SURA YA 431; Tai Alievunjwa Mbawa.

jacobmushi
By jacobmushi
2 Min Read

Siku Moja Mzee aliekuwa anafuga kuku kwenye Kijiji fulani, alikuwa anapita porini akaokota yai kubwa ambalo hakuelewa ni la Ndege gani.

Aliamua kulichukua yai lile na kuliweka katika mayai yaliyoanza kuatamiwa siku za Karibuni.

Baada ya siku kadhaa kupita yule kuku akawa anatotoa mayai yake na kama muujiza hivi na lile yai kubwa likatotolewa.

Kumbe yai lilikuwa ni la Tai. Mzee akawa amefanikiwa kupata kifaranga cha Tai akafurahi sana.

Yule kifaranga akaendelea kukua na pia akawa anajiona tofauti na vifaranga wengine. Kwanza alikuwa mkubwa na mbawa zake zilikuwa kubwa na zenye nguvu.
Siku moja alikuwa anajaribu kuruka angani kwasababu ya ile asili ya tai ni kuruka juu hivyo akajikuta anatamani kuruka.

Majogoo pamoja na mitetea mikubwa ilipomuona kifaranga huyu anajaribu kuruka walimfata na kuanza kumdonoa. Walimdonoa hadi akapata majeraha makubwa kwenye mbawa zake.

Kwanini walimdonoa? Kwasababu alikuwa anajaribu kufanya kitu ambacho hakijawahi kufanywa na kuku. Hivyo kuna jogoo walimpiga kwasababu waliona huyu dogo anataka kutuaibisha.

Maskini huyu Tai aliumizwa sana na mwisho wake akashindwa kabisa kuruka tena. Akabakia anaishi maisha ya kuku.

Hadithi hii inatufundisha nini?

Tumezaliwa na Uwezo Mkubwa na Ukuu ndani yetu lakini tupo katikati ya watu waliokwisha kukata tamaa na wasioamini tena.

Sisi ni kama kifaranga cha Tai kilichozaliwa katikati ya kuku, hatupaswi kuwa kuku bali kuwaonesha kuku kwamba inawezekana kuruka juu.

Wapo watakaotuzuia, watakaotutenga, watakaotusema vibaya lakini hatupaswi kuruhusu kuumia au kukata tamaa na Kukubaliana nao.

Wanaweza kuwa Rafiki zako, wazazi wako, watu unaowaamini sana. Watakuja wakwambie hizo Ndoto ulizonazo haziwezekani. Kamwe Usikubali kuyumba endelea kusimamia unachokiamini.

Pamoja na kuumizwa tusikubali kukata tamaa, turudi upya uwanjani tupambane ili tupate ushindi. Tumetumwa kushinda, tusiondoke uwanjani bila ushindi.

Rafiki Yako Kocha Jacob Mushi.
www.jacobmushi.com/kocha

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading