Jaribu kuvuta picha upo katikati ya msitu, unatafuta samaki. Umejipanga kila kitu unacho, una chambo za kutosha, una vifaa vya kubebea na pia una hamasa na nguvu za kutosha kutafuta samaki. Kitu kimoja ambacho kitakufanya uendelee kuwatafuta samaki Maisha yako yote ni kwamba ulikuwa huna ufahamu kwamba samaki hawapatikani msituni wanapatikana majini.

Haijalishi utakuwa na hamasa kubwa kiasi gani, haijalishi utakuwa umejipanga vya kutosha kiasi gani endapo hao samaki utakuwa unawatafuta porini ni ngumu kupata samaki. Mwisho wa siku utarudi na kusema hakuna samaki, utarudi na kusema kupata samaki sio kazi rahisi.

Hadi pale atakapotokea jamaa mmoja akwambie kuwa unakosea samaki huwa hawapatikani porini wanapatikana kwenye maji, unaweza kwenda kuwatafuta mtoni, bwawani, ziwani au baharini. Kinyume nah apo utaishia kuamini kwamba sio rahisi kupata samaki kwasababu wewe ulikuwa unawatafuta porini.

Kwenye Maisha yetu tuna watu wengi waliokuwa wanatafuta samaki porini wakakosa. Ukikutana nao hawa watakwambia na kukuhakikishia kabisa kwamba huwezi kupata samaki kwasababu wao walitumia Miaka kadhaa kuwatafuta na hawajapata. Ukikosea kidogo kuwaamini bila kujua kuwa walikuwa wanatafutia porini utaishia Njiani.

Ni vyema sana kabla hujamsikiliza mtu anaekwambia haiwezekani basi umuulize maswali ya kutosha kwasababu wengine kwao imekuwa haiwezekani kwasababu walikuwa wanatafutia samaki porini badala ya kwenye maji. Usikubali kusikiliza tu kila taarifa kwasababu wengine wanaweza kukupotosha kwa kutokuelewa kwao.

Kuna mengi tangu zamani umekuwa unaaminishwa kwamba haiwezekani au kitu Fulani huwezi kupata mpaka upitie mahali Fulani kumbe ni uongo. Na kizazi hata kizazi kimekuwa kinaamini uongo wa namna mbalimbali. Sasa mtu anasema huwezi kufanikiwa kama hujasoma, au ukifeli shule ndio Maisha yako yameharibika halafu wewe unamuamini na unakata tamaa kabisa baada ya kufeli shule. Kumbe hiyo haikuwa kweli bado una uwezo wa kwenda kutafuta kile unachokitaka endapo utajua kwamba mahali kinapopatikana ni wapi.

Naomba ujiulize sana Swali hili, Je Hiki ninachokitafuta nakitafutia sehemu sahihi?

Maana yawezekana hupati unachokitafuta kwasababu unakitafutia sehemu ambayo sio sahihi.

Mtu anapokwambia haiwezekani usikubali kirahisi hata kama ni mtu unaemuamini sana kwasababu huenda nay eye alikuwa anatafuta samaki porini bila kujua halafu akakuaminisha kwamba na wewe hutaweza kupata samaki maishani mwako.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading