“Kuna kipindi Fulani nilisafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kikazi. Nilipofikia kwenye familia moja ambayo ilikuwa inanifahamu. Sikuwa nawafahamu sana watu kwenye ile familia Zaidi ya baba mwenye familia ambaye alikuwa mwenyeji wangu.

Wakati naendelea kukaa pale nilitokea kuzoeana na binti yake sana hadi nikaanza kuona hisia za upendo. Kiukweli nilikuwa namheshimu sana mzee yule hivyo nikaona haitakuwa vyema sana nikaanza mapema kumweleza huu binti kwamba nampenda. Nikasema ngoja nirudi nyumbani tutawasiliana halafu ndio nitakuja kumwambia siku moja.

Baada ya kazi kuisha nikaondoka huku nikiwa na mawasiliano ya yule binti. Tuliendelea kuwasiliana kwa muda na baada ya mwezi mmoja hivi tukapotezana akawa hapatikani kwenye simu tena ghafla. Sikuwa nimemwambia chochote hivyo sikuweza kujaribu kumuulizia kwa baba yake.

Baada ya miaka miwili kupita nikaja kukutana nae kwenye mtandao wa Facebook na tukaanza kuwasiliana tena. Akaniambia ameshaolewa na ana Watoto. Hapo hapo akanieleza kwanini niliogopa kumweleza kuwa nampenda kwani hata yeye alijua hilo. Akasema alikata tamaa baada ya kuona siongei chochote na baada ya kupoteza simu hakuthubutu kumuomba baba yake namba zangu.” Alinisimulia Rafiki yangu.

Hii inatufundisha kwamba kama usipoamua kuchukua kwenye chochote kile unachokitaka basi kitaishia kichwani kwako. Haijalishi umekuwa na hamasa kiasi gani, haijalishi umekisifia kiasi gani endapo tu hutaanza hatua ya kwanza ya matendo huwezi kukipata. Huyu Rafiki yangu angeweza kufanya kitendo kimoja tu kusema yaliyoko moyoni mwake basi lakini alisita na kukatokea kikwazo.

Tumezoea kusema ndoto zetu kwa watu ni kweli inahamasisha sana, ile leo nataka kukwambia hiyo ndoto ili iwe yako ni pale tu utakapoanza kuifanyia kazi. Haijalishi umewaza na kuandika mambo makubwa kiasi gani bado unatakiwa uimiliki ndoto yako kwa kuifanyia kazi ili ionekane kweli.

Ule wimbo uliouta jana usiku sio wako mpaka uende studio kurekodi.

Lile ghorofa unalowaza kulijenga sio lako mpaka pale utakapoanza kuweka matofali chini.

Yule mke/mume wa ndoto yako unaewaza kuwa nae sio wako mpaka pale utakapochukua hatua ya kumfuata na kumueleza yaliyopo ndani ya moyo wako.

Acha kupoteza muda Rafiki kile unachokiwaza kuna mwingine pia anakiwaza. Kadiri unavyoendelea kuchelewa kuchukua hatua ndio na wengine wanachukua hatua kwenye yale mawazo yako uliyoyawaza.

Mungu hajakueletea hilo wazo likae kichwani kwako tu. Ukishindwa kulitekeleza atalihamishia kwa mtu mwingine anaeweza kuchukua hatua.

Anza sasa kuchukua hatua ili umiliki ndoto yako. Anza sasa kuwekeza ili umiliki ndoto ya kufikia uhuru wa kifedha. Anza sasa kuandika ili kile kitabu kitoke kichwani kije kwenye uhalisia watu wakisome.

Usiahirishe ukitaka kuimiliki ndoto yako ni lazima ukubali kuchukua hatua Madhubuti na usiwe mtu wa kukata tamaa.

Mchakato ndio unaleta matokeo usiishie kuwaza bila kutenda. Mahindi hayawezi kuota shamba kwa kuwaza. Lazima utoke uende shambani ukafanya mchakato wa kuotesha mahindi.

Nakutakia Kila la Kheri katika kuimiliki ndoto Yako.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/huduma

8 Responses

  1. Daaah asante sana mentor anguu ww n zaidi ya rafiki kwangu umenigusa sana na huu ujumbe.
    Asante pia kwa kunikumbuka mara kwa mara nakuombea kwa mungu akuzidishie mara dufu.

  2. Ahsante sana mpendwa wangu hakika Mungu wa mbinguni akubariki sana kwa huduma hii ya kutufungua vijana hakika makala hii ya kutimiza ndoto imenigusa kama vile nimewai kukusimulia yani

  3. Umetisha mkuu kweli ni wakati wa kuvitoa vitu kichwani asante sana kwa makala nzuri kazi yako ni njema na nakuhakikishia siyo bure unachokifanya .

Leave a Reply to Jacob MushiCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading