujui dunia itakuaje, kuna vitu vingi sana vinaweza visiwepo tena hasa unavyovitumia sasa hivi. Lakini hiyo kazi yako itakuwepo. Huenda na wewe kwa kipindi hicho kutakuwa na watu wenye umri sawa na watoto au wajukuu zako wakifurahia kazi ulizofanya miaka iliyopita.
Muhimu usiangalie faida unayopata sasa hivi angalia kule unapokwenda, angalia kugusa maisha ya watu.
Nilikua namsikiliza Bilionea mmoja anasema wakati wanapata wazo la biashara yao hawakuwahi kuwaza kufika hapa walipo sasa hivi (Netflix) idea yao ilikuwa ni kuuza cd na dvd kwa njia ya kuwatumia watu.
Tunapozungumza sasa hivi ni story nyingine kabisa. Kile Unachokifanya kifanye kwa kukipenda, penda yale matatizo unayotatua, penda watu unaowatatulia matatizo yao, hutachoka. Endena na mabadiliko Jifunze vitu vipya vinavyokuja ili usihe kuachwa nyuma. Kaa na watu wanaojua vitu ambavyo huvijui, usikae zaidi na wale mnaofanana kimawazo, jichanganye na watu ambao wana vitu ambavyo huna kichwani kwako.
Kitu kingine kama Unachokifanya unakipenda usikiache endelea kufanya, tafuta suluhisho la matatizo, usikimbie. Usiishie Njiani. Kama umeamua kuwa mwandishi andika kuwa bora, umeamua kuimba imba, tafuta kila njia sahihi, usikubali chochote kikuzuie, kuwa bora Zaidi ya jana.