Umeshawahi kuangalia mashindano yoyote? Au sherehe za ugawaji wa tunzo?/ Bai kama umewahi kuangalia kuna kitu ambacho kinajirudia kwa watu wote wanaoshinda. Huwa wanatoa insha ndefu na kutaja majina ya watu waliowasaidia kufika hapo walipo, na wakati mwingine huwa wakilia kwa furaha ya jinsi hao watu walivyohusika katika ushindi wao wa hiyo tunzo au hayo mashindano. Kuanzia hapo ndo nilipogundua kwamba ili kufanikiwa unahitaji watu, unahitaji timu ua wanaokusapoti. Kwa ufupi mimi ni mtoto wa pekee kwetu, nimedekezwa, nimezoeshwa kuwa mimi peke yangu, na wakati nakua nimekaa muda mwingi peke yangu kwahiyo nimekuwa nikiamini kwamba kila jambo naliweza mwenyewe na sihitaji msaada wa mtu yeyote kwenye maisha. Imenichukua miaka 22 kugundua kuwa dunia ina watu bilioni 7 kwasababu Mungu hakutaka mtu mmoja peke yake ndio afanye mambo mbalimbali. Imenichukua muda mrefu kugundua umuhimu wa watu waliopo kwenye maisha yangu, na imenichukua miaka mingine mingi kujifunza kuwakubali hao watu, na kuishi nao vizuri na kwa ukaribu, lakini zaidi ya wote kuwatumia katika kunisaidia katika mafanikio yangu.

Kuwatumia huku simaanishi kuwa na urafiki na watu kwaajili ya faida zako hapana, na maanisha watu walio karibu yako ambao kwa sababu wanakujali, kwasababu wanataka waone unafanikiwa wanachangia vitu chanya kwenye maisha, labda ni mawazo, nguvu zao, pesa zao au nafasi mbalimbali kwaajili ya wewe kufanikiwa. Katika dunia ya sasa ambayo kila mtu anajiaminisha anaweza kufanikiwa mwenyewe, katika dunia ambayo kuna mashindano sana ya mafanikio au hata kushindana na wale ambao wangekunyanyua hapo ulipo, nina sababu kumi kwa nini unahitaji watu wanaokuongezea vitu chanya kwenye maisha yako,sababu kumi kwa nini unahitaji watu ambao watachangia kwenye mafanikio yako:

1. Unahitaji watu watakaokutia moyo kuendelea na mwendo utakapokata tamaa- Hata Usain Bolt alikuwa na mtu wa kumtia moyo na kumkumbusha kwanini anakimbia, japo kuwa huyo rafiki yake yeye alikuwa hakimbii.

2. Watu wamepewa vipaji/ vipawa/ ujuzi tofauti na chako ambao mkifanya kazi pamoja mtatengeneza kitu kikubwa na kizuri zaidi ya vile ambavyo ungefanya peke yako.

3. Umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu- hata bank inakuwa rahisi sana kuwakopesha kikundi kuliko mtu mmoja, mkiwa pamoja mnafanikiwa katika mambo haraka kwasababu wafikiriaji wa hilo swala wanakuwa wengi, lakini pia watendaji wanakuwa wengi.

4. Unawapa nafasi watu ya kuifanyia kazi ndoto yako- sio wote ni waanzilishi kwenye maisha, wengine ni watu wanaotakiwa kuifanyia kazi maono ya mtu kwa moyo mmoja, ni watu ambao Mungu anawaleta kwenye maisha yako kwaajili ya kukusaidia kutimiza maono yako,unapotaka kuwa mwenyewe unawanyima watu nafasi ya kushirikiana na wewe kutimiza maono.

5. Unajengeka na kuwa bora- mara nyingi watu huongeza kwenye maisha yetu na kutufanya kuwa bora, kwa kutupa maoni ya vitu tunavyotakiwa kuongeza au kupunguza katika mambo tunayoyafanya, kama mtu kuna vitu vya kuvibadilisha kwa jinsi unaishi au jinsi unavyofanya kazi, ukiwa na watu wanakusaidia kuwa bora.

6. Wakati nasoma ujasiriamali tulijifunza kwamba wajasiriamali wengi wanateseka na upweke, ukifanya kazi na watu wanakuondolea upweke kwani hao ndio unaokutana nao, na kujenga nao ukaribu na urafiki.

7. Kufanya kazi katika timu na kufanikiwa pamoja kunakuondolea kujisifu na majivuno kwasababu unaona kabisa sio wewe uliyefanikisha ila ni timu nzuri, na ndio maana hata kwenye mpira hata kama goli kafunga Ronaldo linakuwa la timu nzuri kwasababu inahitajika timu nzima ili kufanikisha hilo goli.

8. Kuongeza ubora wa kile unachokifanya- ukiwa peke yako mafanikio utakayoyapata ni ya mtu mmoja ila ukiwa na watu wengi utapata mafanikio ya watu wengi kwa wakati mmoja na hivyo kitu kitakachotoka ni bora ya kile ambacho ungekifanya peke yako.

9. Unapata ushauri na maoni- pasipo ushauri watu hupotea, pasipo ushauri watu huangamia, pasipo ushauri watu huaribu brands zao na majina yao, pasipo ushauri watu husahau nia lakini pia hukosa moyo wa kuendelea kufanya wanayoyafanya. Kuna watu wengi ambao wamefanikiwa huwa na watu wanaowashauri kabla hawajafanya jambo fulani au kuamua uamuzi fulani kwasababu uamuzi mmoja unaweza kuharibu jina ulilojaribu kulijenga kwa miaka kumi.

10. Lakini pia unahitaji watu watakaokujua kwa undani kwa ukaribu- mafanikio yanagharama sana na kama hautokuwa na watu wanaokujua vile ulivyo ni rahisi sana kupotea na ukakosa watu watakaokuelekeza njia nzuri ya kwenda. Ni vizuri kuwa na watu wanaokuamini ili kufanikiwa, watu wanaokujua vizuri kwa ukaribu na ambao wako tayari kuongea mazuri kwa ajili yako.

Na hizo ni sababu kumi za kwanini unahitaji watu ili kufanikiwa, katika utamaduni na kipindi ambacho kujitegemea kumekuwa sana na kujiona unajiweza na unaweza kufanya lolote wewe mwenyewe, nimeamua kukukumbusha kwanini unahitaji watu ili ufanikiwe.

Eunice Tossy
abiblegirl.blogspot.com

One Response

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading