505; Mama Usimtukane Mwanao.

Nilikuwa napita katika mitaa ya uswahilini hapa Tandika, sasa nikakutana na mama mmoja anamwogesha mwanae wa kiume. Sasa yule mtoto akawa anasumbua sumbua, yule mama akamporomoshea matusi mazito ya nguoni. Yaani alimuita viungo vyake yeye mwenyewe vya siri, nilisikitika sana, nikawaza huyu mtoto akija kupata akili sawasawa akaja kujua maana ya kile anachotukanwa na mama yake atakuwa mtu wa aina gani?

Unajua tumezoea kusema yale maneno watu wanasema juu yako hayana maana sana kama kile unachosema juu yako mwenyewe. Hili ni kweli lakini kwa Watoto wadogo hawana maneno ya kusema juu yao, hawajui mazuri na mabaya. Sasa jiulize tangu akiwa na umri wa kuanza kutembea anatukanwa matusi mazito ya nguoni akili yake itakua ikibeba vitu vya aina gani?

Tuna kizazi kibovu sana lakini naomba tukumbuke kwamba hakijajiharibu chenyewe, yale maneno unayomuita mwanao yanamharibu. Ukimuita mtoto wa kiume viungo vya uzazi vya mwanamke akija kukua akawa shoga Usithubutu kumlaumu, wewe ndio umemtengeneza. Nataka nikwambie acha mara moja, na ukiona popote pale mtu anamtukana mwingine mwambie aache mara moja, ukiona mtu anamtamkia mabaya mwenzake mwambie aacha mara moja.

Tunatengeneza majambazi, tunatengeneza wanawake wanaojiuza, tunatengeneza wanaume wanaobadili jinsia zao na kuwa wanawake kwa maneno na vitendo tunavyotamka na kufanya mbele yao. Naomba nikwmabie mtoto wako hanijui mimi angejifunza kwangu, hajui maneno ya Mungu angejifunza, mtu pekee anaejifunza kwake ni wewe, cha ajabu anachoambulia kwako kama somo ni matusi mazito na vitendo visivyofaa. Akija kuwa mtu mbaya jamii nzima inamlaumu na kumtenga wakati mwingine inataka hata kumuua.

Nataka nikwambie unaweza kuibadili dunia kwa kufanya kitu kimoja nenda nyumbani ukaipende familia yako, Alisema Mother Theresa. Kuipenda familia yako ni pamoja na kuwatamkia na kuwatendea yaliyo mema. Unaweza kuanza upya, tengeneza kizazi ambacho unakitaka.

Usimtamkie mtu neno ambalo unajua kabisa sio zuri, kwasababu huyu mtu akija kuharibika atakuja kukuharibu na wewe pia. Akija kuharibika atakuja kuharibu na Watoto wako, ndugu zako unaowapenda. Popote pale ulipo ongea wema na tenda wema.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading