Habari za Leo Rafiki yangu. Natumaini unaendelea vyema na kupambana pamoja na kutafuta mafanikio kwa bidii. Leo ninapenda tuangalie sehemu mbili za kuzingatia wakati tunatafuta pesa kwa bidii.

Ni kweli Maisha ya sasa huwezi kuyafurahia hata kidogo kama huna pesa za kutosha. Na pesa za kutosha zinapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kujifunza mambo mbalimbali ya uwekezaji. Ukiweza kupata hizo pesa za kutosha tunaanza kusema wewe una uhuru wa kipesa. Yaani wewe matatizo yote yanayohusu pesa kwako sio matatizo tena kwasababu unaweza kuyamudu.

Kabla ya kufika huko kwenye uhuru wa kipesa unatakiwa utambue kwamba kwenye dunia hii kuna mambo mawili yakikaa vibaya hata kama una pesa kuliko wote hapa duniani hutaweza kuishi Maisha yenye Amani ya moyo. Kwanza kama mwili wako utakuwa unasumbuliwa na magonjwa huwezi kushi kwa raha wala kutumia pesa kwa raha. Pili kama mahusiano yako ni mabovu huwezi kufurahia pesa ulizonazo hata kidogo.

Mambo Haya Yazingatie Sana.

Afya Yako.

Kwa vyovyote vile hakikisha unapotafuta pesa kwa bidii unaikumbuka afya yako mara kwa mara. Kuikumbuka na kuijali afya yako kunaonyesha ni namna gani unavyojipenda. Kama utashindwa kuangalia afya yako ni ukweli kabisa hutaweza kujua afya za wengine kama ni nzuri. Kama wewe mwenyewe unazembea kwenda hospitali kucheki afya yako mara kwa mara huwezi kuwahimiza wengine.

Soma: Hiki ndio Kitu Muhimu Kuliko Vingine

Ili uweze kuwajali wengine anza kujijali wewe mwenyewe. Fanya mazoezi kila siku uepuke magonjwa yatokanayo na kutokufanya mazoezi. Kula vyakula bora ili kueopuka magonjwa na mwili usio na afya.

Sidhani kama utafurahia Maisha umekuwa bilionea halafu una kansa. Kansa hii imeletwa na uzembe wako wa kutokucheki afya yako mara kwa mara na kutokujijali. Sidhani kama utafurahia Maisha wakati umeshapata pesa zote halafu unaambiwa una tatizo la nguvu za kiume.

Matatizo ya afya ni mengi sana na mengi yamesababishwa na uzembe wetu binafsi, kuiga Maisha ya wengine. Kupendelea vitu virahisi badala ya kuandaa vyako mwenyewe. Kula vyakula vibovu. Watu wengi wakaula ili washibe na sio kwa ajili ya afya na kujenga miili yao.

Usisubiri hadi uambiwe na Dokta ule matunda na mbogamboga anza kuzila wakati huu ni kwa faida yako mwenyewe. Watu wengi ambao wanazijali afya zao ni watu wasiosumbuliwa na magonjwa.

Sipendi nije kusikia unasumbuliwa kwa magonjwa yanayosababishwa na ulaji mbovu wa vyakula. Ni hatari sana kwa afya yako na hutaacha alama nzuri kwenye dunia hii.

Ijali afya yako nayo itakujali wakati unaihitaji. Ili uweze kuwa na uzalishaji bora unatakiwa uwe na afya bora.

Mahusiano Yako.

Mahusiano yamegawanyika katika sehemu kuu mbili.

Mahusiano yako na Mungu.

Kama utamsahau Mungu hata ukipata pes azote utakosa Amani ya moyo kwenye Maisha yako. Ni vyema sana wakati huu unapopambana na kuzitafuta pesa uwe karibu na Mungu wako. Jijengee tabia ya kumuomba, kuongea nae. Mweleze shida zako. Kaa nae karibu na Maisha yako yatafanikiwa.

Hakuna binadamu ambaye anaishi kwa Amani kama hana Mungu ndani yake. Mtafuteni Mungu kwa bidii nanyi muipate Amani yake.

Katika kila jambo unalofanya mtangulize yeye kwanza. Anapotangulia Mungu atakuonyesha njia vyema. Anapotangulia yeye atakuonyesha ni wapi sahihi pa kupita. Kuna nyakati utapitia changamoto kubwa sana lakini kwasababu ulimweka mbele atakuwa msaada wako.

Hudhuria ibada usisubiri umepata matatizo ndio unakwenda kanisani au msikitini kutafuta msaada. Wakati huu huu unapotafuta pesa kwa bidii nenda ibadani kwa bidii. Sidhani kama kuna binadamu anapenda kutafutwa na watu wakati wanashida wanahitaji watatuliwe. Hata kama ni wewe ukiona kuna marafiki au ndugu zako wanaokutafuta kipindi wana shida za pesa pekee yake hutawapatia. Mara nyingine utawaona hawa wananitafuta kipindi wana shida tuu.

Mungu yeye si kama mwanadamu ndio lakini haimaanishi ndio tumtafute wakati tuna matatizo. Hata wakati wa furaha pia kaa karibu na Mungu wako.

Soma: Mambo matatu ya Kuzingatia Kila Siku

Mahusiano yako Na Wengine.

Hapa tunaangaza mahusiano yako na wanadamu wenzako. Kama wewe kwenye dunia hii utakuwa na mahusiano mabovu na wengine huwezi kufurahia pesa zako. Kwanza hakikisha kile unachokifanya kinaleta furaha kwenye Maisha ya wengine.

Usidhulumu wengine. Usiumize mioyo ya wengine kwa makusudi. Timiza kile unachokiahidi kwa wengine.

Maisha yako yatakuwa na furaha sana na Amani kama watu waliokuzunguka watakuwa wanafurahia uwepo wako hapa duniani. Watu watafurahia uwepo wako hapa duniani endapo unawagusa kwa kile unachokifanya.

Nikwambie ukweli ukitafuta pesa kwa bidii ukanunua gari nzuri sana kisha ukaendesha umekaa na mwenzi wako hamuongei mmenuniana gari halina raha yake. Umejenga nyumba nzuri sana nay a gharama lakini ndani unashindwa kutabasamu watoto wakikuona wanasema baba kwanini ulituacha hiyo nyumba haiwezi kuwa na Amani.

Wakati huu huu wa kuwa bize hakikisha wanaelewa kwanini upo bize. Hakikisha yule umpendae hapati maswali juu ya ubize wako. Kuwa muwazi kwake na hakikisha anapata Amani ya moyo. Yeye ndie anatakiwa awe mtu wa kwanza kukutia moyo unapopitia magumu na kukupongeza unapofanya vizuri.

Rafiki Yako,

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading